Binti darasa la 7 ajiingiza kuuza mwili ili kununua pedi

29Jun 2020
Neema Emmanuel
MWANZA
Nipashe
Binti darasa la 7 ajiingiza kuuza mwili ili kununua pedi
  • "Mabadiliko ya binti yangu ni ya gafla mno naweza sema marafiki ndio wanaompotosha mwanangu mwanzo hakuwa na tabia mbaya alikuwa anajiheshimu anapenda kusoma Biblia  muda wote lakini alikuja kubadilika gafla mtaani wananisema sana....

"Maisha ni mtihani na Safari ndefu natamani kupata kitu nakosa watu wasio na huruma na utu wanatumia nafasi hiyo kunirubuni kwa shilingi elfu mbili ili wakipate wanachokiitaji,"....

Ofisa tarafa ya Ngudu wilaya ya Kwimba, Hamza Hussein Hamza akizungumza na mwandishi wa habari hii (hayupo pichani).

Hiyo ni kauli ya Lucy Nestory (siyo jina halisi) mwenye umri wa miaka 13 mwanafunzi wa  darasa la saba katika shule moja ya msingi iliyopo wilayani Kwimba Jijini Mwanza.

Mwandishi wa The Guardian Digital na Nipashe, Neema Emmanuel alikutana na binti huyo na kumsimulia masahibu anayokutana nayo kila kukicha, kutokana na ugumu wa maisha uliopelekea kujiingiza katika biashara ya kuuza mwili wake kwa gharama ya shilingi elfu mbili ili kumuwezesha kupata fedha za kununua baadhi ya mahitaji yake ikiwemo taulo za kike na kuhudumia familia yake.

Anasema kuwa yeye ni mtoto wa nne kuzaliwa kati ya watano ambapo baba yake mzazi amefariki dunia akiwa mtoto huku mama yake akiwa ni muhathirika wa virisi vya Ukimwi anayetegemea riziki yake kwa kujishughulisha na shughuli za kilimo kijijini hapo.

Lucy, anaeleza kuwa alijiingiza katika maisha hayo ya kuuza mwili wake akiwa darasa la sita baada ya siku moja kukosa pesa ya kununua taulo ya kike alipokuwa kwenye siku zake na ndipo alipopokea ushari kutoka kwa rafiki zake wakimueleza namna mahusiano ya kimapenzi yalivyo mazuri.

"Baadhi ya marafiki zangu ambao wapo kidato cha nne na mwingine darasa la saba walinionyesha picha za ngono kupitia simu zao  za mkononi na walikuwa wakiwasifia wapenzi wao na walidai wanawapatia mahitaji yao vyema, nilivutika na kujiingiza kwenye hiyo tabia mbaya, nikamzalau mama yangu, nyumbani nilijihusisha kimahusiano na watu wazima lakini sasa hivi najuta..nahitaji kuwa mtoto mwema nifikie malengo yangu na kutimiza ndoto nije kumsaidia mama yangu "ameeleza Lucy huku akiinamisha kichwa chake chini.

Anasema kuwa moja ya mbinu alizokuwa akitumia kupata pesa ni pamoja na kusingizia mama yake kuwa ni kipofu ili kuwashawishi wanaume kumpatia pesa huku wengine wakimtaka kufanya nae mapenzi ili wampatie msaada ho.

MAMA AELEZA

Mama yake Lucy ambaye akutaka kutaja jina lake, anasema kuwa mabadiliko ya mtoto wake yalianza mwaka jana na amechukua hatua mbalimbali za kumkanya ikiwamo kumchapa, kumfungia nje na kushirikisha ndugu na marafiki kumkanya mtoto wake.

"Mabadiliko ya binti yangu ni ya gafla mno naweza sema marafiki ndio wanaompotosha mwanangu mwanzo hakuwa na tabia mbaya alikuwa anajiheshimu anapenda kusoma Biblia  muda wote lakini alikuja kubadilika gafla mtaani wananisema sana lakini nikawa na imani atabadilika na kuwa mtoto mwema, darasani alikuwa anafanya vizuri sana  lakini gafla matokeo yakaanza kushuka,nishamfungia nje, sema kuna siku aliwahi kuniomba hela akanunue taulo ya kike (Pedi) sikuwa nayo nahisi ndio akaamua kubadilika," amesema 

Amesema kuwa mara kwa mara amekuwa akimpatia mtoto wake elimu ya makuzi na athari za kujiingiza kwenye mahusiano akiwa na umri mdogo.

