CCM inahitaji Katibu Mkuu wa aina gani?

25May 2016
Restuta James
Dar es Salaam
Nipashe
CCM inahitaji Katibu Mkuu wa aina gani?

KATIBU Mkuu wa taasisi, kama vile chama cha siasa katika muundo wa kawaida huwa ndiye mtendaji mkuu wa shughuli za kila siku.

Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana

Majukumu yake yanajumuisha mambo kama utekelezaji wa maamuzi na maagizo yanayohusu chama, ubunifu na usimamizi wa uendeshaji wa shughuli za kila siku katika kufikia malengo ya taasisi husika.

Kwa maana hiyo, ana nafasi kubwa sana katika kuunda au kuzalisha ubora wa taasisi.

Hivyo, chama cha siasa asilimia kubwa ya uhai wake imejishikiza katika ubora wa utendaji wa Katibu Mkuu, jambo linalofanya mara nyingi Makatibu Wakuu wa vyama hawawi wanasiasa zaidi na badala yake wanakuwa watendaji.

Hata muundo wa vyama vingi anaingia katika kundi la watumishi wanaolipwa mshahara ili awe na muda wa kutosha wa kuwajibika kwa kina.

Ni dhahiri kuwa ubunifu, presha na mwenendo wa siasa za dunia hivi sasa zinaongeza sifa ya ziada ya Katibu Mkuu hasa wa vyama vya siasa.

Kwamba watendaji hawa wanaweza kuoana na matakwa ya siasa za sasa hasa kuhimili kundi la vijana na purukushani zinazoendelea kwenye mitandao ya kijamii kuanzia whatsapp, instagram, facebook hadi twitter.

Katibu Mkuu ambaye ataweza kulikusanya kundi la vijana ambao wamepoteza matumaini na vyama vya siasa kikiwamo Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho kwa mwenendo wa uchaguzi mkuu wa mwaka jana, walionekana kuunga mkono zaidi upinzani.

Vijana waendesha bodaboda, mama lishe, waendesha mikokoteni na wenye elimu ya kati na walio vyuo vikuu walionyesha dhahiri kukerwa na mfumo wa utawala, hivyo mhemko mkubwa ukawa kutaka mabadiliko; ambayo waliamini yangetoka nje ya CCM.

Wadadisi wanaelewa kwamba uchaguzi wa mwaka jana ulikuwa na presha kubwa ya mabadiliko na kila mgombea kwa nafasi yake alikuwa akinadi mabadiliko kiasi cha vyama kama Chadema kilishutumu CCM kwa kuiba nembo yake ya M4C yaani Movement for Change ambayo ilitumika kumnadi Rais John Magufuli (Magufuli for Change –M4C).

Msukumo huo wa kisiasa ni ama umevilazimisha baadhi ya vyama vya siasa kama Chadema, The National Alliance (TNA) na Orange Democratic Movement (ODM), vya nchini Kenya kulazimika kuzingatia matakwa ya wakati na kuwa na Makatibu Wakuu wenye umri wa kati.

Mathalani, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji, ana miaka 43 akiwa ni mtendaji mkuu wa chama ambacho kina nguvu zaidi nchini hata baada ya kuungana na vyama vingine vya siasa. Kitaaluma Dk. Mashinji ni daktari bingwa wa magonjwa ya binadamu.

Katibu Mkuu wa ODM, Ababu Namwamba, ana miaka 41 na ni mwanasheria mbobezi wakati yule wa TNA ambacho ni chama cha Rais Uhuru Kenyatta, Onyango Oloo, naye ana umri wa kati na pia ni wakili mzuri na mwanaharakati.

Pamoja na suala la uzoefu ndani ya chama kuna moja ya kigezo muhimu, lakini mazingira ya sasa ya siasa yanaongeza vigezo.

Wadadisi wa mambo wanaangalia utendaji wa Rais John Magufuli, misimamo yake katika kubadilisha uchumi wa nchi hasa suala la viwanda na kuona kwamba anahitaji mtendaji mkuu wa chama mwenye kuona Tanzania ya Magufuli kiuchumi, kisiasa na kijamii lakini pia kwenye anga za kimataifa kikanda kwa kushirikiana na majirani, Afrika na nje ya bara hili.

Hata hivyo, Mhadhiri na mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Dk. Azavel Lwaitama, anasema umri siyo kigezo pekee kwa uteuzi wa Katibu Mkuu wa CCM, bali kinachotakiwa ni kuweka kada ambaye atajielekeza kukijenga chama badala ya kulumbana na upinzani.

“Katibu Mkuu ataweza kufanya vizuri kama tu atakuwa amebeba matumaini ya wengi ambayo yamepotea. Siyo Katibu Mkuu wa kulumbana na Lowassa au upinzani,” anaonya.

Anasema uchaguzi wa mwaka jana ulionyesha hasira na hisia kila kuanzia wafanyakazi, vijana, wanawake na wazee ambao kwa kiwango kikubwa walikuwa wanadai mabadiliko, hivyo hata Katibu Mkuu ajaye wa CCM anapaswa kuzingatia hitaji hilo. Alete mabadiliko ya kweli, yanayoboresha na kuinua maisha ya Watanzania.

Awe mtu anayejua kile watu wanachotaka ambacho ni usimamizi bora wa majukumu na kufanyakazi kwa uadilifu, kuhakikisha haki za binadamu zinazingatiwa na taifa linaongozwa kwa misingi ya kisheria na kuthamini utu wa mtu bila kujali dini, itikadi au rangi.

“Umri siyo jambo la msingi sana…ni kuangalia kiongozi kama huyu (Katibu Mkuu), amebeba matumaini ya nani? Kwa sababu Dk. Wilbrod Slaa, alikuwa anapendwa sana na vijana pamoja na watu wengine, lakini alikuwa mzee…alikuwa anabeba matumaini ya watu wengi,” anasema.

Anaeleza kuwa hata baada ya Dk. Slaa kuondoka Chadema, vijana na watu wa kada mbalimbali bado wameonyesha kukiamini chama hicho, kwa kuwa kimebeba matumaini ya kuleta mabadiliko.

“Utaona hoja ni kwamba nani anabeba matumaini ya akina nani au anajenga chama kinachobeba matumaini ya watu gani. Anaweza kuwa mzee au kijana na akakubalika kutokana na misimamo yake,” anasema.

Anasema hata Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, alipoondoka CCM na kujiunga Chadema, aliendelea kupendwa kwa sababu alionekana kubeba ajenda za kuwasaidia watu wengi.

Dk. Lwaitama anamtaja Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere pamoja na Mwasisi wa Taifa la Afrika Kusini, hayati Nelson Mandela wanapendwa na vijana pamoja na watu wengine kutokana na kwamba uongozi wao ulibeba matumaini ya vijana wa wakati wao na wa kizazi kilichofuata.

“Kwa hiyo Katibu Mkuu anatakiwa awe na sifa za kuweza kukisaidia kizazi cha sasa na vingine vijavyo siyo Katibu Mkuu wa kuja kulumbana na Lowassa,” anasema.

MAKATIBU WAKUU CCM
Makatibu wakuu wa CCM waliopita ni Pius Msekwa, Rashid Kawawa, Horace Kolimba, Lawrence Gama, Philip Mangula, Yusuf Makamba, Wilson Mukama na sasa Abdulrahiman Kinana.

Habari Kubwa