CHIMBUKO JKT

06Dec 2017
Flora Wingia
Nipashe
CHIMBUKO JKT
  • Meja Jenerali Isamuhyo afunguka sababu zilizofanya JKT kulegea
  • *Waliojiunga walikuwa na elimu ndogo

HISTORIA ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) inaanzia pale lilipoasisiwa tarehe 10 Julai 1963. Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Michael Wambura Isamuhyo, alielezea kwa kina chimbuko la jeshi hilo, katika kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na kituo cha ITV
Novemba 13, mwaka huu.

Mtangazaji alikuwa Sam Mahela.

Sehemu hii ya pili ya mfululizo wa mahojiano hayo, atakujuza pamoja na mambo mengine sababu zilizochangia JKT kulegalega. Endelea…

 

SWALI: Pengine baada ya kupata historia fupi na lengo la kuanzishwa kwa JKT, Meja Jenerali natamani kujua malengo yanaonekana yalikuwa mazuri sana na ‘mlitageti’(Mlilenga) kitu kizuri. Lakini haya malengo sasa bado yanasimama? Kwa sababu kuna wakati tuliona kwamba jeshi la Kujenga Taifa kama limelegea legea hivi, kama halipo halipo fulani hivi na kuna baadhi ya miaka tulikuwa tunaona mafunzo kama vile yalikuwa yamesimama, na maeneo ya mafunzo kama vile yalikuwa yamefungwa. Je, haya malengo bado yanaendelea mpaka sasa hivi au vipi, tueleze kwa faida ya Watanzania.

KULEGALEGA KWA JKT

JIBU: Mtangazaji, hilo ni swali zuri sana. Kwanza tujue kwamba malezi ya vijana ni endelevu kwa sababu vijana wapo leo na wapo kesho na kuendelea.

Kila nchi inao utaratibu wa kuhakikisha kuwa vijana wanalelewa katika utaratibu ambao unaoeleweka. Kwa hiyo, kwa kipindi cha sasa nadhani hii inahitajika zaidi kwa sababu kipindi tunapata uhuru utakumbuka teknolojia ilikuwa siyo kubwa sana.

Hata ITV haikuwapo, TV yoyote haikuwapo, tulikuwa na Radio moja inaitwa RTD (Radio Tanzania Dar es Salaam). Na yalikuwapo magazeti ya serikali machache tu, Uhuru/Mzalendo, Daily News na Sunday News.

Kwa hiyo utaona kwamba, na hayakuwa yanafika maeneo mengi. Sasa hivi tuna teknolojia ambayo ni kubwa zaidi ambayo sasa hivi tuna mitandao ya kijamii, tuna internet na kadhalika. Tv nyingi, magazeti mengi. Kuna uhuru wa habari. Kwa hiyo yale ambayo tunadhani kwamba tungeweza kuwafundisha vijana wetu sisi wenyewe, vijana wanajifunza mambo mengine.

Kwa hiyo lazima tuwe na utaratibu wa kuwarudisha hata kama ni wachache lakini tuwe tunawaandaa wale ambao wanaweza kutumikia taifa hili vizuri.

WALIOJIUNGA WALIKUWA NA ELIMU NDOGO

Ni kweli kama ulivyosema huko nyuma lililegalega kidogo, baada ya kuanzishwa mwaka 1963, JKT iliendelea bila matatizo lakini katika kipindi hicho baada ya kuanzisha, katika mwaka 1963, 1964, 1965, vijana ambao waliojitokeza kuingia kwa hiari ilikuwa ni vijana wale waliokuwa na elimu ndogo.

Lengo lilikuwa ni waingie wote, wale vijana wa Tanzania, lakini bahati mbaya wasomi hawakuitikia wito huo. Mwaka 1966 ikabidi wabadilishe kifungu cha sheria ya mwaka 1966 ambayo ilianzisha National Service (Jeshi la Kujenga Taifa) ili kuwalazimisha vijana wanaomaliza shule ili waweze kuingia kwa lazima.

Kwa hiyo kuanzia mwaka 1966 tulikuwa tuna makundi mawili ya vijana; vijana waliokuwa wanajiunga kwa mujibu wa sheria kwa lazima na vijana waliojiunga kwa hiari. Kwa hiyo utaratibu huo uliendelea vizuri sana.

 

Lakini ilipofika mwaka 1987, baada ya vita vya Kagera, uchumi wa nchi yetu nadhani sote tunakumbuka haukuwa mzuri sana. Kwa hiyo ikabidi tulazimishwe pia na sera za taasisi za kimataifa kama World Bank (Benki ya Dunia) ambazo zilikuwa zinaleta fedha wakasema hawawezi kuleta fedha katika Tanzania kama msaada na wafadhili wengine kwa ajili ya kuendesha shughuli pamoja na shughuli za kijeshi.

Kwa hiyo wakawa wamezuia wakati ule wa vita. Mwaka 1994 mafunzo yakawa yamesimamishwa. Kwa hiyo kuanzia mwaka 1995 hapakuwa na kijana yoyote ndani ya makambi ya JKT. Lakini katika kipindi hicho, kuanzia kipindi hicho 1995 mpaka 2000, kulikuwa na

mabadiliko makubwa sana kwa upande wa hali ya vijana wetu wale ambao hawakupata nafasi ya kupitia JKT, sehemu za kazi kulikuwa na masuala ya ajabu ajabu, shuleni kulikuwa na mambo ya ajabu ajabu, utovu wa nidhamu kwa vijana, kutokuwa na uvumilivu na kadhalika.

