Dawati la jinsia na watoto ni msaada kwa waathirika wa ukatili

15Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Dawati la jinsia na watoto ni msaada kwa waathirika wa ukatili

MKOA wa Iringa umefanikiwa kubaini, kuzuia, kupambana na kutanzua uhalifu kutokana na jitihada mbalimbali zinazoendelea kufanywa kupitia vikosi vyake vikiwamo vya Polisi Jamii, Dawati la Jinsia na Watoto pamoja na doria zinazofanyika mara kwa mara.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Juma Bwire Makanya. PICHA: MTANDAO

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Juma Bwire Makanya, anasema ushirikiano bora uliopo baina ya vikosi vyote ndiyo chachu ya mafanikio chanya ya mkoa kuwa na lengo na dhana moja.

Dawati la Jinsia na Watoto na Polisi Jamii vitengo hivi vimekuwa msaada mkubwa kwetu katika kupanga mikakati ya kubaini, kuzuia, kupambana na kutanzua uhalifu.

Tunaendelea kutoa elimu shuleni, ambapo wanafunzi wamepewa ufahamu wakujilinda wenyewe, kutoa taarifa pale wanapoona kuna matishio yakiwamo ya udhalilishaji wa kingono na ubakaji hususani shuleni, nyumbani wanapoenda na kurudi katika shughuli zao.

Vilevile hufanyika mikutano ya hadhara kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi kuachana na tabia zinazosababisha unyanyasaji wa kingono, ukatili wa kijinsia na ubakaji.

Dawati la Jinsia hushirikiana na taasisi zisizo za kiserikali kupeleka elimu hiyo maeneo ya vijijini, ambapo matukio ya aina hiyo hutokea lakini hushindwa kuripotiwa kwa wakati katika vituo vya polisi.

Taarifa zinaonyesha baadhi ya wazazi hasa wa vijijini mara nyingi wanashindwa kulea watoto inavyotakiwa ikiwamo kutowasikiliza au kuwashauri katika masuala ya mahusiano ya kimapenzi, hali inayosababisha watoto kudhalilishwa au kutendewa matukio ya kingono bila kuyatolea taarifa kwa wazazi.

Jitihada za elimu zinazoendelea kutolewa zimesaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa matukio hayo, hatua hiyo imetokana na umakini na weledi wa askari wa kitengo hicho ambao hutumia taaluma kukamilisha majukumu yao.

Mikakati mingine ni kuwajengea uwezo wafanyakazi na wafanyabiashara na wafanyakazi wa taasisi nyingine ili kubaini mbinu za uhalifu kabla na baada kwa kuwa uzoefu unaonyesha kuwa matukio mengi ya uhalifu yanayotendeka yanatokana na uvujaji wa taarifa kutoka kwa wafanyakazi hao.

Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Deusdedit Kasindo, anasema uhalifu na wahalifu wamedhibitiwa kwa kiasi kikubwa kwa kipindi cha robo mwaka kuanzia Januari hadi Machi 2018, ilhali makosa makubwa ya jinai yaliyoripotiwa yalikuwa 295 ikilinganishwa na makosa 338 yaliyoripotiwa kwa kipindi hicho mwaka 2017 ikiwa ni punguzo la makosa 43 ambayo ni sawa na asilimia 12.

Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kuendelea kuamini kazi zinazofanywa na jeshi hilo kupitia vitengo vyake hususani kitengo cha Polisi Jamii na Dawati la Jinsia na Watoto na kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili kusaidia kazi za polisi katika mkoa wa Iringa.

Imetolewa na kitengo cha Uhusiano, Polisi Makao Makuu, Dar es Salaam. Barua pepe [email protected] au [email protected]gmail.com