DK. KAPOLOGWE: Kila kituo cha afya nchini sasa kufanya upasuaji

07Dec 2017
Augusta Njoji
Nipashe
DK. KAPOLOGWE: Kila kituo cha afya nchini sasa kufanya upasuaji
  • Serikali ‘kumwagia’ kila kimoja mil.500/-

“KUHAKIKISHA Afya Njema na Ustawi wa Watu wa Rika zote.” Hilo ni lengo la tatu kati ya 17 ya Maendeleo Endelevu ya Dunia, linalohusu kuwezesha watu kuishi kwa afya bora, hivyo kuongeza umri wao kwa watu wa rika zote ifikapo 2030.

Vifaa vya kisasa vinavyohitajika katika mageuzi hospitalini. Picha na Augusta Njoji

Ni lengo ambalo nchini linaigusa serikali ya mitaa kuhakikisha zinapunguza vifo vya kinamama na wajawazito chini ya 398 vilivyo kati ya 100,000.

 

Pia, katika hilo linagusa kupunguza vifo vya watoto wanaozaliwa na walio chini ya umri wa miaka mitano.

 

Zipo takwimu zinazotaja vifo 51 kwa kila wazazi hai 1000 kwa watoto wa kiume, pia vifo 41 kwa vizazi hai 1000 vya wasichana.

 

Ili kufanikisha lengo hilo, ndio linapozaa wajibu wa serikali kuweka mikakati mbalimbali na taarifa sahihi za elimu na stadi za huduma ya afya ya uzazi kwa wananchi, kwa ajili ya utekelezaji.

 

Inaelezwa kuwa, mtu anapokwa na afya njema, ana nafasi kubwa ya kuzalisha mali na hata kuongeza kipato binafsi na familia yake kwa ujumla.

 

Mkurugenzi wa Afya katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), Dk. Ntuli Kapologwe, anasema katika idara hiyo kuna vitengo vikuu vitatu ambavyo ni vinavyohusika na: Lishe, Ustawi wa Jamii na Afya.

 

Dk.Kapologwe anasema lengo lililopo ni kujiwekea mikakati mbalimbali, ili kuimarisha sekta ya afya kwa kujenga miundombinu muhimu na kupunguza changamoto za utoaji huduma kwa wananchi.

 

Vipaumbele vya maboresho

 

Mkurugenzi huyo anasema, Tamisemi ina vipaumbele vyake anavyovitaja kuwa ni Uboreshaji miundombinu kwa kuwa Tanzania ni kubwa sana na bado inahitaji miundombinu kwa sehemu kubwa.

 

Dk. Kapologwe anatoa mfano wa sasa nchini, ikiwa na jumla ya kata 4,420, lakini vituo vya afya vilivyopo ni 512 pekee, ambavyo ni sawa na asilimia 11.6.

 

Kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Afya (MMAM) inayokaribia kuwa na miaka 1p ya kutumika, kila kata inatakiwa kuwa na kituo cha afya na kila kijiji kiwe na zahanati, huku jumla ya vijiji hivyo nchini ni 12, 545.

 

Dk. Kapologwe anafafanua kuwapo jumla ya zahanati 6,640 ambazo ni sawa na asilimia 53 ya mahitaji nchi nzima na katika orodha hiyo, zinazomilikiwa na serikali jumla yake ni 4534.

 

Vivyo hivyo, sera hiyo ya afya inaelekeza ngazi ya wilaya kuwa na hospitali, zikiongozwa juu yake na hospitali za mkoa ambazo ni mahsusi kwa rufaa.

 

Aidha, ngazi zingine za kanda kuna hospitali za rufaa na juu yake kuna hospitali ya taifa, ambayo ni Muhimbili.

 

Huku akifafanua kuhusu MMAM ilivyoanzishwa mwaka 2007 (na kuanza kutekekezwa rasmi 2008), Dk. Kapologwe anaeleza maboresho yaliyopo sasa kwa huduma ya mama na mtoto ilivyo, alisema:

 

“Kwa sasa serikali imeandaa andiko na kuridhiwa na wafadhili lenye lengo la kuboresha miundombinu ya vituo vya afya, ili viweze kutoa huduma ya dharura ya upasuaji wa kinamama wajawazito.”

 

Miradi iliyobuniwa

 

Dk.Kapologwe anasema kwa sasa serikali imebuni miradi mbalimbali inayosimamiwa na serikali ya Tanzania, kwa kushirikiana na Mfuko wa Dunia( Global Fund)m, unaoshughulikia mapambano dhidi ya maradhi ya Kifua Kikuu, Ukoma , Malaria na Ukimwi.

 

Mganga Mkuu huyo wa Afya serikalini, anasema Tamisemi kwa sasa inasimamia mradi mkubwa wa Malipo kwa Ufanisi, unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.

