Corona ilivyopaisha matumizi ya tiba asili kwa wahitaji Tanzania

21Jan 2021
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Corona ilivyopaisha matumizi ya tiba asili kwa wahitaji Tanzania
  • Mti wa mkaratusi na limao zang’ara
  • Serikali: Wahitaji tiba hiyo ni wengi

TANZANIA imebarikiwa miti mingi ambayo ni tiba ya magonjwa mbalimbali. Hilo limethibitika wakati wa janga la corona, watu wengi kutumia mitishamba ambayo iliwapa ahueni kubwa na kupona kabisa.

Muuzaji malimao, Harun Iddi katika Soko la Majengo, Dodoma, bidhaa iliyoongezeka sokoni, kutokana na kutumika kutibu corona. PICHA ZOTE: MTANDAO

Mimea mingi ilithibitika kusaidia watu wengi wenye matatizo mbalimbali ya mfumo wa hewa kama kifua, homa, mafua na magonjwa mengine.

Hapo inajumuisha matawi ya mwarobaini, mvumbasi, mchaichai, mpera, malimao, mkaratusi, tangawizi na mimea mbalimbali ya kujifukiza, ili kuondoa kirusi hicho mwilini.

Dawa hizo za asili hutumika ama kwa kujifukiza au kunywa. Hapo inabeba maana ya kuchemsha aina mbalimbali za mimea, kisha mgonjwa anakaa kwenye kigoda na kufunikwa shuka ili kupata mvuke anaouvuta, akiwa amefunikwa na kuingia moja kwa moja kwenye mfumo wake wa upumuaji.

Majani ya mkaratusi yamekuwa yakitumika kama tiba kwa watu kujifukiza. Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Tiba Asili na Tiba Mbadala Mkoa wa Dodoma, Mohamed Mdoe, anathibitisha hilo.

Hiyo ni baada ya ugonjwa huo kuibuka nchini na wananchi kutumia dawa mbalimbali za kujifukiza, huku kukikosekana mti maalum au dawa, isipokuwa mkaratusi unaonekana kutumiwa na wengi.

“Mti uliotumika kwa kiasi kikubwa ni mkaratusi waliupenda sana na kwa sababu huu mti ni mzuri hasa kwa maradhi mbalimbali, wazee wa zamani walikuwa wanapenda kutumia dawa hii.

“Kwa hiyo, tukachukulia wazee wetu wa zamani kama vile kipindi cha ugonjwa wa ndui watu walikuwa wakiogeshwa mti huo kuna maradhi kama UTI (maambukizi kwa njia ya mkojo na huathiri mfumo wa mkojo), mtu anachemshiwa huo mti anakunywa,” anasema.

Anasema majani ya mti huo yalitumiwa na watu wengi kutokana na sifa za kutibu maradhi mbalimbali kwenye mwili wa binadamu.

Mdoe anasema, kila mwananchi alikuwa na namna yake ya kutafuta mti huo ambao kwa Dodoma si mingi, ikilinganishwa na mikoa ya Tanga na Kilimanjaro.

Anafafanua kwamba kuna wakati watu wa Dodoma walikuwa wanaagizia mkoani Tanga ili kupata majani hayo ya mkaratusi.

“Kukata matawi kila mmoja alikuwa nakwenda kivyake hapakuwapo na kubebana kwa pamoja kwenda kukata na kila mmoja alikuwa anajua anapata eneo gani mti huu, tunashukuru hali ni nzuri kwa sasa,” alisema.

Anaongeza: “Wakati wa corona kila mmoja alikuwa anaangalia njia gani kikwao au kikabila, hivyo walikuwa wanaangalia ni dawa gani inayofaa siyo dawa maalum kwa corona, kila mtu alitumia dawa kulingana na anavyoamini kikwao.”

Anabainisha matumizi hayo ya tiba mbadala kwa kujifukiza ilisaidia watu wengi kufanikiwa hasa waliokuwa wakihisi mafua au homa inayofanana na dalili za ugonjwa huo.

Mdoe anasema: “Kila mmoja alitafuta namna ya kujinusuru hakukuwa na dawa maalum ya kutumia kwa ajili ya corona, wazee walitufundisha matumizi ya dawa hizi, sisi kama wataalamu wa tiba.

