Daktari Bingwa: Macho kuwasha hatari yake zaidi ya unavyofikiria

17Jan 2019
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
Daktari Bingwa: Macho kuwasha hatari yake zaidi ya unavyofikiria
  • Miwani bila kupima, hatari zaidi

ASILIMIA kubwa ya magonjwa ya macho yanatibika ikiwamo upeo mdogo wa macho kuona, ambao inazuilika kwa miwani, endapo mtu akiwahi katika kituo cha kutoa huduma ya afya.

Daktari bingwa wa macho, Profesa Ugurcan Keskin, kutoka International Eye Hospital, akimpima macho mgonjwa aliyefika hospitalini hapo. PICHA: SABATO KASIKA.

Ni kauli ya Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Eliud Eliakimu, aliyoitoa kabla ya maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Afya ya Macho Duniani, Oktoba mwaka jana, jijini Dodoma.

Maadhimisho ya Siku ya Afya ya Macho Duniani yalifikiwa na Lions Club International Foundation mwaka 1998 na baadaye kuungwa mkono na wadau wengine wa huduma za macho.

Hao wanajumuishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), Muungano wa Mashirika ya Kimataifa yanayojihusisha na Huduma za Macho, serikali na wataalamu wa afya, taasisi na watu binafsi.

Mtazamo wa jumla ni kufanikisha Dira ya Kimataifa ya Kutokomeza Upofu Unaozuilika Duniani, ifikapo mwaka 2020 kwa kuthamini haki ya kuona kwa wote, ambayo serikali ya Tanzania iliridhia na kuungana na mataifa mengine duniani kutekeleza azimio hilo, tangu mwezi Mei mwaka 2003.

Kwa mujibu wa makadirio na takwimu za WHO, asilimia moja ya Watanzania hawaoni na kwa ujumla watu wote wenye matatizo ya kuona kwa viwango mbalimbali nchini wanakadiriwa kuwa ni mara tatu ya watu ya wasiyoona ambao ni takriban watu 1,730,000.

MTOTO WA JICHO

Inaelezwa, matatizo makubwa ya upofu unaoweza kuzuilika nchini na dunia kwa ujumla ni mtoto wa jicho, shinikizo la jicho, matatizo ya ‘retina’ ni pamoja na yatokanayo na ugonjwa wa kisukari na umri mkubwa.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alishakaririwa akisema bado jamii ina matatizo mengine ya macho yanayohitaji ushauri wa kitabibu.

Katika kukabiliana na matatizo haya, wadau mbalimbali wa afya ya macho wamekuwa wakisaidiana na serikali kuhakikisha Watanzania wanapata tiba ya uhakika.

DALILI ZAKE

Tabibu Bingwa wa macho katika hospitali iitwayo, International Eye Hospital, jijini Dar es Salaam, Profesa, Ugurcan Keskin, yumo katika orodha hiyo ya matabibu.

Dk. Keskin anataja dalili hatari, zisizopewa uzito na jamii kuwa ni macho kuwasha, kutokwa machozi, kuogopa mwanga, jicho jekundu na kufikicha macho kila wakati.

Anafafanua kuwa, dalili hizo zinaweza kuchukuliwa na jamii kama jambo la kawaida, lakini ukweli ni kwamba, hicho ni kisababishi cha uoni hafifu.

"Kumekuwa na mazoea kwa baadhi ya watu kupenda kukimbilia kumeza dawa waumwapo kichwa, bila ya kujua ni moja ya dalili ya kuugua macho.

‘Wengine ambao hawapati dalili za wazi hadi wanapofikia hatua ya kuwa vipofu kabisa, ndipo huenda kwa wataalamu wa macho na kujikuta wakiwa hawaponi kwa sababu ya kuchelewa," anasema Dk. Keskin.

Anasema kuna faida kubwa ya kupima macho mara kwa mara na kupatiwa tiba husika, kuliko kusubiri hadi ugonjwa unapojitokeza.

"Magonjwa ya macho yapo mengi, mengine yanasababishwa na nzi, kama vile trakoma na mengine hutokana na mionzi, inayoweza kuwa ya jua na runinga, ambavyo vinasababisha macho kutofanya kazi vizuri kama kuona mbali na kuona karibu na pia kichwa kuuma," anasema.

Anaainisha magonjwa yote yanatibika, inategemea hatua ya ugonjwa huo wa macho ilipofikia, kama kuona karibu anaweza kupona kwa kutumia lenzi mbonyeo na kuona mbali unatumia lenzi mbinuko katika miwani.

"Hii inasaidia mgonjwa kuona vizuri na kuweza kutofautisha vitu mbalimbali na pia ukihisi kama macho yako yanauma, unaweza ukala karoti kwa sababu ina Vitamini A inayoweza kukusaidia ukiwa na ukavu macho," anasema.

USIVAMIE MIWANI

Dk. Keskin anasema, kuna baadhi ya waliozoea kununua miwani na kuivaa bila ya kupatiwa ushauri wa kidaktari, kwamba ni kosa.

"Watu waepuke kununua miwani, kabla ya kuonana na wataalamu waliosomea, waweze kuwashauri na kuwapima, ndipo ijulikane kama wanatakiwa kuvaa miwani au hapana," anasema.

Anasema lengo la kuona wataalamu wa macho, ni njia ya kupata uridhisho na kupewa dawa inayostahili, tofauti na kumeza dawa bila ya kuwaona wataalamu.

"Yaani ni vyema mtu mwenye tatizo la macho, kabla ya kununua dawa na kuvaa miwani aonane na wataalamu wa macho au kliniki za macho zinazotambulika na kufanyiwa vipimo ili kubaini tatizo," anasema.

Dk. Keskin anasema, hata ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu, wanapaswa kuonana na madaktari wa macho kufanyiwa kipimo maalumu kila mwaka ama mara moja au mbili, kubaini athari za magonjwa.

Anasema huduma zote za kutibu maradhi hayo zinapatikana katika hospitali zenye vifaa bora, ambavyo vinavyotambua dalili hatarishi za ugonjwa kirahisi.

Habari Kubwa