Chama kilivyoing’ang’ania Dar, wanawake watwishwa ugombea

05Aug 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Chama kilivyoing’ang’ania Dar, wanawake watwishwa ugombea

SUALA la wanawake kuteuliwa kuwa wagombea kwenye majimbo au kata wakati wa uchaguzi mkuu, limekuwa kigugumizi kwa vyama vingi vinavyoongozwa na hofu kuwa kinamama hawatachaguliwa.

Naibu Katibu Mkuu wa ADC Queen Sendega akizungumza na wanachama hivi karibuni jijini Dar es Salaam. PICHA: MIRAJI MSALA.

Kwa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), kimeeleza kuwa kinapindua meza kwa majimbo yote ya Dar es Salaam, kwa kuweka wagombea ubunge na udiwani kuwa wanawake.

Hata hivyo, wakosoaji wake wanasema licha ya kufanya hivyo hakuna tija kwa sababu wagombea hao, hawafahamiki na chama hicho hakijulikani na wengi Bara na kwamba hakuna matumaini.

ADC iliyosajiliwa Machi 2012 na kushiriki uchaguzi wa mwaka 2015 inawataka Watanzania kuwachagua wanawake kushika nafasi mbalimbali za kuongoza taifa kwani wana sifa zikiwamo umakini na utulivu, uadilifu na uchungu kwa watoto na familia zao.

Katibu Mkuu wa ADC, Doyo Hassan, anaieleza Nipashe hayo na kuviasa vyama vya siasa kubeba jukumu la kuivusha nchi kwenye uchaguzi na kuiepusha na machafuko ya ukosefu wa amani lakini kuipa viongozi wanaochaguliwa kwa misingi kuheshimu ajenda na usawa wa kijinsia.

Aidha, Doyo anasema wanawake ni watulivu, wavumilivu na wana uwezo mkubwa wa kufanya mambo mengi kwa muda mfupi hivyo wakipewa nafasi ya kuliongoza taifa hili watalifikisha linapotaka kwenda kwa miaka michache ijayo.

“Ifike wakati Watanzania wabadilishe mitazamo na kufuta mawazo hasi kwamba kinamama hawawezi. Wanawake wamefanya vizuri sana ndani ya serikali ya awamu ya tano kwa kipindi cha miaka mitano jambo ambalo limetufanya sisi ADC kuamua kusimamisha wagombea wanawake tu kwa mkoa wa Dar es Salaam.

“Ni kutokana na imani kwamba wataijenga Dar mpya, jiji la kibiashara baada ya watu wengi kuhamia Dodoma. Ndicho tunachotaka.” Anasema Hassan.

Vile vile Katibu Mkuu wa ADC, anaona kuwa ni wakati wa vyama kutengeneza uhusino mwema na wananchi ili uchaguzi uwe huru na wa haki kwani Tanzania ni miongoni mwa nchi nne tu ambazo hazijaguswa na machafuko ya kisiasa baada ya uchaguzi.

Nakumbusha kuwa nyingine ni Namibia, Botswana, Lesotho na kwamba hilo ni la muhimu.

Hivyo ni lazima vyama vitambue umuhimu wa amani nchini na viwe na uelewa kwamba si kila anayekuchekea atakupigia kura.

“Hakuna sababu ya vurugu. Ukishindwa ukubali matokeo ya kushindwa kwa amani kwani kila aliyekushangilia jukwaani haimaanishi kwamba amekupigia kura. Watakushangilia milioni na watakaokupigia kura ni 10 pekee.” Anakumbusha mwanasiasa huyo.

KWANINI WANAWAKE?

Naibu Katibu Mkuu wa ADC, Queen Sendega, akizungumzia hatua ya kuwapitisha wanawake kuwa wagombea wa majimbo yote Dar anasema ni jambo lililokubaliwa na chama na wengi wamejitokeza.

Anaeleza kuwa katika Jimbo la Kigamboni wamejitokeza wagombea watatu na kwamba miongoni mwao yumo mwanamke naye ndiye aliyepewa jukumu la kukiongoza chama.

Anasema kinachotakiwa na chama hicho ni kuona kuwa uchaguzi unakuwa na kufanyika uchaguzi kwa huru na haki na kwamba muda wa kufanya siasa kwa wakati huu hautoshi.

Queen anaiomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi kusimamia haki kwa wagombea wa vyama vyote na kwa ngazi zote.

Anaongeza: “Ilitakiwa tupewe walau mwaka mzima wa kufanya siasa ili kila chama kinadi sera zake kwa wananchi, lakini sasa muda ni finyu mno kwa vyama visivyo na ruzuku kuwafikia Watanzania wote. Kwa mantiki hiyo, tunaiomba NEC itende haki kwa vyama vyote na kwa wagombea wa ngazi zote.” Anasema Queen.

KINACHOKWAMISHA WANAWAKE

Akizungumzia sababu za wanawake wengi kushindwa kushiriki kwenye kampeni za majimboni na kata, anasema ni tatizo la pesa.

Anafafanua kuwa wanawake wanatakiwa kuungwa mkono kwa kuwa uchaguzi ni gharama na zinahitajika pesa nyingi kwenye kampeni.

Naibu Katibu Mkuu anasema kuwa mathalani, mkutano mmoja wa kampeni kwenye jimbo kwa gharama ya chini unagharimu Sh. 500,000 nacho ni kiasi cha chini mno.

“Anatakiwa kufanya takribani mikutano 10 inamaanisha anatakiwa kujiandaa na 5,000,000 ni nyingi na bila kuungwa mkono na chama wengi wanashindwa,”

Naibu Katibu Mkuu wa ADC, anasema gharama za uchaguzi ni kubwa kama kulipa mawakala na kugharamia usafiri wao na kwamba bila kuwa na juhudi za kusaidia wanawake wagombea wataishia kuwa wasindikizaji.

Mawakala wanatakiwa kulipiwa angalau Sh. 5,000 za chakula na 10,000 posho ya kusimamia uchaguzi. Yote hayo hutegemea idadi ya mawakala katika vituo vyote.

ADC WABEZWA

Baadhi ya wagombea ambao hawakutaka majina yao yatajwe walipoulizwa na Nipashe maoni yao kuhusu uteuzi wa wanawake Dar, walieleza kuwa hawatashinda.

Mmoja wa wanachama hao kutoka kisiwani Pemba anasema si kwamba anakikejeli chama chake, lakini anachofahamu ni kwamba itakuwa vigumu kupata hata kura 10.

Akizungumzia ugumu wa kupata kura Dar es Salaam, anasema haoni kama kuna haja ya kuweka wanawake eneo ambalo hata vigogo wameangushwa na inashangaza kuona kuwa ADC haijafanya jitihada za kujitangaza kikamilifu inakimbilia kuweka wagombea Dar es Salaam.

Habari Kubwa