Changamka kupanda migomba inastawi popote

25Jun 2016
Gaudensia Mngumi
Dar es Salaam
Nipashe
Changamka kupanda migomba inastawi popote

KAMA ambavyo mboga huweza kustawi popote penye bustani, ndivyo pia migomba nayo anavyoweza kustawishwa kila sehemu nchini, baada ya watafiti kugundua mbegu bora isiyoshambuliwa na maradhi tena inayoweza kuzaa mkungu mikubwa inayokaribia uzito wa robo tani.

Hii ni faraja kwa wakulima wa migomba ambao zamani walikuwa wamekata tamaa kutokana na maradhi sugu ya ndizi maarufu kama ‘Panama’, yanayokausha mizizi, shina , matunda na kusababisha kilio mikoani Kilimanjaro, Kigoma, Kagera, Arusha, Manyara na Mwanza.

‘Panama’ kama saratani ya migomba, imeanza kudhibitiwa kwa kutumia mbegu zenye ukinzani na ugonjwa huo, ambazo ni migomba ya kisasa, isiyoshambuliwa na magonjwa na yenye sifa ya kustawi kwenye ardhi yoyote hata ikiwa kame.

Taarifa za kuidhibiti na kuwatia moyo wakulima na walaji wa ndizi zinatolewa na Mtafiti Mkuu wa Taasisi ya Kilimo ya Maruku mkoani Kagera na kiongozi wa utafiti wa migomba nchini, Mgenzi Byabachwezi ,akieleza kuwa, utafiti wa kupata ndizi zilizoboreshwa na zenye ukinzani na magonjwa umeleta mafanikio makubwa na migomba sasa inastawishwa popote.

Anatoa mfano kuwa mkoani Mwanza kuna aina mpya ya migomba iitwayo kitafiti ‘FHIA’ inayoweza kupandwa popote hata mikoa mikame mfano Singida au Dodoma almradi mkulima ahakikishe shina la ndizi linapata maji na kuhifadhi unyevu mara kwa mara.

Anaongeza kuwa Tanzania inaweza kuwa shamba la migomba kwa kuimarisha miundo mbinu ya maji.

Akizungumza na Nipashe kutoka Maruku mkoani Kagera, anasema migomba inashambuliwa na aina mbili za ‘Panama’ ambazo ni ‘mnyauko fusari’ iliyoenea mikoa ya kaskazini hasa Kilimanjaro, Arusha, Manyara na pia kuna ‘mnyauko bakteri’, uliojikita mikoa ya Kanda wa Ziwa ya Kagera, Kigoma na Mwanza.

Anaongeza kuwa ‘mnyauko fusari’ unatokana na virusi vya ‘Panama’ vinavyoweza kuishi ardhini kwa miongo mingi hata zaidi ya miaka 30, wakati ule wa ‘bakteri’ unatokana na bakiteria wanoweza kusambazwa kupitia vifaa kama panga au jembe ambalo hueneza ugonjwa kwa kuusambaza kutoka shina kwenda jingine ama shamba moja kupeleka kwingine.

Anasema katika haya mnyauko fusari ni hatari zaidi ndiyo maana mkoani Kilimanjaro hali ya migomba iko taabani ikilinganishwa na Bukoba, lakini anawatia moyo wakulima kuwa hata huko mkoani Kilimanjaro kwenye ‘mnyauko fusari mkali’, migomba hii mipya inapopandwa uhakika wa kupata ndizi kwa chakula pamoja na matunda upo zaidi ya asilimia 100.

Anawataka wapenzi wa ndizi kupata matunda na chakula kwa kupanda mashina ya migomba nyumbani katika sehemu ambazo wanamwaga maji ya kunawa au ya jikoni, eneo ambalo linaweza kuwa na uhakika wa maji muda wote na kueleza kuwa migomba ya FHIA haishambuliwi na magonjwa mbalimbali yanayotishia mimea hiyo.

MBEGU MPYA ZINAKUBALIKA

“Aina hii mpya ya migomba tuliyogundua inatoa mikungu mikubwa tumeisambaza mkoani Kagera na baadhi ya wilaya za mkoa wa Kigoma. Hii ina ndizi za uhakika. Inaweza kutoa mikungu inayofikia kilo 200. Miche yake ina soko kote nchini na hata nje ya nchini mathalani Nigeria na Jordan. Aina inayofanya vizuri ni FHIA17 na 23,” anasema.

Anaongeza kuwa hayo ni majina ya kitafiti na kwamba uzinduzi utakapofanyika migomba hiyo itapewa majina ya Kitanzania, kuenzi kazi za watafiti wa humu nchini. Anakumbusha kuwa tafiti zilianza tangu mwaka 1997 huko mkoani Kagera na migomba ya mbegu bora ilianza kuwafikia wakulima kuanzia miaka ya 2000.