“Tulikuwa tunafuatilia watu walikuwa wanaomba ushauri wa dawa hasa za kujifukiza, tulikuwa tunawaelekeza watumie mti fulani, mwamko ulikuwa mkubwa.”

Mwenyekiti huyo anaeleza kuwa walikuwa wakiwapa ushauri wa dawa hizo kuchemsha na kujifukiza na siyo za kunywa. Anafafanua:

“Watu walikuwa wakienda porini huko kutafuta na kuwauzia watu, wengine kusaidiana bure hakukuwa na gharama maalum, kila mtu alikuwa na namna yake, walikuwa wanapeana tu, ni mtu kuelekeza tumia dawa hii au hii.”

TAARIFA YA NIMR

Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), kupitia kwa Mkurugenzi Mkuu, Prof. Yunus Mgaya, wakati wa corona nchini, alisema ikiwa watu watatumia mimea zaidi ya minne, upo uwezekano wa dawa hizo kuanza kupambana zenyewe katika utendaji badala ya kumsaidia mgonjwa.

Anaifafanua mchanganyiko unaotakiwa, kundi la kwanza ni mchanganyiko wa majani ya mkaratusi, majani ya kivumbasi (kashwagala) na mchaichai; kundi la pili ni mchanganyiko wa mchaichai, karafuu, tangawizi iliyopondwa na majani ya limao; lingine ni majani ya mwarobaini, majani ya mpera, mchaichai na majani ya mlimao.

Prof. Mgaya anasema mtu anatakiwa kutumia gramu 50 za majani ya mkaratusi, gramu 50 za kivumbasi na gramu 20 za mchaichai na kwamba tiba joto hiyo au mvuke ni muhimu kusaidia kuongeza kinga ya mwili, kufungua njia ya hewa na kurarua virusi vya corona, kama bado vimo kwenye njia ya hewa na havijaingia kwenye mapafu.

USHUHUDA

Mtumiaji dawa hizo, Edward Mathias, anasema alihisi dalili za ugonjwa h akiwa nyumbani na akaamua kujitenga kwa wiki nzima, huku akijifukiza kwa kutumia mimea minne ikiwamo, mkaratusi, mvumbasi, mchaichai na tangawizi.

Anasema kwa muda mfupi hali hiyo ya kuumwa mwili na mafua yasiyopona iliondoka na hadi sasa hajasikia hali ya aina hiyo mwilini mwake. Mtahias anasimulia:

“Miajani ya mkaratusi niliyapata kwa jirani yangu, mvumbasi unapenda kuota kwenye viwanja vya mpira, nikapata mimea yote minne nilikuwa nachemsha maji kwanza yakichemka ndio natumbukiza majani haya.

“Kwa dakika chache tu nikiwa nimefunikia, baada ya hapo nasogeza jiko likiwa limebandikwa sufuria najifunika shuka kwa ajili ya kujifukiza.

“Yaani ule mvuke nausikia kabisa unaingia kwenye mfumo wa hewa. Nilikuwa natumia dakika 10 kukaa humo kila siku jioni, nikitoka naoga maji ya vuguvugu ili kuondoa kirusi maana wataalamu walituambia kirusi kina asili ya mafuta, kweli kufukiza kumenisaidia.”

Mnamo Mei 17 mwaka jana, Rais John Magufuli akitoa salamu kwa Watanzania aliposhiriki ibada ya Jumapili akiwa Chato mkoani Geita, aliwaambia kuwa mtoto wake aliambukizwa virusi vya corona, lakini alipona baada ya kujitenga, kunywa malimao na kujifukiza.

WATENGENEZA DAWA

Mapema mwaka jana, Mkurugenzi wa Kitengo cha Tiba Asili kutoka NIMR, Dk. Justine Omolo, alisema dawa ya NIMRCAF iliyofanyiwa utafiti na taasisi hiyo, ilionyesha matumaini ya kudhibiti ugonjwa huo.

Dk. Omolo anasema dawa hiyo ni kanuni ya tiba lishe yenye mchanganyiko wa pilipili kichaa, tangawizi, limao, kitunguu saumu, asali na maji na inasaidia kumpa nafuu mgonjwa wa corona, kwa kudhibiti dalili zake.

