Dk. Bashiru anapowachoka wenye uchu mali za chama

03Jul 2019
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
Dk. Bashiru anapowachoka wenye uchu mali za chama
  • *Aagiza washughulikiwe kuepusha migogoro
  • *Akemea tabia ya kulindana na kukingiana kifua

MWISHONI mwa wiki iliyopita, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, alikutana na wanachama wa chama hicho wa Wilaya ya Ubungo Dar es Salaam na kufanya nao mkutano.

Dk. Bashiru.

Katika mkutano huo, Dk. Bashiru alibainisha kuwa ana taarifa kwamba kuna migogoro ya viongozi wa chama hicho wanaogombea mali za chama na kuagiza tatizo hilo lishughulikiwe.

Dk. Bashiru katika maelekezo yake, anataka wanachama wa aina hiyo wasivumiliwe bali watimuliwe, kwa kuzingatia kwamba chama hicho hakina uhaba wa wanachama.

“Kila mwanachama ana haki ya kuongoza, hivyo hizo tabia za kulindana na kukingiana kifua zimesababisha chama kufikia hapa kilipo... mali za chama zinatakiwa kulindwa na kutunzwa,” anasema Dk. Bashiru.

Anabainisha kwamba mtindo wa baadhi ya viongozi kugombea mali za chama na wakati mwingine kuzikwapua haukubaliki na unasababisha watu wenye nia njema ya kujitolea kusaidia chama kukata tamaa.

MAKONDOKANDO

Kwa maelezo hayo ya Dk. Bashiru ni kwamba licha ya juhudi zote za kuimarisha chama zinazofanywa na viongozi wa juu, bado kuna wanachama wachache wanaoifanya CCM iwe na makandokando.

Katika juhudi za kupambana na makondokando ndani ya chama, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Magufuli aliunda tume ya kuhakiki mali za chama, iliyoongozwa na Dk. Bashiru Ally.

Tume hiyo ya watu tisa iliundwa mwishoni mwa mwaka 2017 ikiwa na jukumu la kufuatilia na kuhakiki mali za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kote nchini baada ya kubainika kuwa zinanufaisha wajanja wachache.

Mwenyekiti huyo aliunda tume hiyo ikiwa ni utekelezaji wa dhamira ya kupiga vita rushwa na ufisadi, kwa vile anaamini kwamba hawezi akaanza kupiga vita rushwa na ufisadi ndani ya serikali wakati chama kina rushwa na ufisadi.

Anasafisha chama ili kiachane na mambo ya rushwa na ufisadi na hivyo Tanzania isonge mbele.

Kwa hiyo hao wanaodaiwa kugombea mali za chama, ina maana kwamba hawajajua nia ya viongozi wao wa juu ya kumaliza makondokando.

Kama kweli viongozi wa aina hiyo wapo ndani ya chama na wanaendelea kulindana, wanakiharibia chama ambacho kimeamua kujiweka kando na kila aina ya mambo ambayo yanakwenda kinyume na utaratibu.

MIRADI YA CCM

Dk. Bashiru anatolea mfano mkoa wa Dar es Salaam kuwa CCM ina miradi, ambayo inaweza kujiingizia Sh. bilioni tano kwa mwaka na kuifanya ijiendeshe yenyewe kwa ufanisi.

Hata hivyo, katibu huyo anasema anaumizwa na baadhi ya watu wasiotaka utaratibu wa malipo uliopo anaoutaja kwa jina la 'control number.’

“Hapa ninamaanisha kwamba wapo baadhi ya viongozi, ambao hawafuati mfumo uliowekwa wa kutumia control number. Yaani hawalipi kwa kutumia mfumo huo, matokeo yake fedha zinatumika kiholela,” anasema.

Anasema chama kitaendelea kukemea vitendo vichafu vikiwamo hivyo, ambavyo vinasababisha wananchi wakione kama hakiko imara, kumbe ni kwasababu ya watu wachache wanaopaswa kushughulikiwa.

“CCM imejiimarisha na inaendelea kujiimarisha zaidi, hivyo haiwezi kuwavumilia watu wenye nia ya kuifanya isiaminike mbele ya umma wa Watanzania,” anasema.

Dk. Bashiru anasema chama hicho kinapambana kwa dhati na kila aina ya vitendo viovu vikiwamo vya rushwa, ambavyo CCM Mpya na Tanzania Mpya haitaki kuvikumbatia.

CCM MPYA, TANZANIA MPYA

Katibu wa Itikadi na Uenezi Taifa, Humphrey Poleple, anasema viongozi wa CCM wameshaeleza fikra na mipango yao na tayari wameanza kusimamia na kutekeleza ajenda ya mageuzi ndani ya chama, ambayo msingi wake ni kuirejesha CCM kwa watu

“Msimamo wa kufanya mageuzi kwenye CCM ni kukirudisha kwenye misingi, ambayo chama kilianzishwa, kwa maana ya chama cha wanyonge wakiwamo wakulima na wafanyakazi,” anasema Polepole.

Hapa anamaanisha kwamba kinachoendelea sasa ni kufanya kazi kwa bidii kwa kutumikia wananchi, kwa vile Watanzania bado wana matumaini kwa chama hicho tawala.

Anasema kinachotakiwa ni wanachama kuendelea kuheshimu maelekezo ya viongozi na kutimiza wajibu wao inavyotakiwa ili chama kizidi kukubalika mbele ya umma wa Watanzania.

“Chama Cha Mapinduzi kinachapa kazi na kinaendelea kuchapa kazi, na dhamira ya kujenga Tanzania Mpya inaakisiwa na kuleta CCM Mpya, ambayo ni kimbilio la Watanzania wengi,” anasema.

USHIRIKIANO VITANI

Binafsi naamini kwamba kila mwana CCM anapaswa kushiriki katika kufanikisha dhana ya CCM Mpya na Tanzania Mpya badala ya kudhani kwamba vita ya kupinga uovu ndani ya chama ni ya viongozi wa juu.

Kwa ushirkiano wa wanachama wote kuna uwezekano mkubwa wa kukomesha vitendo vya rushwa ambavyo vimekuwa vikipigiwa kelele kwa muda mrefu na viongozi wa chama.

Mwenyekiti wa CCM anaamini kwamba kwa Mtanzania mwaminifu kwa imani yake hatakuwa na kigugumizi cha kuwa mstari wa mbele kupambana na rushwa na ufisadi.

Hii ingekuwa ni imani ya kila mwanachama wa CCM na hata Watanzania kwa ujumla wao ili waweze kutoa mchango katika kupambana na vitendo hivyo vinavyowanyima haki wanyonge.

Vitendo hivyo vikikomeshwa hakutakuwa na kulindana wala kukingiana kifua na kusababisha chama kionekane hakifai, kumbe ni watu wachache walioamua kuziba masikio ili wasisikie maonyo.

Kwa hali hiyo sasa ni vyema wale ambao bado hawajatambua kuwa wako ndani ya CCM Mpya, wabadilike na kuchukua hatua za kubadilika haraka wasije kujikuta wanaingia kwenye anga za Dk. Bashiru.

Habari Kubwa