DESTURI ZA KISHAPU

01Sep 2016
Christina Mwakangale
aliyekuwa KISHAPU
Nipashe
DESTURI ZA KISHAPU
  • Mimba si kesi: wazazi wanapenda kuoza mabinti kuliko kusomesha

JUMAMOSI iliyopita katika gazeti la Nipashe, kulikuwapo simulizi ya msichana Mariam Shishi (17), kutoka Kata ya Maganzo, aliyemo katika orodha ya wanafunzi wilayani Kishapu wanaopata mimba kila mwaka.

Mwanaume mkazi wa kijiji cha Masagala, katika Kata ya Maganzo, wilayani Kishapu, akiwa amefikishwa katika kituo cha Polisi akituhumiwa, binti yake mwenye umri wa miaka mitatu, katika tukio analidaiwa kulifanuya kila mara. PICHA: MTANDAO.

Ni matokeo ya mfumo wa maisha uliowatawala mahali hapo. Miongoni mwa kasoro zilizopo ni maisha yaliyotawaliwa na mila potofu, isiyothamini hadhi ya mtoto wa kike.

“Taarifa za wanafunzi (wasichana) hawa zinafahamika, lakini zinashindwa kwenda mbele kutokana na ushirikiano mdogo kutoka kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla, kwani wanashindwa kuelezea na kuwataja wahusika. Hata kama wanawajua,” anasema Ofisa Mtendaji wa Kata ya Maganzo, Nunya Chege.

Imani potofu, mila, desturi, pamoja na utamaduni katika eneo husika, zinatajwa kuwa sababu zinazoathiri maisha ya wasichana katika eneo hilo.

KWA VIPI?
Mbali na kauli za wenyeji, takwimu za kitafiti zilizotolewa na taasisi mbalimbali, ikiwamo Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu Duniani (UNFPA), mwaka 2010 ilibainika asilimia 59 ya mimba zinazopatikana kwenye umri mdogo nchini, lipo mkoani Shinyanga.

Baadhi ya wakazi wa Kishapu wanaamini mtoto wa kike hastahili kusoma, jambo linalowafanya waishie katika kutopewa kipaumbele kwa masomo yao.

Mkazi wa Maganzo, Kabula Josephat, anasema kuna wazazi na walezi waliojenga imani kwamba, msichana anapopevuka, anahitaji kutolewa mahari na kuolewa na si lingine katika maisha yake.

“Ni wazazi wachache sana katika kata hii ambao wana nia ya kumsomesha mtoto wake wa kike. Binti akishapevuka, mzazi anawaza kumuozesha hata kama anasoma na anafanya vizuri darasani,” anasema Kabula.

Kuwapo shuguli za kiuchumi za jamii, zilizoegemea katika uchimbaji wa madini kwa miaka mingi na wengine wakitegemea vibarua vya Mgodi wa Almasi wa Mwadui uliopo umbali wa kilomita nne kutoka Maganzo. Hilo ni janga jingine kwa mabinti wa Mwadui.

Mmoja wa wakazi hao, , Abdul Almasi, anakiri ukweli wa tamko hilo akisema vijana wadogo wa kike na kiume wa Kishapu, hata walio masomoni hutumia muda mwingi kujishughulisha na uchimbaji madini, katika machimbo rasmi na yasiyo rasmi.

“Mtoto akiamka asubuhi, anawaza kuchukua karai na kwenda kuchekecha, ili apate fedha. Suala la elimu kwa ujumla katika mkoa huu kwa baadhi yao halina kipaumbele, ila uchimbaji madini,” anaeleza Almasi.

Kabula anaongeza kuwa mila na desturi zilizotawala jamii ya sehemu hiyo, ni kwamba jukumu la mtoto wa kike ni kusaidia kazi za nyumbani, ikiwamo kuchota maji, kilimo na ufugaji.

MTAZAMO WA POLISI NA SERIKALI
Pili Misungwi, ni Mkuu wa Kitengo cha Dawati la Jinsia katika Kituo Kikuu cha Polisi Shinyanga. Anasema wamekuwa wakipokea kesi nyingi za wanafuzi kupwa ujauzito.

Mlinzi huyo wa Jinsia kupitia Polisi, anasema changamoto iliyo mbele yao, ni namna ya kukamilisha taratibu zinazotakiwa kufungua kesi, kwani mahitaji huwa hayajitoshelezi.