 

Dk. Kapologwe anasema mradi huo unatekelezwa katika mikoa minane katika Kanda za Ziwa, Mashariki na Magharibi na Pwani.

 

Anasema lengo la mradi huo wa kujenga, kuwezesha malipo kwa ufanisi na kuboresha miundombinu ya utoaji huduma kwa kufanya ukarabati pamoja na ununuzi wa vifaa tiba, vinavyotumika katika vituo vya afya.

Sambamba na hilo, Dk, Kapologwe anasema katika mradi huo, asilimia 25 ya fedha zake zinatumika kuwapa watumishi motisha mbalimbali, zitokanazo na kazi mbalimbali wanazozifanya.

 

Anafafanua kuwapo Mfuko wa Pamoja wa kukusanya pesa, maarufu kama ‘Basket Fund’ unaodhaminiwa na Shirika la Maendeleo la Denmark (Danida), Benki ya Dunia, serikali za Canada, Uswisi, pamoja na Ireland.

 

Lengo katika hilo ni kuwezesha fedha zinazopatikana zitolewe kwenye vituo vyote vya afya na zahanati, ili kuhuduma afya bora kwa jamii.

 

“Serikali inasaidiwa fedha mbalimbali za wafadhili ambao ni UNFPA,Unicef,ILO husaidia idara ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi,” anasema

 

 

Miundombinu

 

Dk.Kapologwe anasema, serikali imeshapata fedha za kuboresha miundombinu ya vituo 173 vya afya, ikiwamo kuhakikisha huduma ya upasuaji zinakuwepo katika vioto hivyo vya afya.

 

Anasema, ni hatua inayohakikisha kupunguza vifo vya kinamama wajawazito na watoto vitokanavyo na uzazi.

 

Daktari huyo aliyeko katika ngazi ya uongozi kusimamia mipango, anasema kuwa mpaka sasa, serikali imeshapeleka wastani wa Sh. bilioni 22 kwa vituo 44, kila kimoja kikitarajiwa kufanya ukarabati wa wastani wa Sh. bilioni 22 na kila kituo kitatumia fedha Sh. milioni 500.

 

Kadhalika, Dk. Kapologwe anasema, kila kituo cha afya kitapatiwa Sh. milioni 220 kwa ajili ya kununua vifaa vinavyohitajika na vifaa tiba.

 

Mkurugenzi huyo anafafanua matumizi ya fedha hizi Sh. milioni 500, kwamba itajengwa mifumo ya maji ya mvua, vichomea taka, ujenzi wa mashimo kwa ajili ya kutupia kondo la nyuma na nyumba ya watumishi, walai kila kituo kuwa na nyumba ya mtumishi.

 

Anasema mradi, pia utajenga nyumba za watumishi 173, ili kuwasaidia watumishi wa vijijini, kupunguza changamoto ya nyumba za kupanga.

 

Dk.Kapologwe anaongeza kuwa, serikali imejipanga kujenga wodi za wazazi na wodi za watoto, pia vyumba vya kuhifadhi maiti katika sehemu zenye mahitaji.

 

 

Anaahidi kuwa serikali itaendelea kuwashirikisha wadau mbalimbali na kwa bajeti ya mwaka uliopo wa fedha; 2017/2018, imetenga Sh. bilioni 69.9 kwa ajili ya kukamilisha majengo katika maeneo mbalimbali nchini.

 

Anayataja majengo hayo kuwa ni zahanati, vituo vya afya na hospitali za mikoa na Dk. Kapologwe anafafanua:

 

“Hivi sasa zipo hospitali nne nchini ujenzi unaendelea, ambazo ni Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe, Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga, Hospitali ya Mkoa wa Geita na Mkoa wa Simiyu.

 

“Hizi zote zikishakamilika, zitasaidia katika utoaji huduma za kirufaa na kuwapunguzia wananchi adha ya kusafiri umbali mrefu kwenda kutafuta huduma za rufaa.”

 

Mkurugenzi huyo anaendelea kuwa zitahitajika Sh. bilioni 191,250 kuhakikisha vituo vyote vya afya vilivyobaki 225 viweze kutoa huduma za upasuaji wa dharura.

 

Hiyo anasemna inaendana na kuboresha majengo ya wodi za kinamama, watoto, vyumba vya maabara na mfumo wa uvunaji maji ya mvua hospitalini

 

Anasema serikali inatarajia kufanya ukarabati mkubwa wa zahanati, kila moja kikihitaji Sh. bilioni 227 na kwa sasa wanawashiliana na wadau kupunguza changamoto zilizopo katika zahanati nchini.

 

Anadokeza kuwa hivi sasa serikali ina jumla ya maboma 1875 nchini na wanaendelea kuzihamasisha Halmashauri mbalimbali na Tawala za Mikoa nchini.

 

 

 

 

Habari Kubwa