Bomoabomoa mpakani inavyowatia kiwewe wakazi wakongwe Rombo

29Jun 2017
James Lanka
ROMBO
Nipashe
Bomoabomoa mpakani inavyowatia kiwewe wakazi wakongwe Rombo
  • L Nyumba zatiwa ‘X’; DC anena ni sehemu ya ‘hapa kazi tu’

MEI 5 mwaka huu, ilikuwa tarehe ya msukosuko kwa baadhi ya wakazi wa eneo la Tarakea Mjini wilayani hapa, timu ya askari na maofisa wa serikali wakifika katika baadhi ya nyumba, wanapima uhalali wao katika maeneo jirani na mpaka.

Hiyo iliendana na baadhi ya nyumba kuwekewa alama ‘X’ na baadhi ya bomoabomoa kuwafika ndani ya wiki moja.

Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Agness Hokororo, anafafanua kuhusu tukio hilo kuwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais Dk. John Magufuli, kuhusu ‘kusafisha’ mipaka yote ya nchi, kwa sabaabu za kiusalama na kuzuia biashara za magendo.

“Kwa mfano katika wilaya yetu ya Rombo ambayo iko mpakani, kuna eneo linaitwa ‘White House.’ hapo imegundulika kuwa biashara nyingi za magendo zinafanyika hapo na nyumba zote hapo zimejengwa kwenye ‘bicorn’ (vyuma vya mpaka) kabisa, jambo ambalo ni hatari kiusalama na hata kiuchumi,” anasema Agness.

Mkuu huyo wa wilaya, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya Rombo, anasema kilichofanyika ni tathmini ya kujua idadi ya nyumba zilizojengwa ndani ya eneo lisiloruhusiwa kisheria mipakani.

Anaainisha eneo halali la kujenga kisheria ni umbali wa mita 50, kutoka zilipo alama za kimataifa za mipaka. Anaongeza:

“Baada ya tathmini hiyo kukamilika na kajadiliwa katika ngazi ya wilaya, tumeshaiwasilisha kwenye Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa chini ya Mwenyekiti wake, ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro (Wakati huo Saidi Mecky Sadick) kwa nafasi yake.”

Kuhusiana na hatua zaidi za kuchukuliwa, Agness anasema bado majadiliano yanaendelea, kabla ya kuchukuliwa hatua.

Kutoka kwa waathirika

Theresia Ndeng’aso, mkazi wa kijiji cha Kikelewa katika Kata ya Tarakea Motamburu, Rombo anasema alipogiwa simu na familia yake nyumbani, kuambiwa nyumba aliyoachiwa na marehemu mumewe, imo katika orodha ya bomoabomoa.

Anafafanua kwa hoja: “Maofisa wa serikali wakipima eneo ilipo nyumba ya familia yangu na kuwaambia watoto waliokuwa ndani kuwa, nyumba yangu niliyoachiwa na marehemu mume inapaswa kubomolewa ndani ya siku saba kwa kuwa imejengewa mpakani.”

Ni utekelezaji uliotanguliwa na habari zilizozagaa kwamba, inawahusu wakazi wanaoishi maeneo ya mpaka wa Kenya na Tanzania, kuanzia Tarakea hadi Holili, wilayani Rombo.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, wakazi wanaodaiwa kujenga ndani ya mita 50 kutoka zilipo alama maalumu za mpaka kimataifa zilizojengwa kwa zege tangu zama za ukoloni, walitakiwa kubomoa nyumba zao ndani ya siku tatu hadi saba, kwa mahali hapo ni eneo la ardhi ya kimataifa.

Ushuhuda wa mwandishi wa makala hii katika kijiji cha Kikelewa, nyumba kadhaa zilizoko jirani na mpaka wa kuingia Kenya, zilikuwa zimewekewa alama ya ‘X’ na kuna baadhi ya nyumba zilizokuwa na maandishi ‘bomoa.’

Mkazi Theresia, mmoja wa waathirika wa mwanzo anakiri ni hatua inayochukuliwa dhidi yao na hajui, hatima yao.

“Nakumbuka mwaka 2012, walikuja maofisa wa serikali na kupima eneo la mpaka na kutuambia kuwa tunaweza kufanya shughuli zetu za kimaendeleo umbali wa mita 25 kutoka katika ‘bicorn’(vyuma) na wamekuwa wakija kila mara kufanya usafi eneo la wazi la mpakani,”anasema Theresia na kuongeza:

“Ila inanishangaza sana kuwa tarehe 5 Mei mwaka huu, wamefika kijijini na kupima tena maeneo na kuongeza mita 25 zaidi ya zile za awali, hadi kufikia mita 50 ambako nyumba nyingi katika kijiji chetu cha Kikelelwa na vijiji vya jirani hadi Holili zimekumbwa na kadhia hiyo.”

