Dhana ‘takwimu' ilivyokamata kelele, vilio vya watumia maji

10Oct 2019
Frank Monyo
Dar es Salaam
Nipashe
Dhana ‘takwimu' ilivyokamata kelele, vilio vya watumia maji
  • Wataalamu: Wadai gharama, ilikotoka hawajui
  • Udhibiti matumizi wengi bado ‘mbumbumbu’
  • Imebeba siri ya ugomvi wakulima vs wafugaji
  • Imekamata utalii, viwanda, miji, madaraja

“MIAKA miwili iliyopita baada ya mume wangu kufariki, maisha yalikuwa magumu sana, maana mzigo wote wa familia ulikuwa juu ya yangu.

Picha ya kutengenezwa mtambo wa maji ruvu chini kulia. kushoto ni ujumbe maalum ukiongozwa na Katibu mkuu wizara ya maji profesa kitila mkumbo walipotembelea mtambo wa kuzalisha maji wa ruvu juu.

“Kilichokuwa kinaniumiza hasa ni bili ya maji. Nilikuwa nalipa Sh. 50,000 hadi Sh. 65,000 kwa mwezi, bado na mahitaji mengine," anasema Flora Mbega, mkazi wa Kimara, jijini Dar es Salaam, mwenye familia ya watu watano.

Flora, mchuuzi katika wa Soko la Mabibo, Dar es Salaam, anaeleza amekuwa akigombana na wasoma mita, hadi kufikisha malalamiko kwa Meneja wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa) Kimara na makao makuu, kuhusu bili kubwa ya maji.

Anasema alijiuliza kulikoni familia ndogo ina matumizi makubwa ya maji, ingawa upande mwingine anakiri hakuwa na uelewa wa takwimu zake.

Baada ya sintofahamu ya muda mrefu, anasimulia ugunduzi wake: "Ilinibidi nifanye uchunguzi baada ya kushauriwa na Dawasa, ndipo nikagundua msichana wangu wa kazi pamoja na watoto walikuwa hawana ‘discipiline’ (nidhamu) na maji.

“Walikuwa wakiosha vyombo bombani, nguo wanafulia hapo hapo na wanaacha bomba linamwaga maji na walikuwa wanagawa maji kwa majirani."

Anaeleza hatua aliyochukua, ni kuwakanya watoto wanaobaki nyumbani dhidi ya tabia inayomhujumu na akanunua tangi la kuhifadhi maji la lita 10,000, akifafanua: “Pia nilipiga marufuku kufulia nguo bombani na nikawajengea sehemu maalum ya kufanya shughuli hizo.” 

“Kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na takwimu za matumizi ya maji katika ngazi ya familia, ili kuweza kulipia gharama za maji kulingana na matumizi yako,” anaeleza.

Sura ya pili ya kilio cha bili, ipo kwa Joseph Shauri, mkazi wa Tabata, Dar es Salaam, anayelalamika kuwapo wasoma mita wasio waaminifu.

“Nilikuwa naishi kwenye nyumba ya kupanga Tabata, tulikuwa wapangaji kama wanane, kila mwezi bili ilikuwa inapanda. Kwa kawaida tulikuwa tunalipa Sh. 15,000 kwa mwezi, lakini ikafika hadi Sh. 49,000 na wakati mwingine inafika hadi Sh. 50,000.

“Baada ya kusumbuana sana, wapangaji tuliamua kufuatilia jambo hili na kugundua kijana aliyekuwa anasoma mita alikuwa anaichezea,” anasema Sauri.

Mkasa mwingine wenye wajihi huo, unamhusu Maneno Salum, mhudumu katika nyumba ya kulala wageni (jina tunalo) iliyopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam, anayeangukia kilio cha uelewa duni wa wateja kuhusu kiwango cha matumizi yao.

Anasema, kuna baadhi ya wateja wanakosa ustaarabu na kutumia vibaya maji wanapokabidhiwa chumba hata kuna wakati anakuta mabomba hayajafungwa, hivyo anapaisha sauti kwa Dawasa kutoa elimu.

“Hapa kwetu tunatumia maji ya bomba (Dawasa) na tuna matangi ya lita 40,000 ambayo tunayajaza. Hizi tangi unazoziona, maji yanakaa wiki moja au mbili kama kukiwa na shida ya maji, si unajua kuna kufua mashuka pia,” anasema.

Mkazi wa Dar es Salaam, akifua nguo na kuosha vyombo bombani, hali inayoelezwa kuchangia  matumizi mabaya ya maji.

