DC: Tutawapima wanafunzi wote baada likizo ya Covid-19

21May 2020
Yasmine Protace
Mkuranga
Nipashe
DC: Tutawapima wanafunzi wote baada likizo ya Covid-19
  • M/kiti: Mashine X –ray imetua

NI takriban miezi mitatu, tangu ugonjwa wa corona kuingia nchini. Serikali baada ya kuona mambo sivyo, iliagiza kufungwa kwa shule na vyuo, ni kuwabakisha majumbani wanafunzi, kuwaepusha wasipate maambukizo ya ugonjwa huo.

* Wanafunzi wa eneo la Vikundu, Mkuranga katika moja ya matukio ya ugeni uliowahusu. PICHA: MTANDAO.

Kukaa nyumbani ni moja ya jitihada za kuwapunguzia wanafunzi wasirundikane katika madarasa, hosteli au bwenini, iwe vyuoni au shuleni.

Katika kuepuka ugonjwa huo, kikubwa kinaelezwa ni kukwepa mikusanyiko, hivyo wanafunzi wakatakiwa kutoendelea na masomo kutokana na mikusanyiko.

Pamoja na katazo hilo, bado kuna baadhi ya maeneo watoto wadogo ambao ni wanafunzi, bado wanazurura ikiwamo katika baadhi ya masoko na vituo vya daladala, wakiendelea na biashara ndogo.

Siku chache zilizopita, Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Filbeto Sanga, katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Mkuranga, alieleza kusikitishwa na baadhi ya wazazi wanaowaruhusu watoto wao kufanya biashara ndogo katika maeneo mbalimbali ya wilaya, badala ya kutulia nyumbani.

"Kupitia viongozi wetu, tunatakiwa maagizo tuyatii. Watoto wakae nyumbani, wasijiingize katika makundi, pia hata biashara wanazofanya sio sahihi," anasema.

Anaongeza kutokana na ukweli kwamba baadhi yao wanaishia kuzurura mitaani, wanatarajia shule zitakapofunguliwa; msingi na sekondari, watawapima ujauzito.

Pia, Sanga anatoa agizo kwa watendaji wa kata zote wilaya kwake, kwamba waendelee kutoa elimu ya afya na uzazi kwa wazazi na walezi wa wanafunzi hao wa shule, ikilenga mahsusi kuwaepusha na mimba zisizotarajiwa hasa kipindi hiki cha mapumziko ya kupisha janga la corona.

Anaeleza kusikitishwa na baadhi ya wazazi wanaokaidi agizo la kiserikali, ambalo linawasaidia watoto kubaki nyumbani na wakati huohuo, wakijiepusha na vitendo vitakavyoathiri elimu yao, shule zitakapofuguliwa.

Sanga anaitaka jamii iendelee kuchukua hatua kuhusu kujikinga na ugonjwa huo, serikali ikiendelea kuwaunga mkono kwa kuielimisha jamii namna ya kujikinga na maambukizo ya ugonjwa huo.

Anataja msaada mwingine ni vitakasa mikono vilivyopo katika maeneo mbalimbali yenye mwingiliano wa watu wanakofika kupata mahitaji hasa ya lazima, kama vile hospitali na sokoni.

Pia, ana rai anayowaendelezea wananchi kuendelea kuvaa barakoa, huku madiwani waendelee kuwahamasisha kuchukua tahadhari zinazohusu ugonjwa huo.

Sanga anasema, kuibuka corona isiwe kigezo cha watu kushindwa kuwahudumia wananchi kwa kukaa majumbani, bali kinachotakiwa ni kutoogopa ugonjwa, huduma ziendelee zinavyokusudiwa.

X- RAY YATUA

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Mkuranga, Juma Abeid, anazungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani, kwamba kuna hatua waliopiga kwa serikali kuu kuwapatia huduma za X- ray katika Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga.

Mwenyekiti Abeid, anasema kabla ya msaada huo uliotolewa na Rais Dk. John Magufuli, na wagonjwa walienda kupata huduma hiyo nje ya wilaya na hasa mkoa jirani, kwenye Jiji la Dar es Salaam.

Mwenyekiti huyo kupitia nafasi yake, ni miongoni mwa waliofanikisha zahanati na vituo vya afya kujengwa katika maeneo mbalimbali ndani ya Wilaya ya Mkuranga.

Habari Kubwa