Dakika 60 za Waziri Lukuvi jijini Mbeya zaendelea kutimua vumbi

15Mar 2019
Nebart Msokwa
Mbeya
Nipashe
Dakika 60 za Waziri Lukuvi jijini Mbeya zaendelea kutimua vumbi
  • Ardhi yatekeleza maagizo kwa Mchakamchaka
  • RC Chalamila amfuata mtangulizi ‘hapa kazi tu’
  • Meya: Kinachotuumiza siasa, tuzipishe kidogo

MWISHONI mwa mwezi Januari mwaka huu, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alifanya ziara ya kushtukiza katika Wilaya ya Mbeya.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, katika picha tofauti, akifanya ukaguzi katika Masijala ya Ardhi, katika Halmashauri ya jiji la Mbeya, mwishoni mwa Januari mwaka huu, alipofanya ziara ya ghafla. PICHA: NEBART MSOKWA.

Hapo akawa mgeni wa watendaji wa Idara za Ardhi na Mipango Miji wa halmashauri zote mbili za wilaya hiyo.

Waziri Lukuvi, alitumia saa moja katika ofisi za Jiji la Mbeya, alipogeuka shubiri kwa watumishi wa Idara ya Ardhi na Mipango Miji, jijini Mbeya kutokana na mazito aliyoibua katika ofisi hiyo.

Akizungumza na watendaji hao kwenye kikao kilichofanyika katika Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya na kuhudhuriwa na maofisa na wapima ardhi, kutoka katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, pamoja na wataalamu kutoka Ofisi ya ardhi ya Kanda, alisema ameabaini ‘madudu’ kadhaa katika eneo lao la kazi.

Hilo lilianzia pale alipowahoji maswali mbalimbali kuhusu utendaji kazi wao, akasema amebaini kuwa watumishi hao hawana ratiba maalum inayowaongoza kutekeleza majukumu yao, hali iliyomkera na kutishia kuwachukulia hatua kali.

Vilevile anasema, alibaini kuwa watendaji hao wana kasi ndogo ya upimaji viwanja, urasimishaji wa makazi ya wananchi na ukusanyaji kodi ya ardhi, huku akirejea takwimu zilizoko wizarani zinaonyesha kuwapo madeni makubwa.

‘Madudu’ Ardhi

Kaimu Mkuu wa Idara ya Ardhi na Mipango Miji wa jiji hilo, Emeliana Kihunrwa, alikiri kutokuwapo ratiba yoyote katika maandishi, isipokuwa wanatenda kwa kukubaliana kazi za kufanya kupitia vikao.

Ni majibu yaliyoonekana kumkera Waziri Lukuvi, ndipo alipoanza kuibua mapungufu mengine ya utendaji wa sekta ya ardhi, ndani ya jiji hilo.

Waziri Lukuvi, anasema Mbeya ni mji unaomkera kutokana na mpangilio duni wa makazi unaosababishwa na maofisa ardhi na mipango miji, kutowajibika ipasavyo kwenye majukumu yao.

Anasema, wananchi wanalazimika kujipanga kulingana na eneo mtu analolimiliki na kwamba maeneo mengi ya makazi hayajapimwa, pia wamiliki hawana hati miliki za maeneo hayo.

“Jiji hili halinifurahishi kwenye masuala ya ardhi. Hamna ‘master plan’ (mpango mkuu) ya mji na ndio maana, kila mtu anajenga anavyojua, wala hamuonyeshi kushtuka na mpangilio huo,” anasema Lukuvi.

Anasema kasi ndogo ya upimaji viwanja na kuwamilikisha wananchi, inasababisha kuipotezea mapato serikali, kwani watu wanamiliki nyumba na viwanja, bila ya kulipia kodi kwa mujibu wa sheria.

Waziri anasema, taarifa za jiji hilo zilizopo wizarani kwake, zinaonyesha kuwa viwanja vilivyopimwa ni 26,500 lakini vilivyotolewa hatimiliki havizidi 23,000, hali inayofanya zaidi ya viwanja 3000 kuendelea kumilikiwa na watu, lakini hazilipi kodi.

