Corona inavyoacha somo kwa kinamama kujikinga magonjwa ya milipuko

14Aug 2020
Jenifer Gilla
DAR ES SALAAM
Nipashe
Corona inavyoacha somo kwa kinamama kujikinga magonjwa ya milipuko

WAKATI serikali imetangaza kupungua kwa maambukizi ya virusi vya Corona, bado wananchi wanahimizwa kuendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kujikinga na ugonjwa huo.

Wanawake wakiendelea na biasahara zao katika moja ya masoko nchini. PICHA: MTANDAO

Baadhi ya hatua zinazopendekezwa ni kunawa mikono kila mara, kujisafisha kwa kutumia vitakasa mikono, kuvaa barakoa na kujiepusha na mikusanyiko isiyo ya lazima.

Valentina Kasian (45), mkazi wa Tabata, jijini Dar es salaam, ambaye ni mchuuzi wa matunda eneo la Tabata kwa Sesi, ni miongoni mwa watu wanaokiri kujisahau kujikinga dhidi ya virusi vya corona.

Akizungumza na mwandishi wa makala hii, Valentina ambaye hutumia saa 12 akiwa kwenye shughuli zake za biashara, amesema kwa sasa tahadhari kwake si jambo la muhimu kwa kuwa ugonjwa umekwisha.

Kutokana na biashara yake ambayo inambidi kutembea mitaani, hatari ya kuambukizwa inakuwa kubwa.

 “Natumia kama masaa matatu hivi, kuzungukia nyumba zote za maeneo haya ya kwa sesi kuuza mtunda, kisha narudi nyumbani kuhudumia familia”, anasema.

Mama huyo mwenye watoto wawili anakiri kuwa umakini wa kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona kwenye baadhi ya maeneo kama ndani ya daladala na sokoni umepungua.

Anasema imefikia wakati utaona mtu mmoja au watu wawili pekee ndio wanaonekana kuvaa barakoa, jambo ambalo ni hatari.

“Sokoni nako ni hivyo hivyo, ile taharuki ya ugonjwa imepotea kabisa, soko zima unaweza kuona mtu mmoja ndio amevaa barakoa, hata mimi pia sizingatii kwa kweli”.anasema

Mama huyu ni mmoja kati ya asilimia zaidi ya 80 ya wanawake wanaotajwa na Shirika la kazi Duniani (ILO) katika utafiti wa mwaka 2006 ambao wanafanya kazi zao katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu.

Kutokana na takwimu hiyo, wanawake hao wanaonekana kuwa hatarini kupata maambukizi ya ugonjwa wa Corona na kuathiri shughuli zao za kiuchumi.

Amina Ramadhani,  mfanyabiashara wa mbogamboga anayetembeza mtaani, anakiri kuwa ana muda mrefu hajafuata tahadhari ya kujikinga virusi vya corona.

Anaeleza kwamba hana haja ya kuvaa barakoa anapokuwa katika shughuli zake kwa sasa kwa kuwa dalili zinaonyesha umepungua.

 “Kwa kweli sijazingatia, hata unavyoniona hapa sina hata barakoa ingawa kwa wakati mwingine naogopa kama ugonjwa huu ukirudi tena naweza kuambukiza hata watoto nyumbani na kushindwa kufanya shughuli zangu ,” anasema Amina

Amina anatamani uhamasishaji urudi kama ilivyokuwa mwanzo ili watu waendelee kujikinga.

Vilevile vitendo vya kutokuwa makini kwa kuzingatia maagizo yanayotolewa kwa baadhi ya wanawake,  inaelezwa kuwa ni moja kati ya vitu vinavyoweka hatari ya kusambaa kwa kasi kwa corona.

 “Sisi wanawake hatuuzingatii kabisa, unajua ni mtu wa kwenda kwenye mikusanyiko ya watu, kwa nini usichukue tahadhari” anaongeza kusema.

Kisha anaendelea “Mimi ni mama wa familia, ninapoambukizwa ugonjwa huu inamaana nitaambukiza familia yangu yote nyumbani kwa kuwa dalili zake hazijitokezi hapo hapo unapoambukizwa,” anasema

Kwa upande wa Bertha Philimon, mmiliki wa duka la nguo Kariakoo, anasisitiza wanawake kuendelea kuchukua tahadhari kwa sababu wao ndio walezi wa familia.

 ‘Kwa mfano mimi mtu haingii dukani kwangu bila ya kuvaa barakoa na kunawa mikono, kwa sababu ugonjwa huu upo, tunapaswa tuishi nao kwa kuchukua tahadhari.” Anasema Betha.