“Sijui tutakwenda kuishi wapi na watoto wetu ikiwa nyumba zetu zitavunjwa,” analalama.

Anafafanua zaidi kuwa, yeye ni majane mwenye watoto sita kupitia ndoa yake na marehemu mumewe na walibahatika kujenga nyumba, ambayo sasa ina alama ‘X’ ambayo ni ishara kwamba iko katika orodha ya bomoabomoa.

Theresia anasema:“Nakumbuka kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo, wamekuwa wakija na kufyeka hata mazao mashambani katika eneo la mita 25.”

Anasimulia kuwa siku hiyo Mei 5, 2007, waliwavamia kwenye makazi yao bila ya taarifa na kuanza upimaji, wakiambatana na askari wa usalama wakiweka alama ‘X’ katika baadhi ya nyumba.

Theresia:”... wakitutaka tubomoe ndani ya siku tatu hadi saba, pasipo kulipwa fidia. Hivi wanataka tukaishi wapi na sisi tumekulia hapa zaidi ya miongo mitatu hadi mitano?”

Mzee Evarist Lebayi (89), mkazi wa kijiji cha Kikelelwa, anasema ameishi kijijini hapo kwa zaidi ya miaka 50, lakini anashangaa ghalfa wanatakiwa kuwa hawapaswi kufanya shughuli zozote za kimaendeleo ndani ya umbali chini ya mita 25 kutoka katika alama ya mpaka ya kimataifa.

“Mimi nakumbuka tarehe 5 Mei, mwaka huu, nilivamiwa nyumbani kwangu pasipo taarifa yeyote na mapolisi wakiwa na silaha kali za kivita, pamoja wakiongozana na maofisa wa serikali.

“Walipima kwa kutumia futi kamba kutoka kwenye bicorn (chuma) na kuniambia nyumba zangu zote ziko kwenye eneo la mita 50.

“Hivyo, zinatakiwa kubomolewa haraka ndani ya siku saba na kuzipiga alama ya ‘X’ zote kwa rangi nyekundu…” alisimulia Mzee Lebayi kwa masikitiko makubwa.

Mwathirika mwingine, Mzee Steven Shirima, anaeleza mkasa wake kwamba ‘alivamiwa’ nyumbani kwake tarehe 5 Mei mwaka huu, saa saba 7.00 mchana alipokuwa akipaua nyumba yake.

Anasimulia kwamba maofisa hao wa kiserikali walifika na kupima umbali wa mita 50 kutoka ilipo ‘bicorn’ na walimuamuru abomoe sehemu ya nyumba zake ndani ya siku saba.

“Nilishtushwa sana na zoezi hilo ambalo lilikuja pasipo kupewa ‘notice’(taarifa) yoyote na sehemu ya nyumba kupigwa alama ya ‘X’ na kuandika maandishi yanayosomeka ‘Bomoa.’

Anasema siku walizopewa zimeshakwisha na kwa sasa wanasubiri, huku akidokeza ni kiwanja alichoachiwa kupitia urithi kutoka kwa baba yake.

Mwathirika mwingine, Vicent Tivai, anajitambulisha kuwa mzaliwa wa Kikelelwa na kwa sasa anafanya kazi Dar es Salaam,naye nyumba na shamba lake imewekewa alama ‘X.’

Anaongeza kwamba, tayari ameshaandika barua ya malalamiko kwa: Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Mkuu wa Wilaya ya Rombo; na Mkuu wa Mkoa, ili apatiwe ufafanuzi kuhusiana na hatua hiyo iliyochukuliwa ghafla dhidi yake.

Mwenyekiti wa Kijiji

Mweyekiti wa kijiji cha Mbomai, ambako nako kumeathiriwa, anasema ni hatua inayogusa zaidi ya kaya 120 katika vijiji vya Kikelelwa na Mbomai na hajui hatima ya wananchi wa maeneo hayo.

Anataja baadhi ya maeneo anayofahamu kuguswa na operesheni hiyo, ni kuanzia Kata za Tarakea, Motamburu hadi Holili, wilayani humo.

Mwandishi wa Makala haya anapatikana;kwa anwani ya barua pepe: [email protected] na simu:

+255 752 691 129

Habari Kubwa