Lukuvi huku akionyesha uerevu mkubwa katika utendaji unaohusu wizara yake, anasema ukusanyaji wa kodi za ardhi katika jiji hilo ni duni, kwani asilimia 70 ya wananchi wanamiliki nyumba na viwanja, lakini hawalipii kodi ya serikali.

Kutokana na hilo, Waziri Lukuvi anawafananisha maofisa hao na wahujumu uchumi na amewaagiza watendaji hao, kuanza kutekeleza majukumu yao ipasavyo, akiwapa muda hadi mwisho wa mwezi huu, viwanja vyote vya watu visiyolipiwa kodi, viwe vimeshaingia katika mfumo wa kodi.

Uchelewehaji hati

Baada kikao hicho kilichowaweka ‘kitimoto’ watendaji hao, Waziri Lukuvi alihamisha ziara yake katika Ofisi ya Kutunza Kumbukumbu za Idara ya Ardhi ya Jiji, alikodai kubaini udhaifu mkubwa zaidi.

Anasema, kulikuwapo ucheleweshaji wa makusudi katika utoaji hatimiliki za nyumba na viwanja zilizoombwa na wananchi, huku wengine wakiwa wamecheleweshewa kwa zaidi ya miaka 10, baada ya kukamilisha taratibu zao.

Wakati akiendelea na upekuzi, alieleza kubaini kuwapo mwananchi aliyepeleka maombi tangu mwaka 2011 na alilipia Sh. milioni 1.5, lakini mpaka sasa faili lake halijawahi kushughulikiwa na mtumishi yeyote wa idara hiyo.

Kutokana na hali hiyo, aliwaagiza Wakuu wa Idara za Ardhi katika Halmashauri zote nchini, kuwapatia hati wananchi wote waliocheleweshewa ili waanze kulipa kodi.

Pia, akatumia fursa hiyo kuwaagiza wakuu hao wa idara kumpelekea orodha ya maofisa waliochelewesha hati hizo, ili wachukuliwe hatua za kisheria, kwa madai ni kitendo sawa na uhujumu uchumi unaoipotezea serikali mapato.

“Hawa sio wajinga kuacha mafaili yote haya bila kuyafanyia kazi. Watakuwa wanatengeneza mazingira ya ‘kunywa’ na inawezekana ‘wamekunywa sana.’ Sasa nataka wote walioomba wapatiwe haraka na muanze kukusanya kodi,” aliagizwa Lukuvi.

Mkurugenzi akiri.

Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Mbeya, James Kasusura, alikiri jiji lake kutokuwa na mpangilio mzuri na zaidi ya asilimia 90 ya makazi, yako kiholela.

Kasusura anasema, katika kukabiliana na hali hiyo, tayari wamepata ufadhili wa Benki ya Dunia, kwa ajili ya kuandaa ramani ya jiji hilo na wapo katika hatua za mwisho kuanza kazi hiyo.

“Kwa sasa tupo katika harakati za kupima zaidi ya viwanja 50,000 kwa ajili ya New Mbeya City katika eneo la Nsoho na nimemtuma Ofisa Ardhi jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kwenda kuonana na wafadhili wetu, kukamilisha taratibu,” anaeleza Kasusura.

Makala akumbukwa

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Jeremia Minja, amemweleza Waziri Lukuvi, anamtaja aliyekuwa Mkuu wa Mkoa, Amos Makalla, aliyeko Katavi sasa, alifanya juhudi kubwa kuleta mabadiliko ya mpangilio wa mji.

Minja anasema, awali hali ilikuwa tete zaidi, kabla kazi hiyo ya msukumo wa Makalla kufanyika, huku akifafanua kuwapo changamoto nyingi ya migogoro ya ardhi ndani ya na mkoa kiujumla, ambayo Makalla alianzisha utaratibu wa aina yake wa kusikiliza kero na kisha kuzitatua.

Kwa mujibu wa ratiba hizo, ambazo Makalla alijiwekea, vivyo hivyo akawaagiza wakuu wa wilaya nao kuzifuata, ni kila Alhamisi, mwanzo na mwisho wa mwezi, alisikia kero za wananchi na kuzitolea maamuzi.