“Mchanganyiko wa tiba lishe hiyo sio dawa ya corona, lakini inasaidia kumpa nafuu mgonjwa kwa kuwa inatibu dalili zinazoambatana na ugonjwa huo, hadi sasa tiba lishe hii imeshaleta matokeo chanya kwa kuwa imesaidia wagonjwa wengi wa corona,” anasema.

WADAU DODOMA

Mwakilishi wa Shekilindi Bosnia Ant Covid (dawa ya kutibu dalili za Corona), Dodoma, Bashiru Iddy, anasema usajili wa dawa hiyo umekamilika na Mkemia Mkuu wa Serikali amethibitisha kwamba haina sumukuvu yoyote na salama kwa matumizi ya binadamu. Hata hivyo hakuweka wazi mchanganyiko wa dawa alizotumia.

“Kipindi cha corona dawa hii imesaidia watu. Usajili wake upo vizuri, tumepata pia kibali kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na nyaraka zipo. Dawa inafanya kazi kwa kiasi kikubwa magonjwa ya kifua,” anasema.

Bashiru anasema wakati wa corona, chupa ya dawa anayouza ilikuwa Sh. 30,000 na mtu mwenye dalili za ugonjwa huo alishauriwa kunywa chupa hiyo, pamoja na glasi tatu za juisi ya miwa.

“Baada ya saa nne alikuwa anatakiwa kunywa chupa ya pili, pia baada ya saa nne anakunywa chupa ya tatu. Hivyo, mtu mwenye dalili hizo alikuwa anapata tiba.

“Dawa hii imetengenezwa na aina tatu za miti ambayo kitaalamu hatuwezi kuweka wazi ili wengine wasije kufanya utapeli utakaosababisha madhara kwa jamii,” anasema.

WAUZA DAWA ASILI

Muuza dawa asili, Josephina Peter, anasema mwitikio wa watu kujifukiza wakati wa corona ulikuwa mkubwa na wananchi walinunua mkaratusi, mvumbasi na mwarobaini.

Muuzaji wa dawa za tiba asilia, Mariamu Masudi, anasema awali mimea au dawa hizo zilijulikana kwa matumizi mengine, lakini kutokana na ugonjwa huo zilitumika kujifukiza ili kuondoa kirusi hicho mwilini.

MATUMIZI YA MALIMAO

Mfanyabiashara katika Soko Kuu la Majengo jijini Dodoma, Harun Iddy, anasema wakati wa mlipuko wa corona nchini, bidhaa kama malimao, tangawizi na vitunguu saumu viliongezeka sana mahitaji yake sokoni.

Anatumia mifano akitumia vilelezo visivyo rasmi, kwamba kutokana na matumizi ya tiba mbadala, mfanyabiashara aliuza mifuko ya kilo 100, zaidi ya 500 kila siku.

Iddy anasema pamoja na mahitaji hayo makubwa, bidhaa hizo zilipatikana kwa wingi kuhudumia wananchi waliotumia kuchemsha na kijifukiza.

Mwakilishi wa Kikundi cha Shekilindi Bonsnia Ant Covid mjini Dodoma, Bashiru Iddy, akionyesha chupa ya dawa iliyotumiwa na wananchi wakati ugonjwa wa corona, ulipokuwapo nchini.

Anasema katikia kipindi cha mvua, malimao yalikuwa adimu na akalazimika kuzifuata nchi jirani Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Uganda na Sudan.

“Hii imetokana na mvua kunyesha kwa wingi nchini mwaka jana msimu wa pili wa malimao, haukuwapo hali ambayo imesabaisha bidhaa hiyo kuwa adimu,” anasema.

Pia anasema kipindi hicho walikuwa wakiuzia mfuko moja wa kilo 100 kwa zaidi ya Sh. 250,000 na upatikanaji wake ulikuwa wa shida, wakati awali ilichukuliwa kama kitu cha kawaida.

“Zamani mtu ukimwambia unafanya biashara ya malimao anashangaa, lakini hivi sasa hata ukipita barabarani umebeba mzingo wa malimao watu wanakuulizia bei tofauti na zamani,” anasema.