Dawasa wafunguka

Mtumishi wa Dawasa, msoma mita za maji ambaye hakutaka kutaja jina lake, anakiri wingi wa malalamiko ya bili za maji, akitaja sababu kuu ni wateja wengi hawajui uhalisia wa matumizi yao.

 "Binafsi ninapoenda kusoma mita za maji au kuwakatia huduma ya maji wadaiwa sugu kwa kushindwa kulipa. Huwa nawapa darasa kidogo, kuwa maji kwa sasa ni mengi hata mgao wa maji umepungua.

“Baadhi ya maeneo sasa kama utakuwa unafurahia tu kutumia maji bila 'care' (uangalifu) utaleta usumbufu tu wakati wa kulipa,”anasema na kuongeza:

“Nawaambia (anawauliza)  wanajua wanatumia maji kiasi gani kwa mwezi, itawasaidia kupunguza gharama?," Anasema.

Meneja Mawasiliano wa Dawasa, Everlasting Lyaro, anaungana kukiri malalamiko ya bili kubwa za maji tofauti na matumizi halisi.

Anasema, Dawasa ina utaratibu wa kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi sahihi ya maji, kwani wengi wanalalamikia bili, pasipo kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.

 “Utakuta wengine matumizi yao yapo kwenye bustani ya mbogamboga, mifugo na wengine utakuta wanauza maji kabisa, bila ya kujua shughuli hizo huleta gharama kubwa," anasema Lyaro, akibainisha utafiti wao uliowapa mwanga kuhusu shida kubwa iliyojificha kwa wasaidizi wa kazi wanaobaki majumbani.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Mhandisi Cyprian Luhemeja, anasema zamani kulikuwapo na matumizi mazuri ya maji, kwa sababu ya changamoto ya upatikanaji majisafi na salama, tofauti na ilivyo sasa.

Anarejea mwaka 2015, upatikanaji maji jijini Dar es Salaam ulikuwa asilimia 68 na kuwapo maunganisho 123,000. Anaendelea kufafanua:

 “Dawasco kipindi hicho kabla ya kuunganishwa na Dawasa, ilikuwa inakusanya kiasi cha Sh. bilioni 3.2 kwa mwezi. Leo tunapoongea hali ya upatikanaji maji jijini imepanda hadi asilimia 85 na maunganisho ya maji yameongezeka kutoka 123,000 hadi kufika 326, 000."

Mwenyekiti wa Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu, Hamza Sadick (wa kwanza kulia), alipotembelea mtambo wa maji wa Ruvu Chini.

Bonde Wami/Ruvu

Mwenyekiti wa Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu, Hamza Sadick, anasema takwimu za rasilimali maji za muda mrefu ni muhimu kumwondolea umaskini mwananchi, sambamba na kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2030.

Sadick anasema, mamlaka za maji kote nchini, haziwezi kufanya shughuli zake bila ya takwimu zinazoipa dira na mwongozo wa ugawaji maji na utekelezaji miradi yake.

“Kama mamlaka za maji zinatumia takwimu za rasilimali za maji katika kugawa maji kwa watumiaji, kwanini watumiaji wasiwe na takwimu za maji wanayotumia majumbani au kwenye maeneo mengine?” Anahoji.

“Hii itasaidia pia katika utunzaji wa vyanzo vya maji kwani ukijua kutumia maji kwa uangalifu vyanzo vya maji vitabaki salama,” anafafanua.

Anasema takwimu hizo zinasaidia kupunguza umaskini, kuinua kipato, kukuza uchumi na kuipa serikali dira ya utekelezaji miradi kama kilimo, mifugo, utalii, usafirishaji na ujenzi wa madaraja, ikisaidia kutathmini kipindi na kiwango mito inafurika maji na madhara yake

Anasema, nchini kuna vituo vya kukusanya takwimu za uhai wa mito na maji, kazi inayofanyika mara mbili kwa siku; asubuhi saa tatu na alasiri saa tisa alasiri, kwa njia ya kisasa na kizamani, wakitumia vifaa maalum vilivyoweka mtoni.

“Katika upanuzi wa barabara kutoka Kimara (Dar es Salaam) kwenda Kibaha… ukipita pembeni mwa barabara kuna madaraja. Ili ujue, unatakiwa kujenga daraja lenye ukubwa kiasi gani, lazima ujue wingi wa maji yanayopita kwenye daraja hilo kipindi cha kiangazi au masika.

“Ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme la Mto Rufiji, takwimu zake zimeanza kuchukuliwa miaka 60 iliyopita na ndio maana serikali imeamua kuweka fedha nyingi ikiwa na uhakika wa maji ya kutosha kuzalisha umeme.

Anaongeza kwamba, katika maamuzi ya kuhamishia mji mkuu Dodoma, yalifanyika baada ya kupata takwimu zinazojitosheleza kuhusu maji ardhini, hatua inayotumika katika miradi kama kilimo na ufugaji.

Uanzishaji viwanda 

Sadick anasema, mtu hawezi kuanzisha kiwanda pasipo kufahamu kiasi cha upatikanaji maji na matumizi yake, kwani hakuna kiwanda duniani kisichotegemea maji katika shughuli zake za uzalishaji.

Anasema, kwa maana hiyo serikali, wadau wa maendeleo pamoja na wawekezaji hawana budi kutumia takwimu za rasilimali za maji endelevu katika kutekeleza azma ya serikali ya kuwa Tanzania ya viwanda.

“Hivi vitu lazima viende sambamba, serikali kwa sasa imetenga mkoa wa Pwani, kuwa ni eneo la viwanda hivyo ni wazi viwanda vingi vitajengwa kule na lazima vitumie maji. Swali ni je, maji tunayo ya kutosha kwa mahitaji ya viwanda?” Anahoji.

Ofisa wa Maji Bonde la Wami- Ruvu, Simon Ngonyani, anasema wadau wa maendeleo na serikali wanapaswa kuunga mkono utunzaji maji.

Anataja changamoto kubwa kwa bodi yao ni ongezeko la viwanda katika ukanda wa bonde, hivyo inaazaa haja ya kuwapo jitihada kuhakikisha vyanzo vinalindwa kutunza maji, akitaja hofu ya hatari ya maji kuwa kidogo baadaye, sababu ni kuongezeka watumiaji.

“Tujiulize maswali haya; maji yapo wapi? Swali la pili; je, kwa haya maji yaliopo ni endelevu…yataendelea kuwapo na kutosheleza mahitaji?” Anahoji na kuendelea:

“Swali la tatu; je, maji yaliyopo yana ubora? Tukipata majibu ya haya maswali tutaona tunatakiwa kuchukua jitihada za makusudi katika kuongeza nguvu katika utunzaji wa vyanzo vya maji.”

Mfanyakazi wa Dawasa, akihakiki mita ya mteja wakati wa kuwatambua, kuwasikiliza na kutatua kero zao, jijini Dar es Salaam.

Mvua na mto

Sadick, ambaye ni mtaalamu wa rasilimali maji (Hydrogeologist), anasema nchini nyingi ukanda wa tropiki zinategemea mvua kujaza mito na visima na anafafanua: “lakini maji yaende chini ya ardhi, ili visima viwe na maji ya kutosha na chemchemu zitoe maji.” 

Kwa mujibu wa Sadick, takwimu za mvua zinaonyesha jua kali linaweza kukausha maji ya ardhini, hivyo ni lazima kuwapo takwimu za mahitaji kama uvukizo (evaporation), mgandamizo wa hewa, (humidity), kasi ya upepo na ukali wa jua.

Pia anakumbusha asili yake kwamba, maji ni mazingira, wingi na ubora wake unasaidia kuamua matumizi, hivyo anarejea umuhimu wa takwimu ili kuamua mahitaji ya binadamu, kilimo, viwanda na viumbe hai.

Anasema mito yote nchini hufanyiwa tathmini ya kunusuru, kwa kuchukua vipimo vinavyotoa majibu ya uhai wa mto husika, tathmini mojawapo ni viumbe vilivyomo.

“Kuna baadhi ya mito unaweza kupima uhai wake na kukuta baadhi ya viumbe hai havipo hapo utagundua kuwa oksijeni kwenye maji ni ndogo, kwa mfano aina fulani ya samaki hawapo au mimea fulani haipo,” anasema.

 “Wenzetu wa hali ya hewa (TMA) kazi yao ni kutabiri, lakini sisi kwenye maji kazi yetu ni kufanya hesabu mito yetu itachukua maji ya kiasi gani kwa mvua itakayoonyesha, kwani tunafahamu uwezo wa udongo jinsi ya maji yanavyofyonzwa,” anasema.