Kwa mujibu wa maelezo ya mtafiti huyu, migomba zaidi inatafitiwa na itapelekwa kwa wakulima ili kupata maoni ya ubora wa ndizi zake, kabla ya kuanza kuisambaza na kwamba taarifa za kazi hiyo zitatolewa karibuni, katika jopo la sayansi la kutoa vipando (mbegu) na kwa wakati huo ndizi hizo zitafahamika zaidi na pengine soko lake litajulikana na kukubalika na walaji wa mikoa mingi nchini.

TAFITI ZINAGUSA WAKULIMA?

Anapotakiwa kueleza ni kwa kiasi gani utafiti wa Kituo cha Maruku umewanufaisha wakulima hasa wa ukanda wa Ziwa, Byabachwezi anasema , wakulima hasa mkoa wa Kagera wamenufaika kwa kuongeza kipato na kuwa na uhakika wa chakula kutokana na migomba hiyo.

Kwa mfano, wilayani Biharamulo ambako migomba halikuwa zao muhimu, sasa hivi baadhi ya wakulima wanamiliki hadi ekari 25 na wana uhakika wa kuuza hadi mikungu 10 kwa siku.

Mavuno ya migomba Kagera yalikuwa chini ya tani 15 kwa heka lakini sasa ni wastani wa tani 55 kwa hekta. Haya ni mafanikio makubwa.

“Tafiti za kubaini mbegu bora, kudhibiti magonjwa na jamii zinazohimili ukame zinaendelea.

Tafiti za kudhibiti magonjwa, wadudu na ukame zinaendelea na sasa wanajaribu aina 20 za migomba yenye sifa bora inayopandwa kwa majaribio kwenye taasisi za Maruku, Taasisi za Utafiti wa Mazao ya Matunda na Mboga Tengeru mkoani Arusha na ile ya Kilimo ya Uyole mkoani Mbeya.”Anasema.

“Tunaamini ndani ya miaka mitatu ijayo tutakuwa tunasambaza miche hiyo kama wakulima wataiafiki kwa kuonja na kukubali ndizi zake kwa chakula na matumizi mengine.” Anasema Byabachwezi.

WAATHIRIKA

Kwa mujibu wa Mtafiti Mkuu wa Taasisi ya Kilimo ya Maruku mkoani Kagera, waathirika wakubwa ni wakulima wa migomba inayotoa ndizi tamu, ambazo ni zile zinazozaa ndizi kwa ajili ya kuliwa mbivu mfano kisukari na gonja. Lakini kwa Kilimanjaro migomba yote inashambuliwa.

Anaeleza kuwa tatizo hili linadhibitiwa kwa kupanda migomba yenye ukinzani kama vile migomba ya asili ambayo ni ile inayopatikana katika nchi za Maziwa Makuu pekee inayojulikana kama ‘East Africa Highland Bananas’.

“Hadi sasa ugonjwa huu wa unaobadili migomba kuwa na rangi ya manjano unaoshambulia migomba aina zote hauna tiba. Utafiti unafanyika kupata mbegu kinzani.”

PANAMA

Taarifa za mitamdao zinaonyesha kuwa mwaka 1950 huko Amerika ya Kusini ugonjwa wa ‘mnyamko fusari’ au 'Panama’ ulitishia kutoweka kwa migomba baada ya fangasi wa maradhi hayo kushambulia mashamba makubwa ya zao hilo na ulioleta uhaba wa ndizi kwa ajili ya chakula na matunda .

Mtandao unaeleza kuwa mashamba ya migomba yaligeuka njano na kakauka huku ikitishia hatma ya zao hilo kutokana na kushambuliwa na fangasi waitwao ‘fusarium oxysporum’ wanaoishi kwenye udongo wakishambulia mizizi, hukausha shina, majani na baadaye ndizi.

Leo baada ya miaka 55 ya changamoto hali ya migomba mkoani Kilimanjaro, Arusha,Manyara na Tanga ni mbaya na kwamba tegemeo ni mbegu za kisasa, anazoeleza Byabachwezi, ikifafanua kuwa ugonjwa wa “Panama” ulioko mkoani Kilimanjaro upo ardhini na husambulia ndizi zote.

MAONI YA WAKULIMA

Baadhi ya wakulima wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro wanajaribu kupambana na ‘Panama’ kwa kutumia mbolea mbichi ya ng’ombe, inayochimbiwa kwenye shina lililoathiriwa.

Mathalani, baadhi ya wakulima wa vijiji vya Chanjale na Kisangara Juu wanaweka samadi mbichi na mkojo wa wanyama kupambana na ugonjwa huo ujulikanao kama ‘muruka’ kwa Kipare.

Hata hivyo, wakati mwingine fangasi hao wanapungua baada ya kupewa dawa hiyo ya kienyeji lakini hawamaliziki. Ugonjwa huu husababisha kila mwaka kurudishia migomba mipya.

Athari za ugonjwa huu ni kubwa kwani hauishi ardhini na ni wa kudumu na hairuhusu migomba mingine kustawi ni lazima inashambuliwa na hata ndizi hazikomai, zinaoza na kuwa na rangi ya njano.

Habari Kubwa