Demokrasia iwaunganishe Watanzania

31Aug 2016
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
Demokrasia iwaunganishe Watanzania

WATAALAMU wanasema kuwa mfumo wa demokrasia unatoa msukumo wa maendeleo ya uchumi ya muda mrefu, kwa kuhakikisha kuwa kuna utulivu wa kisiasa kwenye nchi husika.

Uongozi wa serikali unaopatikana kikatiba kupitia uchaguzi ulio huru na wa haki, unajenga uhalali wa mfumo mzima wa utawala na serikali iliyoko madarakani.

Mfumo wa demokrasia unaoambatana na utawala wa sheria.

Katika mfumo wa demokrasia, serikali inakuwa ya uwazi na inawajibika kwa wananchi kupitia Bunge.

Vyombo vya habari vilivyo huru, vinafuatilia vitendo vya serikali na kashfa zinafichuliwa hadharani.

Ahadi za serikali za utoaji wa huduma za jamii, ujenzi wa miundombinu ikiwamo ya barabara na mingine unafuatiliwa kikamilifu.

Katika hilo, serikali inayoshindwa kutimiza ahadi zake inaadhibitiwa wakati wa uchaguzi.

Kazi ya serikali ni pamoja na kuweka sheria na taratibu zitazoheshimiwa na wote na watakaokiuka wataadhibiwa ipasavyo.
Polisi na mahakama wafanye kazi kwa kufuata sheria na kutoa haki.

Binafsi sina mashaka na dhamira ya Rais Dk. John Magufuli ya kutaka nchi ibadilike, ifikie maendeleo endelevu ili viongozi watakaokuja baada yake waendeleze pale atakapokuwa ameishia.

Hivyo, ili afikie maendeleo hayo ni lazima awe na mipango ambayo itamfikisha huko alikokusudia.

Na ndiyo maana amekuwa akisisitiza umuhimu wa kuachana na malumbano ya kisiasa na kujikita kwenye maendeleo.

Ajenda yake kuu ni maendeleo, hivyo ili kuyafikia hana budi kuwa na mikakati ya kumfikisha pale anapokusudia.
Kubwa zaidi, likiwa ni kwa Watanzania, bila kujali itikadi zao za kisiasa kuunga mkono juhudi zake ili aweze kufanikiwa katika nia yake hiyo.

Maendeleo yana maumivu yake, kwa kuwa siyo rahisi kuendelea bila maumivu.

Na ndiyo maana sasa kuna malumbano katika uga wa kisiasa, hasa baada ya Rais Magufuli kusema kuwa anataka maendeleo na kuamua kusitisha mambo mengine yakiwamo ya kisiasa.

Kimsingi ni kwamba uamuzi wa Rais Magufuli una maumivu kwa upinzani na kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Na kwa sababu lengo ni maendeleo, basi wahusika wa pande zote hawana budi kukubaliana na hali halisi, ama kutafuta njia nyingine ambayo itawawezesha kufanya siasa.

Ninasema hivyo kwa sababu, siasa ni endelevu hata baada ya kumalizika kwa uchaguzi.

Lakini ipo haja ya kupima hoja na kufanya siasa bila kuathiri upande mwingine, ambao umejikita kwenye maendeleo ya nchi.

Kwa vile demokrasia ina msukumo wa maendeleo, basi wanasiasa waitumie vizuri kwa manufaa ya nchi, badala ya malumbano yanayoendelea sasa na hasa kuhusu hatua ya Rais Magufuli kuzuia shughuli za kisiasa hadi mwaka 2020.

Siyo vibaya rais kusikiliza malalamiko ya wale wanaopinga kauli yake ya kuzuia siasa hadi mwaka 2020, na kuangalia uwezekano wa kuwaruhusu waendelee na shughuli zao ili wamsaidie kuhamasisha maendeleo.

Kimsingi ni kwamba, wote lengo lenu ni moja la kujenga nyumba moja ambayo ni Tanzania.

Kwa hivyo hakuna haja ya kugombania fito, kama ilivyo sasa ambapo wanasiasa wanavuta upande wao, huku serikali nayo ikivuta upande wake.

Malumbano ya kisiasa hawezi kuleta maendeleo, zaidi sana nchi inaweza kuendelea kupiga hatua kidogo badala ya kuharakisha kufikia maendeleo endelevu ambayo Watanzania wanayataka.

Demokrasia iwaunganishe Watanzania kwa ajili ya maendeleo ya nchi yao, badala ya kuwatenganisha kwa misingi ya itikadi ya vyama vyao, huku kila upande ukijiona kama una haki ya kufanya jambo fulani.

Siyo vibaya pande hizi mbili zikakaa pamoja na kumaliza malumbano haya ambayo binafsi ninaamini kwamba yanaweza kumalizika na kuzifanya shughuli za maendeleo kufanyika kwa ufanisi zaidi.

Rais amekuwa akihimiza kwamba anataka maendeleo bila kujali vyama na ndiyo maana aliwahi kutoa kauli kuhusu 'figisufigisu' za uchaguzi wa Meya wa jiji la Dar es Salaam.

Alisema kuwa anataka maendeleo bila kujali kwamba meya amechaguliwa kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ama CCM.

Hiyo ni kwa vile anatambua kuwa, maendeleo ya nchi hayana itikadi za vyama vya siasa.

Kwa maana hiyo, demokrasia ya mfumo wa vyama vingi isiwagawe Watanzania na kujiona wengine bora bali iwaunganishe kuwa kitu kimoja, wakikosoana kwa hoja zinazojenga na siyo zinazowavuruga.

Habari Kubwa