Maji ardhini

“Tunachimba visima sehemu nyingi, lakini tunajua tuna maji kiasi gani chini ya ardhi” anasema na kuongeza: “Lazima tujue tuna maji kiasi gani chini ya ardhi pamoja na aina ya miamba kwa maana hiyo kuna visima vya uchunguzi vipo sehemu mbalimbali.”

Anatoa mfano takwimu zilizokusanywa zaidi ya miaka 40 katika eneo la Mzakwe, Makutupora ambako ni chanzo cha maji kwa jijini Dodoma, zimesaidia serikali kuhamia mkoani humo, licha ya kuwapo ukame.

Sadick anasema, tathmini ya serikali iligundua miaka ijayo maji yaliyoko hayatakidhi matumizi na ikabuni chanzo kingine katika Mto Bubu, eneo la Falkwa Usandawe, kujenga bwawa litakalokinga Mto Bubu, kusambaza maji Dodoma.

Mfugaji wa wilayani Kilosa, akipitisha ng’ombe wake mtoni, baada ya kuwanywesha maji.Picha ndogo ni mfugaji, Matayo Dakelo, kutoka Kilosa.

Wakulima & Wafugaji

Mtaalamu Sadick anasema, takwimu za maji zinasaidia kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji na anatoa mfano kilichotokea mkoani Morogoro, mzizi mkuu ni maji.

“Wafugaji wengi kutoka Mwanza na Arusha wanakimbilia Morogoro na mifugo yao kwa ajili ya kufuata hali ya hewa nzuri kwa mifugo na malisho,” anasema.

Mfugaji kutoka jamii ya Kimasai eneo la Ngerengere mkoani Morogoro, Matayo Dakelo, anasema wakati wa kiangazi wanategemea maji ya mito, mabwawa na visima kunywesha mifugo yao, anakokueleza hayana magonjwa.

Anasema suala la wafugaji kupata taarifa za maji na mvua kwa mwaka au mwezi, ni changamoto katika maeneo yao, kwani wengi hawana elimu hiyo.

 “Maji ambayo yanatembea hayana maradhi, ndio maana tunapenda kunywesha mifugo katika mito, lakini kama serikali imetukataza, basi itusaidie kujenga mabwawa kwa ajili ya kunywesha mifugo yetu na kama wakiweka gharama ndogo tutalipia, ikiwa kubwa hatutaiweza,” anasema Dakelo.

TMA je? 

Septemba 4 mwaka huu, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitoa ripoti ya utabiri wa mwelekeo wa mvua za vuli, kuanzia mwezi Oktoba hadi Desemba, 2019.

TMA inaeleza athari zitakazoweza kutokea kwa sababu ya mvua nyingi inajumuisha magonjwa ya mlipuko na uhaba wa majisafi na salama.

Mkurugenzi wa TMA, Dk. Agnes Kijazi, anasema katika kipindi hicho kunakuwapo upungufu wa malisho, mvua zinakuwa za wastani au kidogo na kusababisha migogoro ya wakulima na wafugaji.

Sadick anasisitiza wakulima na wafugaji kupata takwimu sahihi na za muda mrefu, kuondoa migogoro hiyo.

DC Kilosa

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Adam Mgoyi, analaumu wananchi wake hawazingatii sheria za maji, kwani wengi wanachepusha na kusababisha maafa kupitia mafuriko wakati wa mvua.

“Sisi Kilosa, udongo wetu ni laini, kwa hiyo wananchi wanavyochepusha maji bila utaratibu wa kujali mamlaka zinazosimamia wanasababisha athari.

Katika maoni yake, Salehe Selemani, mkazi wa Kitongoji cha Behewa wilayani Kilosa, ana sababu zingine, akisema katika kata yao kuna miradi mingi ambayo wajenzi wanatumia mchanga kutoka mto Mkondoa kwa njia ya isiyo sahihi na kusabaisha mto kuhamisha mkondo wake.

“Sasa ni mwezi wa 10 tunaenda mwezi wa 12, tunaanza kupokea maji (mafuriko) kutoka kwa wenzetu Bara (mikoa jirani).  Sasa kwa hali hii tusipochukua tahadhari mapema itatuletea shida katika maeneo yetu,” anasema.

Waziri wa maji Profesa Makame Mbarawa akisaidiana na mafundi kulaza bomba la maji katika mradi wa maji Arusha. 

Waziri Mbarawa 

Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa, katika hotuba iliyopita ya bajeti bungeni, anasema Azimio la Mwaka 2010 la Umoja wa Mataifa (UN), linatamka maji na usafi wa mazingira, ni haki ya msingi ya binadamu.

