Darasa la w/ke wauza dagaa DRC

27Aug 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Darasa la w/ke wauza dagaa DRC
  • *Waambiwa itumieni SIDO, h/shauri
  • *Wanunuzi wenu wasiingie ‘jikoni’

“NATAKA kutoka kimaisha, lakini mambo ni magumu. Biashara ya dagaa haijaweza kutufikisha kule tunapopata. Kwa miongo mingi tumeuza dagaa, lakini nyumba zetu ni duni. Angalia ni za makuti na udongo.”

Anasema Fatuma Machalila, mkazi wa Kilwa Masoko, mkoani Lindi, ambaye mapema mwezi huu anatembelewa na wanahabari kufahamu mafanikio na changamoto kwenye biashara ya dagaa inayofanywa na kinamama wengi wilayani humo.

Anasema biashara hiyo haijatengamaa kwani hawana soko la uhakika mnunuzi mkubwa wa dagaa zao ni wafanyabiashara wa Congo, lakini hawajaweza kunufaika kutokana na kukosa mitaji, teknolojia na miundombinu duni wanayotumia kukausha samaki hao.

Mwanamama huyo, anawaambia wanahabari wanaotembelea mafanikio ya kazi za kuhamasisha wanawake kujiinua kiuchumi inayofanywa na SHirika la Action Aid Kilwa, kuwa wanakausha dagaa kwa jua kwenye vichanja na msimu wa mvua hakuna jua, hali ni mbaya zaidi, anasema mwanamama huyo aliyeanza biashara hiyo, 1993.

Pia anasema hawana utaalamu wa kuzichambua kimadaraja, kuzifunganya na kuweka lebo, ili zifike sokoni zikiwa zimeongezewa thamani.

Fatuma ni miongoni mwa wanawake wengi Kilwa waochakata mazao ya samaki, wanaiona kuwa ni pasua kichwa.

Wanaeleza kuwa kinachowakwamisha ni kukosa mitaji hivyo wanasubiri ‘tajiri’ kutoka Congo, awape ‘oda’ na kuwaachia fedha za kufanyia kazi hiyo na wanachofanya ni mbinu za kupata fedha kidogo baada ya kuandaa shehena ya mteja.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake anasema, wanakosa teknolojia na miundombinu ya kufanikisha mnyororo mzima wa biashara hiyo, kuanzia wanapowatoa baharini hadi kumuuzia mteja.

Ili kufahamu namna ya kuwasaidia, Nipashe inazungumza na Ofisa Miradi na Mchambuzi wa Sera, kutoka Shirika la Usimamizi wa Mazingira na Uchumi (EMEDO), Lawrence Kitogo , ambalo pia hufanyakazi na kinamama wachakataji wa mazao ya samaki, anaeleza mambo ya kuwasaidia.

Anasema mtandao wa wanawake wanaochakata mazao ya samaki umesambaa maeneo mengi, wako baharini, maziwani kama Victoria, Tanganyika, Nyasa, mtoni mfano Kilombero na Mtera, pia wapo kwenye mabwawa kama Nyumba ya Mungu.

Anasema tatizo kubwa ni kukosa miundombinu na teknolojia ya kuchakata kuanzia ya kuvua dagaa majini, upokeaji bidhaa hiyo wavuvi wanapofika pwani, vibebeo, vifaa vya kuwasafishia, kuchuja maji, kuwakausha, kuwachambua, kuwaweka kwenye madaraja, kuwafungasha na kuweka lebo.

Kitogo anasema baadhi ya wajasiriamali wanaochakata mazao hayo wanakosa teknolojia hiyo.

Anataja mathalani, ubebaji hufanyika kwenye ndoo za kawaida, lakini kuna matenga ya plastiki maalumu ya kubebea dagaa.

Kitogo anafafanua kuwa dagaa wanaanikwa kwenye chanja, lazima ziwe za kisasa siyo kutumia vyandarua au nyavu za mbu zinazowekwa madirishani na kufunikwa na nailoni au maturubai.

“Vichanja kama sehemu ya miundombinu vinahitajika viwe vya kisasa vya kupokelea, kuchambulia ili kuondoa taka kama uduvi, konokono na taka bahari. Vichanja vya kuchambua na kutofautisha ukubwa navyo ni muhimu. Vingine ni vya kuzikaushia maji na kuanikia kwa kutumia teknolojia ya kisasa,“ anaelezea Kitogo.

Ofisa Miradi na Mchambuzi wa Sera, kutoka EMEDO anasema kina mama hao ni wanachama wao na kwa Tanzania nzima, kuna mashirika zaidi ya 260 ya vikundi vya wafanyabiashara hao zaidi ya 2,000 wanaochakata mazao ya samaki.

“ Wapo wanaoshughulika na dagaa kwenye maji ya chumvi baharini mathalani Kilwa na Tanga, wengine wapo kwenye maji madogo haya ni mabwawani na mtoni na wapo kwenye maji ya baridi ndani ya maziwa mbalimbali kama Victoria na Tanganyika, ambao kwa kukosa miundombinu wanapata matatizo haya.“

Akizungumzia athari za wafanyabiashara kuwafuata wachakataji nyumbani na kuwapa mitaji na `oda‘ au kuruhusiwa kufika kwenye kambi za wavuvi na kutoa maelekezo ya kile wanachotaka siyo biashara endelevu.