Kipato cha Betha katika duka lake ni kati ya Sh. 300,000 hadi 500,000 kwa siku  kwa sasa, nusu ya mapato yamepungua tangu kutangazwa kwa ugonjwa wa corona.

ATHARI UCHUMI

Mkurugenzi wa Taasisi ya Binti makini, Janeth Makini,  anaelezea athari za Covid-19 kwa wanawake kuwa ni nyingi lakini kubwa ni kushuka kwa uchumi kutokana kudorora kwa biashara.

 “Wanawake wajasiriamali wengi kwa sasa wamedhoofika kiuchumi, wengine wameshindwa kurudisha marejesho ya mikopo na hata kupeleka watoto shule, na kuna ambao wamelazimika kuuza vitu vyao vya ndani ili kusimamisha tena biashara zao ,”anasema Janeth.

Kwa mujibu wa mwanaharakati huyu, wakulima vijijini nao corona imewatafuna, akitolea mfano wa wakulima mkoani Lindi, ambao wamelazimika kuuza zao la korosho kwa Sh. 800 Badala ya bei elekezi ya Sh.3000 kutokana kukosa wateja.

ELIMU YAENDELEZWA

FORUM CC ni Taasisi inayojishughulisha na kutoa elimu mbalimbali ikiwemo athari za Mabadiliko ya tabia nchi na wanawake(FORUMCC), kwa kushirikiana Umoja wa Ulaya (EU), inaendelea kuhamashisha wanawake kuendeleza tabia njema ilizojifunza kutokana na ugonjwa wa Covid-19.

“Tumeona ni vizuri kuendeleza tabia njema tulizojifunza kutokana na ugojwa wa corona kama vile kunawa mikono,kuvaa barakoa unapokwenda kwenye sehemu yenye mikusanyiko mikubwa ya watu na pia kutunza mazingira ili kuchukua tahadhari ya magonjwa yanayoambukiza kama corona” alisema Sara Pima, Ofisa Mradi wa ForumCC

COVID-19 VS MAFUA YA HATARI

Akiongelewa tofauti ya ugonjwa na Covid-19 na homa ya kawaida, Dk. Neelum Ismail kutoka hospitali ya Agakhan, anasema kuwa magojwa haya hutokana na virusi tofauti.

Kwa mujibu wa Daktari huyo wa familia, Covid-19 hutokana na virusi vya corona na huambukiza kwa kasi kuliko kirusi cha mafua kiitwacho influenza.

Vilevile  huathiri mfumo wa upumuaji wa mwanadamu  na huweza kuibua  maradhi mengine kama vile homa ya mapafu  na figo kushindwa kufanya kazi.

 

HALI ILIVYOKUWA

Mnamo Machi 16, 2020, Tanzania ilitangaza mgonjwa wake wa kwanza wa virusi vya Covid19 na Machi 17, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa alitangaza kufunga shule zote kuanzia za awali hadi vyuo vikuu.

Pia serikali ilizuia mikusanyiko yote na kuzuia safari za kimataifa zisizo na ulazima ili kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa Covid -19 nchini.

Pia alitangaza kutolewa Sh. milioni 500 kati ya Sh. bilioni moja zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya Mbio za Mwenge wa Uhuru ili zisaidie katika kukabiliana na janga hili.

HATUA KUDHIBITI COVID-19

Jitihada zilizofanywa na Rais John Magufuli, zilisababisha kuwepo na umakini katika kutoa elimu kwa umma kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa corona, dalili zake pamoja na jinsi ya kuepuka maambukizi.

Jamii ilielimishwa umuhimu wa kunawa mikono kwa maji tiririka mara kwa mara,kutumia vitakasa mikono, kuvaa barakoa na kuepuka msongamano kwa kuzingatia umbali baina ya mtu mmoja na mwingine.

MITISHAMBA KUTUMIKA

Katika harakati za kujikinga na ugonjwa corona kulienea imani kuwa mchanganyiko wa baadhi ya mitishamba ‘nyungu’ kuwa na uwezo wa kuua vimelea vya ugonjwa wa corona pale mtu anapojifukiza.

Moja na dawa zilizouzwa ni NIMRCAF iliyotengenezwa na Taasisi ya Taifa ya utafiti wa magonjwa ya binadamu-NIMR.

SHUGHULI KUFUNGULIWA

Mwezi Mei mwaka huu, Serikali ilitangaza shughuli za kawaida za kijamii, kiuchumi ziendelee kama kawaida hali iliyopelekea kufunguliwa kwa shule za msingi, sekondari na vyuo.

Habari Kubwa