Pia anasema malengo yake endelevu ya UN ya mwaka 2015 hadi 2030, yanasisitiza upatikanaji majisafi na salama na usafi wa mazingira kwa wote.

Waziri anasema, Taarifa ya Maendeleo ya Maji Duniani ya Umoja wa Mataifa, inaonyesha zaidi ya watu bilioni mbili duniani wanaishi kwenye uhaba mkubwa wa maji, huku watu na shughuli za kiuchumi, ukame na mafuriko vyote vyaogezeka, kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Anasema, zaidi ya watu bilioni 2.1 duniani hawapati majisafi na salama na kati yao, watu milioni 844 hawapati maji safi ya kunywa.

Programu ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji ya Umoja wa Afrika ya mwaka 2016, inahusu zaidi ya watu milioni 340 wanakosa huduma ya maji ya kunywa na wengine zaidi ya milioni 547 waliko katika mazigira machafu, hivyo kuna hitaji la maboresho.

Profesa Mbarawa anasema, maji nchini yanategemea mvua za vipindi viwili, masika na vuli na katika maeneo mengi yanapata wastani wa milimita 900 hadi 2000 kwa mwaka, wakati maeneo makame nchini yana milimita 400 hadi 550.

Anataja kwenye mvua nyingi, Nyanda za Juu Kusini na Milima ya Usambara, kuna wastani wa milimita 2,200 hadi 2,500 kwa mwaka.

Waziri anakadiria matumizi ya maji kwa mwaka ni mita za ujazo bilioni 126, yakigawanyika maji juu ya ardhi mita za ujazo bilioni 105 na chini ya ardhi, mita za ujazo bilioni 21.

“Hifadhi hiyo ya maji inaonyesha kiwango cha maji kilichopo kwa kila mtu kwa mwaka ni takribani wastani wa mita za ujazo 2,300, ukilinganisha na   wastani wa mita za ujazo 1,700 ambacho ni kiwango cha chini cha mahitaji ya maji kwa mtu kwa mwaka kinachokubalika kimataifa,” anasema.

Anarejea historia, kiasi cha maji kwa mtu kila mwaka kinaendelea kupungua kutoka mita za ujazo 7,862  mwaka 1962 nchi ilipokuwa na watu milioni 10.6 hadi kufikia mita za ujazo 2,300 mwaka 2018, nchi ikiwa na watu  milioni 54.

Waziri anasema, maji yanayohitajika majumbani kumwagilia, viwandani na mazingira, ni mita za ujazo bilioni 40 kwa mwaka, kati ya mita za ujazo bilioni 126 zilizopo kwa mwaka.

Vilevile, makadirio yanaonyesha maji yataongezeka kufikia wastani mita za ujazo bilioni 57 kwa mwaka ifikapo mwaka 2035.

Pofesa Mkumbo

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo, anasema kuanzia mwaka 2032, Dar es Salaam itahitaji maji lita bilioni moja kwa siku.

“Tunataka kuongeza uwezo wa Mto Ruvu, ndio maana tunataka kujenga bwawa linaloitwa Kidunda, liwe linasaidia kuongeza kasi katika Mto Ruvu, wakati wa kiangazi linafunguliwa maji yanaingia Mto Ruvu. Hiyo ndio mipango kwa Jiji la Dar es Salaam,” anasema Profesa Mkumbo.

 “Lakini mwaka 2030 hadi 2035, lazima serikali tufikirie kutumia maji ya bahari ila ukitumia maji ya bahari kwa sasa hivi lazima gharama ya maji ipande Dar es Salaam kutoka Sh. 1, 600 kwa lita hadi Sh. 12, 000,” anasema.

 Anasema, ili kulinda vyanzo mabondeni, serikali  ilitunga sheria ya ada ya kutumia maji kwa wenye viwanda maeneo ya bondeni, ingawa haikutekelezwa kutokana na changamoto mbalimbali. 

Profesa Mkumbo anasema, baada ya mazungumzo inatarajiwa viwanda vilivyopo kama ukanda wa Ziwa Victoria na vya Dar es Salaam vitalipia Bonde la Wami/Ruvu.

Mwakilishi wa wamiliki viwanda, Hussein Suphian, anaunga mkono malipo, kwani kwa viwanda vyote duniani, maji ni rasilimali muhimu katika uzalishaji.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Mhandisi Cyprian Luhemeja akisaidiana na mafundi kuchimba mtalo kwa ajili ya kulaza bomba la maji katika mradi wa maji Kisarawe. PICHA ZOTE: FRANK MONYO

Ubora wa Maji

Waziri Mbarawa, anasema serikali itahakiki ufuatiliaji wa ubora wa maji yanayosambazwa katika Halmashauri, Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira, taasisi na vyanzo vya maji vinavyomilikiwa na watu binafsi.