Vilevile, Minja anasema, lilianzishwa dawati maalumu katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, kwa ajili ya kupokea malalamiko ya wananchi na kuyaandalia utaratibu wa kuyashughulikia, hivyo migogoro mingi ikawa imepatiwa ufumbuzi.

“Hili Jiji lilikuwa na matatizo mengi. Hiki kitengo cha ardhi ndicho kilichokuwa kinalalamikiwa zaidi na wananchi, hivyo hawa wataalamu walifanya kazi ya kutatua migogoro badala ya majukumu yao na wakati huo ‘it was real worse’ (hali ilikuwa mbaya sana),” anasema Minja.

Moto wa RC

Siku chache baada ya Waziri Lukuvi kuondoka, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila ‘aliwawashia moto’ watendaji wa Idara ya Ardhi na Mipango Miji, akiwanyooshea kidole cha uzembe na ndio mzizi wa mpangilio mbovu wa makazi.

Chalamila alitoa mtazamo huo wa ukali, katika kikao kilicholenga kuhamasisha usambazaji wa vitambulisho vya wajasiriamali, pamoja na wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri zote za mkoa huo na watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),
Alitoa mfano uliobeba haiba ya aibu, kwamba Maofisa Ardhi na Mipango Miji, wamefikia hatua ya kuuza maeneo ya wazi yayotengwa na serikali kwa ajili ya shughuli mbalimbali.

Aliwapa siku 14, maofisa hao kuainisha maeneo yote yaliyotengwa kuwa ya wazi na kumpelekea orodha na baada ya hapo, ataanzisha oparesheni maalumu ya kubomoa nyumba zilizojengwa kwenye maeneo hayo.

“Waziri Lukuvi alipokuja juzi hapa alisema jiji hili limepangwa ovyo. Sasa sijui kazi ya maofisa ardhi na mipango miji ni ipi? Maana Jiji letu halina sifa kabisa, sasa nataka mniletee orodha ya maeneo yote ya wazi na kama kuna eneo mtu amejenga nyumba nitabomoa,” anatamka Chalamila.

Pia, akataja kashfa ya hatua ya maofisa hao kupima na kuuza eneo la Uwanja wa Ndege wa Zamani, huku akiapa kuwashughulikia wote waliohusika na upimaji huo.

Ardhi Mbeya yaamka

Mwishoni mwa Mwezi uliopita, ikiwa ni mwezi mmoja baada ya Waziri Lukuvi ‘kutimua vumbi,’ Halmashauri ya Jiji la Mbeya, lilitia saini makubaliano na kampuni binafsi, kwa ajili ya kuandaa mpango wa kuupanga mji huo (Master Plan).

Ofisa Mipango Miji wa Mbeya, Patrick Mwakilili, anasema ni mradi uliofadhiliwa na Benki ya Dunia, kupitia Mpango wa Uendelezaji Mji Kimkakati huku ukiwa ni mkataba wa miezi 18.

Anasema, mpango huo utahusisha upangaji wa matumizi ya jumla ya matumizi ya ardhi, huduma za kijamii na miundombinu, ili kuboresha hali ya mazingira, kiuchumi na kijamii kwa wananchi.

Mwakilili anasema matarajio ni kwamba, mpango utasaidia kuupangilia vizuri mji, huo ili kuwa na mwonekano mzuri na unaendana na hadhi ya jiji kwa muda wa miaka 20 ijayo, hadi mwaka 2039.

Meya wa Jiji la Mbeya, David Mwashilindi, anaahidi mkandarasi husika kupewa ushirikiano kwa kadri inavyostahili, katika hatua hiyo ya Jiji la Mbeya, kuondokana na makazi holela.

Anatumia nafasi yake, kuwataka watendaji wa jiji, kuweka kando siasa na kuchapa kazi kufikia malengo ya majukumu yao, akidai siasa ndio zimekuwa zinakwamisha shughuli za maendeleo.

Habari Kubwa