“Wafanyabiashara wanatakiwa wafike sokoni tu. Siyo kwenye kambi za wavuvi wanapokwenda huko wanaweza kununua bidhaa bila kuwa rekodi. Biashara hiyo inazikosesha halmashauri na mamlaka za mapato mapato na takwimu sahihi za bidhaa na ushuru. Wabanwe kwa kutumia sheria, ili wafuate utaratibu.“

Anataja hasara nyingine kuwa wajasiriamali hao wanashindwa kuchakata kwa viwango vya kufungasha na kuweka lebo na kuuza kwa uzani unaokubalika kama gramu na kilo.

“Kukosa vipimo rasmi kunasababisha wapate hasara ya kuuza kiwango kikubwa kwa gharama ndogo.

Ikumbukwe kazi ya kuchakata inaanzia kuwatoa baharini hadi kuwauza kwa mteja, ikipitia hatua nyingi. Tena wanauza dagaa wakavu, lazima kuwe na utaratibu bora wa kuuza kwa mteja wa mwisho, ili kupata faida na si hasara.“

“Wanapata hasara baada ya mavuno `post harvest loss`

Iwapo hakuna ufungashaji na lebo makini wanunuzi wanaweza kufungasha upya na kuziongezea thamani bidhaa hizo na kupata faida kubwa zaidi hasa inapokwenda nje ya nchi.“

Mazao ya samaki kama dagaa na vibambara au makayabo yanaelezwa kuwa yanatokea Congo husafirishwa nje ya nchi na kufikishwa mji wa Matonge huko Ubelgiji, pia huuzwa katika miji mingine ya Afrika, licha ya kwamba nchi hiyo haina bahari.

UFUMBUZI UNAOPENDEKEZWA

Kitogo ambaye shirika lao linashughulikia mazingira ikiwa ni pamoja na bahari, maziwa na mito, misitu na ardhi, anashauri Wizara ya Mufugo na Uvuvi na halmashauri iwawekee miundombinu na teknolojia ya kukaushia iwe ya gesi, umeme na jua, ili waachane na kuni. Moshi unaharibu bidhaa hizo.

“Iweke viwanda vidogo vidogo, vyenye vichanja, vya kusafisha, kuchambua, kuangalia wakubwa na wadogo, kuchemsha, kukaanga, kukausha, kufunganya kwenye uzito mbalimbali na kuweka lebo...“

Wizara ya Mifugo na Uvuvi ione kama ni hitaji la kinamama wengi na ichukue hatua.

UHIFADHI NI MUHIMU

Akizungumzia namna ya kuboresha soko hilo mchumi na mtafiti Dk. Deogratias Lwezaura, anasema pamoja na kupewa utaalamu wa kisasa wa biashara hiyo, wachakataji hao wa mazao ya samaki watafanikiwa iwapo Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na halmashauri  zitawapatia teknolojia inayoanzia kuwavua majini hadi kuwaweka lebo na kuwauza, ili wafanye shughuli zao kisasa kwa faida zaidi.

“Juhudi hizi ziende pamoja na kuwapatia sehemu za kuhifadhi ‘cold rooms‘ wahifadhiwe kwenye majokofu kila wanapovua, ili kila wakati dagaa wapatikane kusiwe na madai kuwa hawapo, kwa sababu ya upepo au mvua.“

Anashauri kuwa katika uwekezaji huo, vikundi visaidiwe kila kimoja kiwe na lebo yake, ili vifanyekazi kwa utaalamu na kwa ushindani zaidi kuongezea dagaa thamani na kujielekeza kwenye ufanisi zaidi.

Dokta Lwezaura Meneja Mipango na Tathmin wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo TARI-Dodoma, anakumbusha kuwa katika biashara hiyo hakuna haja ya kuwa na mwekezaji mkubwa, badala yake wizara na halmashauri ziwawezeshe wajasiriamali, ili kuinua uchumi wa watu wa chini na kubadili maisha yao.

Anasema kupitia mikopo ya halmashauri ya vijana , wanawake na watu wenye ulemavau hilo linaweza kufanyika. Anasema hayo alipoulizwa iwapo wanaweza kutafutiwa wawekezaji wakashirikiana nao.

SIDO YAWASHAURI

Mhandisi Profesa Sylivester Mpanduji ni Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO), anasema teknolojia za ukaushaji dagaa zipo na zinatumiwa na wanaochakata mfano Mwanza, Kigoma na hivi karibuni wamepokea maombi kutoka kwa wajasiriamali wa Zanzibar.

Anaongeza kuwa wanatoa mafunzo ya kuboresha uchakataji dagaa, ukaushaji na kufunganya kitaalamu na kwamba SIDO Lindi, inaweza kuwasaidia kwenye eneo hilo.

Anataja teknolojia hizo kuwa ni ya kukausha kwa nishatijua na nyingine ni ya mkaa kidogo inayotumia feni zinazotoa upepo mwingi kukausha dagaa hizo kwa ufanisi.

Anawashauri wachakataji hao kama tatizo ni mitaji kuomba fedha za halmashauri kupitia mikopo ya wanawake , wenye ulemavu na vijana pamoja mikopo ya SIDO kwa vile suala hilo limeshapatiwa ufumbuzi.