Bosi Sido asimulia sura mpya kuelekea Tanzania ya Viwanda

03Nov 2017
Yasmine Protace
Nipashe
Bosi Sido asimulia sura mpya kuelekea Tanzania ya Viwanda
  • Asema nao wamo katika mikopo, majukumu ya Veta

HIVI sasa taifa liko katika msisitizo wa kuhamasisha uanzishwaji na uendelezaji viwanda, kukiwapo njia na mbinu mbalimbali za kufanikisha malengo.

Katika kuhakikisha Watanzania wananufaika na kuboresha maisha yao, Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), limeweza kutoa huduma za kiteknolojia zitakazowezesha kunufaisha biashara.

Meneja Huduma za Kifedha wa Sido, Haika Shayo, anasema pamoja na kuhudumia viwanda vidogo na biashara ndogo, wanawapatia wafanyabiashara elimu ya teknolojia katika nyanja mbalimbali za kuwanufaisha.

Anasema, pia wamekuwa wakiwaelimisha wafanyabiashara aina za biashara wanazopaswa kuzifanya na matumizi ya mashine na vifaa mbalimbali stahiki.

Haika anasema elimu imekuwa ikitolewa kwa wafanyabiashara wafanye biashara katika maeneo yanayofaa, pia kujenga majengo bora.

“Kuwasaidia wafanyabiashara kufanya biashara katika maeneo yaliyo bora, hali hiyo inawawezesha hata pia kuwasaidia kupata mikopo kutoka taasisi mbalimbali,” anasema.

Anaongeza kuwa, Sido ilyoanzishwa mwaka 1973, kupitia Mpango wa Pili wa Maendeleo nchini ya mwaka 1969 – 1974, imekuwa ikisaidia kuwashauri wafanyabiashara wenye uwezo wa kutengeneza bidhaa, ili wazalishe bidhaa kwa wingi.

Hadi sasa Sido ina ofisi katika kila mkoa nchini kutimiza majukumu yake hayo kwa maendeleo ya viwanda vidogo.

Mlango wa masoko

Haika anasema, huduma za mafunzo ya ujasiriamali na uwekaji lebo katika bidhaa, ni sehemu ya mbinu za kuwasaidia wazalishaji kukuza ubora katika kiwango kinachokubalika.

Anasema huduma za masoko na habari, ni lengo linalowasaidia wajasiriamali kufikia masoko yenye faida kitaifa na kimataifa.
Lingine analolitaja ni kuwapeleka katika Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa au maarufu kama Sabasaba, yanayofanyika kila mwezi Julai ya mwaka, jijini Dar es Salaam.

Aidha, vivyo hivyo inafanyika katika maonyesho mengine ya ndani na nje ya nchi, hata ikifika mbali hata kuwawezesha wafanyabiashara wa ngazi tofauti kutambulike katika maeneo mbalimbali na bidhaa zao wanazozalisha.

Anasema mbali na kuwasaidia kushiriki katika masoko ya ndani na nje ya nchi, pia wanawasaidia wajasiriamali hao kuwa na vipeperushi vinavyoonyesha biadhaa wanazozalisha.

“Pamoja na kuwawezesha katika kuwapatia vipeperushi, pia wamekuwa wakiwapatia mafunzo ya kufungasha bidhaa zao, ikiwamo kuwashauri rangi za kuweka pamoja na lebo ikiwa na maandishi kuelekezwa jinsi ya kuyaweka,” anasema.

Haika anafafanua kuwa, ili wajasiriamali hao waweze kunufaika na bidhaa na ubora wake, wanawasaidia kutengeneza bidhaa ubora vinavyokidhi viwango vya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA).

Huduma za kifedha

Anasema utaratibu wa Sido, inatoa mkopo kwa mtu mmoja mmoja na hata vikundi vya uzalishaji vinavyokidhi vigezo vyake.

Haika anafafanua namna mikopo hiyo inavyotolewa, kwamba kabla ya walengwa kupatiwa mikopo, inaanza mafunzo maalum ya kuwasaidia kujua mambo muhimu wanayotakiwa kuzingatia, ili wanufaike na mikopo watakayoichukua.

Anasema, pia Sido imekuwa ikiwaunganisha wajasiriamali na taasisi mbalimbali za kifedha, ili wanufaike na mikopo isiyo na masharti magumu.

Haika anasema kutokana na Sido kuwa mdau mkubwa katika kuwaendeleza wadau kupigana na umasikini, wameshashiriki katika siku ya ‘Vikoba Day’ ikiwa namna ya kuonyeha njia rafiki ya kuwakutanisha wajasiriamali kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Haika anasema kuwa mikopo yao ya kuwasaidia wajasiriamali, vigezo vyao ni kuangalia biashara, pesa zinazohitajika na kutoa mafunzo maalum.

Anasema, hata mkopaji anapokwama kulipa, hawakimbilii kumtaifisha mali zake, bali wanachoangalia ni kuainisha na kufanyia kazi sababu zilizomo kwa kurejesha fedha za deni.

