DC Ngaga aingilia kati mwanafunzi kuolewa kisa Ng'ombe

02Jul 2020
Neema Emmanuel
MWANZA
Nipashe
DC Ngaga aingilia kati mwanafunzi kuolewa kisa Ng'ombe
  • Aingilia kati binti asiozeshwe, arudi shule kutimiza ndoto zake...

Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Senyi Ngaga, ametibua mpango wa ndoa ya mwanafunzi wa Kidato cha Kwanza katika Shule ya Sekondari ya Tallo iliyopo Kijiji cha Mwankuba wilayani humo.

Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Senyi Ngaga akizungumza na mwandishi wa habari hii (hayupo pichani).

Akizungumza na mwandishi wa Makala hii, Mkuu wa Wilaya Ngaga alisema binti huyo Pili Misungwi (siyo jina lake halisi) mwenye miaka 13 alitaka kuozeshwa na baba yake kwa lengo la kujipatia Ng’ombe.

Alisema alipopata fununu za kuozeshwa binti huyo kinyume na sheria aliingilia kati kwa kuwakamata wazazi kitu ambacho kilisaidia mtoto huyo kuendelea na masomo huku kiongozi huo akieleza kuwa Ng'ombe katika jamii ya Kisukuma ni muhimu kwani ni ufahari kumiliki Ng'ombe. 

"Mtoto huyo hakupenda kuolewa kabisa na ndiye aliyetoa taarifa baada ya kuona harakati za kuozeshwa, kesi ipo Mahakamani kwa kushirikiana na vyombo vya usalama tulifanikiwa kumunusulu na sasa anaendelea na masomo yake vyema huku hatua za kisheria zikiendelea," alisema Ngaga. 

Baba wa binti aliyenusulika kuolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Nyamasele Nyanda akiwa kwenye picha ya pamoja na Mwandishi wa Makala hii.

BABA MZAZI AELEZA 

Baba mzazi wa binti huyo, Nyamasele Nyanda mwenye watoto 14 ambapo wa 13 ndiye alitaka kumuozesha, alisema kuwa amejifunza na kwamba hatofanya tena kosa hilo na kwa sasa ameahidi atampatia elimu mtoto wake anayostahili.

"Nikimuozesha mtanikamata kwa sasa nimemuacha asome hadi pale atakapoishia yeye mwenyewe sasa yupo kidato cha pili siwezi kabisa kumuozesha… akiwa anasoma lakini akishindwa ataolewa akifaulu ataendelea na masomo yake sasa kazi kwake kusoma kwa nguvu zote"alieleza Nyanda.

Aliongeza kuwa baada ya elimu aliyopewa na Mkuu  wa Wilaya hiyo ameondoa ubaguzi kwa watoto wa kike ambao kwa sasa ana wajali na kuwapa mahitaji yao sawa na wakiume ambao alikuwa anawapa kipaumbele kipindi cha nyuma.

"Mwanangu anaenda shule vizuri siyo mtoro ,mimi mwenyewe baba yake nipo lazima atasoma tu "anaongeza Nyanda.

MWALIMU ANENA

Mwalimu wa Shule ya Sekondari Tallo, ambayo anasoma binti huyo ambaye akupenda kutaja jina lake alisema wazazi wengi wanapenda Ngo'mbe na wakishazipokea visingizio vinakuwa vingi na mtoto anaacha shule wakati mwingine wanatumia mbinu ya kuwataka wafanye vibaya ili matokeo yakitoka watumie nafasi hiyo kumuoza.

Alisema mazingira ya kukaa nyumbani watoto wa kike ni hatari hivyo jambo jema ni ujenzi wa mabweni ,kuwaweka karibu kutasaidia kuwalinda , kuwaepusha na vishawishi mbalimbali ambavyo wakiwa nyumbani wanakumbana navyo.

“Binti anaendelea vizuri na masomo na ata leo alikuwa hapa kuchukua maswali ya kufanya nyumbani (siku tatu kabla shule hazijafunguliwa), Mkuu wa wilaya anafanya kazi kubwa sana na inawezekana jamii inamuelewa kwa kuwa yeye pia ni mwanamke na yanayotendeka yanamgusa moja kwa moja “anaeleza Mwalimu.

OFISA MTENDAJI KATA & OFISA TARAFA, MTUMISHI

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Nyambiti, Mongo Mbombile alisema matukio ya kuwaozesha watoto yapo huku akiwanyooshea vidole wazazi kwa kupenda mifugo kuliko elimu itakayomleta mtoto msingi wa kufanya maamuzi sahihi na  maisha bora.

"Wazazi sasa wana mbinu mpya ya kuomba uhanisho ,usifikilie ukimpa mtoto ataenda kusoma hapana hiyo ni tiketi ya kwenda kumuoza hivi sasa kuna utaratibu mpya kwa watoto wanaohamishwa wengi wakielekea Mpanda hasa wa kike hao wanaenda kuolewa tunamshukuru sana Mkuu wa Wilaya alilisimamia hilo la mtoto kutaka kuolewa na kumnusuru katika kifungo hicho" alieleza Mombile.

Naye Ofisa Tarafa ya  Ibindo, Jeremiah John alisema tatizo wazazi wengi hawajui umuhimu wa mtoto hivyo jukumu walilonalo ni kuwakamata  wazazi,ndugu na marafiki wataohudhuria siku ya utoaji wa mahali kwa mtoto ambaye ni mwanafunzi na kuwafikisha kwenye vyombo husika ili sheria ichukue mkondo wake.

Afisa Tarafa ya Ibindo, Wilaya ya Kwimba, Jeremiah John akizungumza na Mwandishi wa Makala hii.

"Hivi karibuni kuna binti alifaulu kuingia kidato cha kwanza lakini tayari baba yake alikuwa ashachukua mahali tuliingilia kati… kuna mwingine walikuwa ndio wanapokea mahali tuliwasomba watu wote waliokuwa eneo la tukio hiyo pia ilisaidia kwani sasa matukio yameanza kupungua" alieleza John.

Aliongeza kuwa kwa kushirikiana na ngazi mbalimbali ikiwemo ofisi ya mkuu wa Wilaya na vyombo vya usalama wanafatilia sana ambapo ufatiliaji huo umesaidia kujenga hofu kwa jamii na kuachana na matendo hayo.

Pia John Buluhya, Mchungaji wa Kanisa la Africa Inland Church Tanzania (AICT) Nyambiti alisema jamii ibadilike na kutenda mambo mema kwani wote ni watoto wa baba mmoja na kuachana na kufanya vitendo ambavyo vinarudisha nyuma maendeleo yao na nchi kwani kumuoza mtoto bila ridhaa yake nikumfanyia ukatili na kumuharibu kisaikolojia mwisho wa siku kujiona yeye ni mtu asiye na maana katika hii dunia.

“Hata maandiko matakatifu yanatuelekeza Mkamate sana elimu usimwache aende zake maana yeye ni uzima wako hivyo yatupasa kuyazingatia hayo kwa vitendo “alisema

Habari Kubwa