CCM ndege inayopaa...Je, itatua tena 2020 ?

19Mar 2017
Mwinyi Sadallah
Nipashe Jumapili
CCM ndege inayopaa...Je, itatua tena 2020 ?

NAIFANANISHA CCM na ndege inayosafiri ambayo tayari imebeba abiria, imepakia shehena, ina akiba ya mafuta na rubani amekalia kiti, akiwa na ahadi sitawaangusha!

Wana CCM wamejifunga mikanda na matangazo ya kujiokoa endapo ajali itatokea yanaanza kutolewa. Hapa matairi ya ndege yamekanyaga mstari tayari kupasha moto injini ikizunguka kwenye njia yake mara kadhaa kabla ya maofisa wanaosimamia usafiri wa anga kuiruhusu kupaa.

Wakati wowote chombo hicho kitapasua anga na kufika kiendako.Ndege hii yenye abiria waliovalia sare zenye rangi ya kijani na njano, bendera zao zikiwa na alama ya jembe na nyundo , kila mmoja amekamata nakala ya marekebisho ya katiba ya chama hicho tawala.

Inapopaa wanaanza kujiuliza maswali kadhaa kama ugumu wa safari hii angani yenye mabonde, milima mirefu , dhoruba, upepo , bahari, mito na maziwa makubwa ya kuvuka.

Je abiria wote hawa wamejitathimini, wamejipima, kujichambua na kujihakikishia kuwa wako katika safari moja, yenye malengo sawa pamoja na madhumuni na dhamira ni ile moja?.

Wameshajiuliza kama wote wana hati za kusafiria , wamepatiwa visa, wana akiba ya pesa za kigeni za kutosha za matumizi ya nchi za kigeni waendako ,mizigo yao imepekuliwa .

Hakuna anayemtilia shaka na kumshuku abiria mwenzake kwa masuala yoyote aidha iwe ya usaliti, uasi, unafiki , ugaidi au uharamia?

Kama nilivyosema safari hii ni ndefu ilianza tangu nyakati za harakati za kupigania uhuru wa mataifa ya Tanganyika na Zanzibar , ilikuwa chini ya manahodha wake Mwalimu Julius Nyerere na Alhaji Abeid Amani Karume.

Vyombo vilivyoanza kutumiwa vikiitwaTAA, baadaye TANU na ASP ambavyo viliungana kuunda Chama Cha Mapinduzi.

Katika mwanzo wa safari hii mpya kuna taswira inayoonyesha kuyumba na mvumo wa tufani, upepo mkali unaoambatana na mvua za rasharasha na manyunyu yanayoleta ubaridi unaopenya kwenye ngozi kwa kasi.

Yapo madai ya kujitokeza usaliti, uasi, na umangimeza. Je abiria hawa katika safari hii ndefu na mpya ambayo kwao inaoongozwa na jemadari wake mpya, Mwenyekiti wake Rais John Magufuli, wana hakika wa kuvuka mawingu mazito yaliyotanda angani na ndege yao iweze kushuka na kutuma salama ardhini?.

Dunia ya CCM mpya iliyobadilisha katiba Dodoma juzi ni moja kati ya sayari zinazoelea angani Tanzania. Je chombo hiki kipya kitarajiwe kitashuka katika sayari ipi kikiwa salama?

Kitazitembelea zote Neptune, Mars, Pluto, Saturn, Jupiter au Venus au kitakwenda moja kwa moja mwezini?

Baadhi ya makada na wanachama wake vigogo ambao ni wakereketwa mashuhuri, sasa wamevuliwa uanachama, si viongozi tena wa chama hicho tawala wametupwa kwenye sayari nyingine.

Wanashukiwa na pia wamekabiliwa na tuhuma za uasi, usaliti na ushabiki wa kisiasa unaodaiwa kuwa na lengo la kukikwamisha chombo hicho kisipae na kutulia angani kabla ya kushuka tena ardhini kikiwa salama.

Kabla ya safari hii baadhi ya manahodha wake wakuu akiwamo aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, Edward Lowass na mwenzake Frederick Sumaye pamoja na mwanasiasa mkongwe Kingunge Ngombale Mwiru, wamechupa chomboni mwaka 2015 na kujitosa baharini kwenye mawimbi ya upinzani.

Kwa upande wa Tanzania Bara upinzani ukapata nguvu mpya za ushindani wa kisiasa na kunyakua majimbo kadhaa ya uchaguzi mwaka 2015.

Iwe iwavyo mambo yamekuwa magumu kidogo kwa CCM , si rahisi na hakuna wepesi kama ilivyokuwa kabla na baada miaka 20 ya kuingia vyama vingi.

Mbele ya safari hii ya rubani mpya anayerusha ndege kwa kasi ya hapa kazi tu tayari katiba yake imefanyiwa marekebisho ya 16 tangu ilivyoandika miaka 40 iliyopita, anaonyesha kuwa na matumaini licha ya kwamba usoni kwake kuna changamoto kadhaa.

Kuna mambo mengi ya kuhofu ndani ya safari yake wapo maadui waliokomaa hasa umasikini, ujinga, njaa , maradhi, kilimo duni, uhaba wa pembejeo, maji safi na salama.

Anakabiliwa na kukithiri kwa dawa za kulevya ,ubadhirifu, ufisadi , vifo vya wazazi na watoto, Ukimwi na sasa kukimbiwa na misaada ya wahisani wakiwamo wa Marekani, ambao sasa wanakuja na sera mpya za Amerika kwanza.

Yote haya yanaweze kutatuka na kupungua ila kwanza yanahitaji azma ya umoja, malengo, dhamira, kauli moja na mwelekeo imara unaoweza kuwafanya hata abiria waliosafiri katika ndege mpya wafike wakiwa wamoja na salama.

Je kufanyika kwa mabadikiko ya katiba peke yake, kufukaza baadhi ya wanachama au kubadili sera, miongozo, kupungua kwa idadi ya vikao, wajumbe na kubana matumizi ndiko kutakoifanya ndege mpya iruke juu sana?

Hatua hizo zitaiwezesha kufika angani na kushuka salama katika uwanja wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania abiria wote wakiwa salama?

Habari Kubwa