Haika anasema, hiyo ndiyo inayosaidia kufahamu namna ya kusaidia kama mfanyabishara akishindwa kurejesha mkopo. Pia, inaelezwa pindi mhusika anaposhindwa kutoa taarifa, ndio hatua kali huchukuliwa kuhusu kurejesha deni hilo.

Changamoto

Haika anasema kuna ufinyu wa fedha za kutoa mikopo iliyoanza mwaka 1994 na tangu kipindi hicho hadi mwaka huu, maombi ya mkopo yaliyowasilishwa ni 214 yaliyohitaji Shilingi bilioni 165, kukidhi yote.

Lakini, inaelezwa hadi Juni 2017 iliyopita, kiasi cha Shilingi bilioni 63 kilishatolewa na serikali kwa watu 86.

Anasema kumekuwepo changamoto katika fedha na hali hiyo imechangia watu wachache kupata mikopo.

Haika anasema katika kukabiliana na changamoto, wanaendelea kuiomba serikali iwasaidie, ili mfuko uendelee kuwanufaisha wajasiriamli hao.

Bosi huyo wa Sido, hata hivyo anakiri kuwa serikali ina majukumu mengi na imekuwa ikishindwa kuwasaidia, ingawaje haiwakatishi tamaa kuendelea kuiomba iwasaidie kutimiza malengo ya kuboresha maisha ya wajasiriamli nchini.

Haika anasema katika kipindi cha mwaka 1994, zilitengwa Shilingi milioni 800, lakini hadi Juni iliyopita, walipewa Shilingi milioni 500 na kwa jumla wameshapokea Shilingi bilioni tano.

Anasema fedha wamekuwa wakizungusha na kuongeza kuwa asilimia 50 zinarudi katika mfuko ambako mpaka Juni mwaka huu, wameshazalisha Shiingi bilioni saba.

Haika anaendeleza simulizi yake kuwa, mikopo wanayoitoa ni katika biashara zote na kisheria katika sekta ya huduma za uzalishaji.

Anasema katika uzalishaji, asilimia 78, inatolewa katika sekta hiyo na viwanda vinachukua asilimia 34 na ndio sababu inayowafanya wahamasishe kuanzishwa viwanda mjini na vijijini, ambako wamepokea asilimia 31 ya mikopo.

Haika anasema, katika masuala ya mikopo, wanawake awali walikuwa nyuma katika kuomba mikopo, lakini sasa uwiano ni wastani wa ‘nusu kwa nusu’ kwa jinsia zote.

Sura ya mikopo

Haika anasema kuwa, wamekuwa wakitoa kuanzia kiwango cha Shilingi milioni sita na wateja wanaweza kuomba hadi Shilingi milioni 100.

Anasema, kupitia taarifa ya utekelezaji mwaka wa fedha 2016/2017 serikali kupitia bajeti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Shilingi bilioni 2.4 kwa ajili ya kukuza mtaji wa mfuko. 

Haika anakiri kuwapo changamoto mbalimbali zilizoikabili bajeti ya serikali, hadi kufikia Juni 2017, fedha hizo hazikuweza kupatikana kama ilivyopangwa.
 
Anafafanua kuwa, kukosekana nyongeza hiyo ya mtaji katika mfuko, imeifanya Sido ishindwe kufikia malengo yake kwa mwaka huo wa fedha - 2016/2017.

Kupitia wastani wa matarajio ya mkopo wa Shilingi 1,480,119.20 kwa kila mwombaji, ilitegemewa kutolewa jumla ya mikopo 1,621 kwa wajasiriamali na kuzalisha ajira mpya 4,387 kwa wastani wa kila ajira kutoa ujira wa Shilingi 547,078.65, kila mkopo ukizalisha ajira tatu.

Kwa kutumia mtaji uliopo, kwa kipindi cha mwaka 2016/17, Shirika lilipokea  jumla ya maombi 9,773 yenye thamani ya Shilingi 13.3 bilioni kutoka kwa Wajasiriamali Wadogo kwenye mikoa 22 ya Tanzania Bara. Hata hivyo, jumla ya maombi 4,112 yenye thamani ya Shilingi bilioni sita, ililiyotolewa hadi kufikia mwezi Juni 2017.  Idadi ya mikopo iliyotolewa ni sawa na asilimia 42 ya maombi yaliyopokewa.

Aidha, jumla ya maombi ya mikopo yaliyopokewa, asilimia 46.1 ilitolewa mikopo.

Haika anasema, kuna mpango endelevu katika sekta ya mafundi ukiwa na lengo la kukuza viwanda vidogo vipate teknolojia na huduma za kifundi, ili kuongeza ajira, kujenga uchumi na kupunguza umasikini.

Anasema walengwa wa mpango huo, ni vijana wanaoishi vijijini na mjini, wanawake na walemavu wa viungo, wanaoweza kuzalisha bidhaa au kutoa huduma za kiufundi, kulingana mahitaji ya wateja.

Hilo linafanyika kwa kutumia teknolojia rahisi zinazoendana na rasilimali za maeneo husika.

Habari Kubwa