Jumatatu wiki hii akiwa mkoani Rukwa, Rais John Magufuli, alichukua hatua kali za kinidhamu na kisheria, dhidi ya hujuma zinazofanyika katika vyanzo vya maji mkoani humo, akimwagiza Profesa Mbarawa kubaki baada ya ziara kufuatilia utekelezaji.

Anasema, takwimu za maji hadi Aprili mwaka huu, kuna sampuli 4,165 zilizokusanywa na kufanyiwa uchunguzi na matokeo asilimia 91 zilikidhi viwango  na zilizobaki zilikuwa na vimelea vya wadudu na madini.

Victoria/ Tanganyika

Hivi sasa serikali inatekeleza mradi wa maji katika Ziwa Tanganyika utakaohudumia wakazi wa maeneo pembezoni mwa ziwa na hadi mwezi Aprili, Waziri anaeleza mtaalamu mshauri ameshawasilisha taarifa ya upembuzi yakinifu kuhusu athari za kimazingira na kijamii.

Ni mradi unaotekelezwa katika mikoa ya Kigoma, Rukwa na Katavi na utahusisha vijiji 73 vya wilaya za Kigoma, Uvinza, Nkasi, Kalambo, Mpimbwe na Mpanda.

Pia anasema serikali imepanga mradi wa maji Ziwa Victoria, utakaohudumia wakazi wa pembezoni mwa ziwa na mtaalamu mshauri anaendelea na sanifu katika vijiji vitakavyonufaika.

 “Usanifu utakapokamilika, ujenzi wa mradi utaanza na utanufaisha jumla ya vijiji 301 vilivyopo pembezoni mwa Ziwa Victoria katika Mikoa ya Mwanza, Kagera, Geita, Mara na Simiyu,” anasema.

Jijini  Dodoma

Profesa Mbarawa anasema, serikali inatekeleza mradi wa maji katika mji mpya wa serikali eneo la Ihumwa, ambao umegawanyika katika awamu mbili.

Awamu ya kwanza, inagharimu Sh. bilioni 3.6 iliyohusisha kupima maji ardhini; ujenzi wa tangi la kukusanya maji ujazo wa lita 200,000; tangi la lita milioni moja; na kuchimba visima saba.

Mengine anataja ni ulazaji bomba kuu la kilomita 4.5 kutoka maji yanapokusanywa hadi kunakohifadhiwa; kununua pampu na kujenga pa kuhifadhi mitambo; kufunga transfoma na kupeleka umeme visimani.

Anasema, mkakati wa muda mrefu wa kupata maji ya uhakika Dodoma mjini, unahusu ujenzi wa bwawa la Farkwa, wilayani Chemba, litakalokuwa chanzo kikuu ikitarajiwa kuongeza maji kwa ujazo lita milioni 120 kwa siku, kwa ajili ya wakazi zaidi ya milioni moja.

RC Pwani

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo, anasema wakati Dar es Salaam inategemea maji ya Ruvu Juu na Chini, Dawasa ipo kwenye mchakato wa kutumia maji ya Rufiji kama chanzo chake kingine.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Mhandisi Luhemeja, anathibitisha kwamba kamati imeshaundwa kushughulikia hilo akifafanua: “Tumetumia fursa ya bwawa la Rufiji linalojengwa na sisi tutajenga mtambo mkubwa wa maji kutoka Rufiji… Tumeshawasiliana na wadau wetu Tanesco ambao ndio wenye bwawa.”

Pia anasema wameshafanya mawasiliano na mkandarasi rasilimali wa bwawa na wakala wa barabara Tanzania (Tanroads) kuhusu ujenzi wa mtambo wa maji.

 “Mwakani tutawasilisha hoja Bodi ya Dawasa kwa ajili ya kupata kibali, kisha upembuzi yakinifu ufanyike na kazi ianze, mtambo utajengwa kwa gharama ya takribani Sh. bilioni 200 ambazo ni fedha za ndani. Mradi utaanza Julai mwakani na utatumia miaka mitatu kukamilika,” anasema.

 

Mwandishi anapatikana kwa simu: (+255) 0658 141286; barua pepe: [email protected]

Habari Kubwa