Mfanyabiashara Hassan Chitembedya, anasema malimao hivio sasa sokoni hayakai, kutoka na mahitaji makubwa na mengi yanasafirishwa nje ya nchi, ikiwamo Kenya kwa ajili ya matumizi ya tiba mbadala corona.

Kitaalamu, limao ingawa si tunda lenye virutubisho vingi vya vitamini C, lakini ni bora kwa kuwa na kemikali inayosaidia kutibu mafua na mfumo wa kupumua.

 

Maji ya limao yanatajwa kuwa na takriban miligramu 18.6 za vitamini C na vipimo kamili vya kila siku vinavyopendekezwa kwa watu wazima ni kati ya miligramu 65 na 90.

WIZARA YA AFYA

Mkurugenzi Msaidizi wa Tiba Asili na Tiba Mbadala wa Wizara ya Afya, Dk. Paulo Mhame, anakiri ujio wa ugonjwa huo nchini umesaidia huduma za tiba asili nchini kukubalika kwa wengi, pasipo kujali kiwango chao cha elimu na hadhi yao kijamii, mtazamo ulliokuwapo awali.

 “Wengi wametumia kunywa hususani matumizi ya tangawizi, limao, vitunguu na vitunguu swaumu, pia katika kujifukiza kumewapaisha Watanzania ugonjwa wenyewe uklionekana sio kitu.

“Llakini hadi leo watu wanaendelea kujifukiza hata kama hawavai barakoa wala kunawa mikono na wanatumia mafuta tete kwa ajili ya kufukiza hususan matumizi ya kivumbasi, mchaichai na mkaratusi nao unatumika kwa wingi,” anasema.

Anasema dhana ya kuona tiba asili ni ushiriki inaondoka, lakini kiserikali bado kuna kazi ya kuendelea kuelimisha wananchi matumizi ya huduma za tiba asili.

Mwaka juzi, dunia ilikumbwa na homa kali ya mapafu, inayosababishwa na virusi vya corona na kuripotiwa kwa mara ya kwanza mjini Wuhan, China na baadaye ukasambaa duniani.

Utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa wagonjwa 56,000, ulibaini asilimia 80 ya walioambukizwa, hupata dalili zisizo kali kama vile kukohoa, joto mwilini na mara nyingine homa ya mapafu.

Pia asilimia 14 hupatwa na dalili kali kama vile tatizo la kupumua; asilimia sita wanakuwa na tatizo la mapafu kushindwa kufanya kazi na viungo vingine mwilini na hata kusababisha kifo.

Takwimu zinazotolewa kila siku na WHO, hadi kufikia Januari 6, 2020 wakati corona ilivamia dunia , kulikuwapo jumla wagonjwa milioni 83.32 na vifo 1,830,000 katika nchi zote zilizokumbwa.

Nchini Tanzania, mgonjwa wa kwanza aliripotiwa Machi 16, 2020 na serikali ilichukua hatua mbalimbali za kukabiliana nao, ikihimiza pia wananchi kutumia tiba ya asili jambo lililowasaidia kutojifungia (lockdown) na wengi waliendelea na shughuli zao.

Katika kipindi cha corona, Tanzania ilionekana kinara wa matumizi ya tiba hiyo, baada ya Rais John Magufuli kutoa wito kwa Watanzania kupitia hotuba zake mbalimbali kutumia ili kupambana na ugonjwa huo kwa kujifukiza, sambamba na ibada maalumu kupitia nyumba za ibada.

SIMULIZI ZA WATUMIAJI

Mkazi wa Dodoma, John Mnyahimbu, anasema majani hayo wakati wa kujifukiza yalimsaidia kutokwa na jasho kwa wingi na anayehisi mafua, mfumo wake wa hewa  unafunguka.

“Mimi nilikuwa najifukiza mara moja kila siku jioni, nikirudi kwenye mihangaiko yangu. Nikifika na majani yangu nachemsha nimeyafunikia yakichemka napunguza moto halafu najifunika na nguo,” anadokeza na kuendelea:

“Nakuwa nimeinamia ili kupata mvuke, nilikuwa naona inanisaidia hata viungo vya mwili vikionekana kuchoka ile ni kama sauna.”

Habari Kubwa