Amesema kuwa kati ya watoto wake wote Lucy ndiyo alikuwa na tabia tofauti na wenzake huku akiwa na imani kuwa elimu aliyopewa na Ofisa Tarafa ya Ngudu, wilayani Kwimba, Hamza Hussein Hamza imemjenga na kumbadilisha na kuonyesha nuru na mafanikio ya mbele kwa mtoto wake.

VIONGOZI WA DINI & WADAU 

Mchungaji wa Kanisa la Pentecostal Assemblies of God Tanzania (P.A.G.T) Ngudu,  Elias Shileka,  amesema suala la watoto wenye umri wa miaka 12 hasa wa kike kujiingiza katika mahusiano limekuwa tatizo kubwa lenye kuleta mmomonyoko wa kimaadili katika jamii na kusababisha kukatishwa masomo kwa kudanganywa na vitu vidogo.

"Unakuta mzazi anampa uhuru uliopitiliza mtoto, lakini wakati tulionao ni wakuomba na kuwatanguliza watoto katika maombi yao ili tuwe na kizazi kilichochema na kimpendezacho Mwenyezi Mungu" amesema Mchungaji Shileka.

Naye Ofisa Tathimini na Ufuatiliaji Mradi wa Boresha (TIP) Kwimba, Hamisi Kibayasi, amesema kuna baadhi ya mambo ikiwemo umaskini katika baadhi ya jamii kuwatumia watoto kama chanzo cha kuwaingizia kipato mambo ambayo uchochea mtoto kujiingiza kwenye mahusiano mwisho wa siku kufanyiwa vitendo vya kikatili.

Amesema kuwa wakati umefika wa jamii kupewa elimu ya kutosha kuhusiana na masuala ya ukatili dhidi ya watoto kwani wapo wanapofanyiwa pasipo wao kujua elimu ya ukatili ikianza kutolewa kuanzia ngazi mashuleni itasaidia kuondokana na adha hizo.

"Sisi tumekutana na kesi nyingi zinazowahusu watoto kufanyiwa ukatili lakini Shirika letu limeanza kutoa elimu kwa watoto ambao wapo Shule ya Jumapili 'Sunday School' na Madrasa tunawaelimisha walimu nao wanatoa kwa wanafunzi lengo elimu hiyo iweze kufika chini na itawasaidia watoto kujitambua na kujua ukatili ni nini ,tunapendekeza elimu hii ianze kutolewa mashuleni itawasaidia watoto kutambua ukatili ni nini, kujikinga, kujiepusha na kuondokana na ukatili," amesema Kibayasi

Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Senyi Ngaga akielezea namna wanavyopambana na changamoto ya mimba za utotoni.

MKUU WA WILAYA ANENA 

Mkuu wa Wilaya Kwimba, Senyi Ngaga akizungumzia matukio hayo ya watoto kwenda kinyume na maadili amesema wanajikita kutoa elimu kwa watoto wa kike ili kuleta mabadiliko yenye tija na kuondokana na changamoto za mimba za utotoni katika wilaya hiyo.

OFISA TARAFA AFUNGUKA 

Naye Ofisa Tarafa ya Ngudu, Hamza Hussein Hamza, amesema changamoto kubwa zilizopo kwenye tarafa hiyo ni sakata kubwa la wanafunzi ni kujihusisha na masuala ya mahusiano ya kingono jambo amablo linatokana na wazazi kutochukua wajibu wao.

Amesema kuwa chanzo kikubwa ni utandawazi,tamaa ya watoto hao inayochangiwa na kukosa mahitaji yao ya msingi ikiwemo nguo na taulo kike sambamba na kununua vyakula hivyo kupelekea wao kushawishika kwa vitu vidogovidogo.

" Huyo binti alikuwa ananikimbia kila ninapokutana naye kwa sababu ninawakamata na nimempa elimu na ameahidi kubadilika na natumaini atabadilika mwanzo alinidanganya mama yake ni kipofu na inamlazimu kufanya tabia hiyo ili kuudumia familia siku choka kufatilia na ndipo nikabaini ukweli na niliongea naye akanieleza kila kitu na sitochoka kumfatilia na kuwafatilia watoto wengine tunaitaji kuwa na watoto wakike wasomi na wenye kushika nafasi mbalimbali katika uongozi hakika sitochoka kupambana na hili " amesema Hamza 

Ameongeza kuwa moja ya mikakati yao ni kutoa elimu kwa jamii sambamba na kufanya msako kwa wale wanaowashawishi watoto wanakamatwa na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria pamoja na kuangalia namna gani vijana wanaojihusisha na masuala hayo.

Habari Kubwa