“Kesi nyingi huwa hazina ushahidi, kutokana na baadhi ya familia kuingiwa na tama, wanakubaliana na kuelewana namna ya kulituliza suala lao.

“Utakuta binti anafundishwa kukataa kumtaja mhusika aliyempa mimba, ila kwa chache ambazo zinakamilika upelelezi, zinapelekwa kwa Mwendesha Mashtaka na kufikishwa mahakamani,” anasema Pili.

OFISA ELIMU MKOA
Ofisa Elimu wa Mkoa wa Shinyanga, James Malima, naye anakiri kuwapo tatizo kubwa la mimba za wanafunzi waliopo masomoni.

Anasema tatizo linachangiwa na mambo mengi, ikiwamo umbali mrefu kati ya shuleni na wanakoishi n wakiwa njiani wanakumbana na vishawishi wanavyodhani vitawakwamua kutoka mazingira hayo magumu.

Malima anataja changamoto nyingine, ni ukosefu wa mabweni ya wasichana kwa baadhi ya shule za sekondari.

Anaongeza jingine ni kuwapo changamoto ya wazazi na walezi wanaokataa kuwapeleka watoto wao kukaa katika shule za bweni na badala yake, wanawapangishia vyumba katika nyumba jirani na shule.

“Mzazi anaona kuliko kumleta mtoto wake katika baadhi ya shule zilizo na bweni, utakuta anaamua kumpa fedha akapange mtaani. Mfano, ni katika shule ya Bweni ya Sekondari ya Mangu, ina nafasi za kutosha kwa ajili ya wanafunzi hawa, lakini wazazi hawawapeleki,” anasema.

Anasema katika shule hiyo, hadi sasa bweni lake lina nafasi 99 na wanafunzi wanaoishi bwenini ni 78 pekee.

KAMATI YA WIZARA
Takwimu hizo za utitiri wa mimba za utotoni, zimeishitua Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Ufundi, iliyoamua kuunda kamati maalum ya kufuatilia suala hilo.

Waziri Profesa Joyce Ndalichako, anasema wizara yake ilianza kutekeleza kwa kukutanisha wabunge na wataalam mbalimbali, waliojadili janga hilo la elimu nchini na kutoa ripoti ya pamoja.

Anasema kamati hiyo iliangalia namna ya kuwarudisha wanafunzi shuleni au katika mafunzo yasiyo rasmi, lakini unatambulika na mapendekezo husika yameshamfikia mezani kwak.

“Wiki mbili zijazo kuanzia sasa (kuanzia Julai 19 mwaka huu), nitakutana na Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ili tupeane majukumu, yaani katika elimu kwa mwanafunzi sisi Wizara ya elimu na katika makuzi ya mtoto aliyezaliwa analelewaje-Afya; Tutatoa mapendekezo,” anasema Profesa Ndalichako.

“Tunatakiwa tushirikiane sisi wizara mbili, ili mtoto wa kike asipoteze haki yake ya elimu baada ya kupata ujauzito,” anasema.

Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, anatoa onyo kwamba wanaume wanaoendelea kuwapa mimba wasichana walio na umri chini ya miaka 18, wajiandae na hatua za kisheria.

Anasema, kuna Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971, unaotarajiwa kufikishwa bungeni, mwezi huu utakaojenga manzigira bora zaidi ya sheria hiyo.

MTAALAM
Mhadhiri Msaidizi wa Chuo cha Ustawi wa Jamii cha Dar es Salaam, Zainab Rashid, anasema kuna sababu nyingi za mabinti kupata mimba, licha ya wengi wao kutokufahamu mengi katika umri huo chini ya miaka 18, ikiwamo yanayohusu mabadiliko ya mwili wao.

Zainab anatoa mfano wa kijana anapokuwa shuleni huwa hajui mabadiliko ya mwili wake na madhara ya kujihusisha na ngono, hivyo mara nyingi hujikuta tayari wameshabeba ujauzito kutokana na ushawishi unaowaangukia.

“Kimsingi vijana wengi hasa wasichana chini ya miaka 18, huwa hawapangi kuhusu maisha ya kimahusiano au masuala ya ngono.

“Wengi hujikuta wameingia kwenye masuala ya kimapenzi na kufikia kufanya ngono kwa mihemko tu ya kimwili au ushawishi kutoka mtu mwongine na si kwamba anajua hicho anachokifanya na madhara yake,” anafafanua Zainab.

Habari Kubwa