Kwa hiyo, baada ya serikali kuliona hilo na wananchi kupaza sauti zao kwamba national service ilikuwa ni muhimu, ni kweli ilikuwa inachukua watu wachache, lakini wale waliokuwa wanapitia walikuwa wanaonekana tofauti kidogo na wengine.

Kwa hiyo mwaka 2001 wakaingia tena kwa mara nyingine hadi sasa tunao. Walianza wa kujitolea mwaka 2000, na mwaka 2013 wakaanza kuingia vijana kwa mujibu wa sheria na tunao hadi sasa.

Kwa kujibu swali ni kwamba bado umuhimu upo kwa sababu vijana kuna matishio mengi ambayo yapo, masuala yenye dalili za migomo, masuala ya kutengana kidini na kadhalika vilianza kujitokeza. Sasa hivi hali siyo mbaya.  Kwa hiyo bado umuhimu wa National Service ni mkubwa zaidi pengine kuliko huko tulikotoka.

 

SABABU KUJIUNGA JKT KABLA YA ULAZIMA:

SWALI: Meja Jenerali nikurudishe nyuma kidogo katika maelezo yako umetueleza kwamba kabla hamjatoa sheria hii ya ulazima wa mtu kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa wakati watu wengine hawataki kwenda, wanaamua kwamba mimi siendi, katika kudadisi mlihisi kwamba walikuwa wanadharau Jeshi la Kujenga Taifa au ilikuwa ni nini inasababisha watu hawataki kujiunga na jeshi hilo kabla ya sheria kulazimisha waende?

JIBU: Mwanzo nilijaribu kueleza kwamba wakoloni walijitahidi sana kuwajenga Watanzania au Tanganyika wakati huo wachukie kazi za mikono, wavae tai waende ofisini. Ilikuwa zaidi wanaandaliwa kwa ajili ya uongozi na masuala ya ofisini.

Kwa hiyo, kwa sababu walikuwa wanaandaliwa katika utaratibu huo, waligundua kwamba national service, walijua kwamba kuna mafunzo ambayo ni magumu na kadhalika. Kwa hiyo, hawakutaka.

Lakini pia nadhani kulikuwa na ambao kasumba ilikuwa imekuwa zaidi hawakutaka tuwe na muunganiko. Kwa hiyo, na wakati huo vyuo vingi na shule nyingi bado zilikuwa zinafundishwa na hata watu weupe ambao walibidi kusubiri tupate wataalamu wa kwetu.

Kwa hiyo, hata huko vyuoni walikuwa wakiwaambia msijiunge huko ndio maana kulikuwa na hali ya kutopenda kuingia makambini.

SWALI: Pengine Meja Jenerali turudi, kwa sasa hivi, wakati huu, siku hizi tunaona zaidi vijana kama wanaonekana kukosa uzalendo na taifa lao. Kuna wakati hata kuna ile hali ya migomo migomo, lakini kuna wakati fulani watu wanakosa uzalendo na taifa lao.

Huko jeshini watu wakipelekwa wanafundishwa namna ambavyo unaweza ukaipenda nchi yako, namna ambavyo unaweza ukajitoa kwa ajili ya nchi yako, lakini sasa hivi sivyo.

JIBU: Yapo mazingira mapya yanaweza yakasababishia vijana hali hiyo ikaonekana kuwepo. Lakini nadhani bado hatujafikia kwamba tuko katika hali mbaya kwa upande wa uzalendo.

Bado Watanzania vijana wetu wengi ni wazalendo. Hata wale ambao hawajatokea national service wanaonyesha uzalendo katika masuala mbalimbali. Kwa sababu kuna hizi tofauti ambazo zinaonekana sasa hivi za uhuru wa habari watu wanatoa comments zao, hayo ni mawazo yao.

Lazima hata kama mnapendana, hata hiyo Israel tulikuwa tunaizungumza kwamba kuna uzalendo wa hali ya juu ambao ndio umeonyeshwa dunia, lakini wakati mwingine kunakuwa na matatizo sana, hayo ni mambo ya kawaida.

Lakini inapotokea masuala yanayohusiana na manufaa ya taifa, maslahi ya taifa hapo ndipo unaweza ukasema watu wako wapi. Kwa hiyo wako vijana wachache na kwa sababu wako katika mazingira ya vyama vingi, mazingira ya masuala ya dini, mazingira ya vyombo hivi vya habari na kadhalika.

Kwa hiyo watu wanaweza wakawa na hayo mawazo, lakini hatujakuwa na tatizo kubwa la kitaifa ambalo unaweza kuona kwamba uzalendo haupo. Ndio maana ukitaka kujua hilo ikitokezea matatizo makubwa, ajali unaona jinsi ambavyo tuliungana kuhakikisha kwamba wanatatua yale matatizo.

Kwa hiyo, mimi nadhani kwamba siwezi kusema kwamba uzalendo haupo, uzalendo unaweza kuona jinsi ambavyo uchaguzi unavyokwenda vizuri na kuisha. Matatizo madogo madogo yanayotokea baadaye uchaguzi unaisha vizuri bila shida inaonekana taifa bado ni moja.

*ITAENDELEA JUMATANO IJAYO.

 

Habari Kubwa