Dk. Makongoro Mahanga 1955-2020

25Mar 2020
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
Dk. Makongoro Mahanga 1955-2020
  • .Muasisi wa majimbo Ukonga na Segerea
  • .Alibobea uhasibu na ugavi kwa mpigo
  • .Aliibukia siasa ghafla, akang'ara

JUZI asubuhi, kama ilivyo kawaida ya mitandao ya mawasiliano nchini na kimataifa, ilivyo 'fasta' ni taarifa nyingine ya kifo cha Dk. Milton Makongoro Mahanga, mkazi wa Tabata Segerea, vilevile aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo la Ukonga na hata pale lilipogawanywa, aliwania nafasi hiyo kwa jimbo la...

la nyumbani kwake Segerea.

Hili ni pigo, kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kwani hadi taarifa ya msiba, uliotokea katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), jijini Dar es Salaam, alikuwa mwenyekiti wa chama hicho, Mkoa wa Ilala.

Katibu wake mkoani Ilala, Jerome Olomi, alithibitisha kutokea kwa kifo hicho taarifa za awali wakizipata kutoka kwa mke wake.
Ni wastani wa takriban miongo miwili sasa, kwa maana ya miaka 20 kasoro miezi kadhaa tangu aanze kuonekana na kung'ara katika anga za siasa nchini.

Huenda kutokana na sababu mbalimbali kama vile umri, ufuatiliaji kwa hatua na weledi wa namna mbalimbali vinawafanya watu kumfahamu Dk. Mahanga kuanzia ngazi tofauti za miaka; Kuna wanaomfahamu kuanzia siasa za uchaguzi mwaka 2000, wengine alipobeba jina kubwa la naibu waziri.

Pia wapo walioanza kumfahamu, pale alipokipa kisogo Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga na Chadema, akiwa sehemu ya "timu Lowassa", kupitia yale yaliyojiri katika kumsaka mgombea urais kwa tiketi ya CCM, ambayo undani wake hauna jipya la kuwasimulia wengi leo hii, katika siasa.

ALIKOIBUKIA

Huko nyuma kabla ya mwaka 2000, hakuwahi kusikika, kuwa na jina linalotamba kitaifa kwa kiwango alichoonekana kisiasa, na hata kwa wanamjua, hakutabiriwa hata siku moja kwamba angejitosa kwenye siasa kubwa, eneo lililomeza jina lake hadi umauti.

Kwa kudodosa wasifu wake, huyu ni msomi aliyeshiba kitaaluma 'kisawasawa' hasa katika eneo la menejimenti na kwa 'kumchimba' zaidi, taaluma aliyosimama nayo kwa kina, ni fani ya ugavi, ambayo msingi wake aliupata katika Chuo cha Nyegezi Mwanza, ambacho sasa ni Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT).

Dk. Mahanga, alizama zaidi katika taaluma hiyo na kupata cheti cha juu zaidi ya taaluma, kinachotolewa na Bodi ya Taifa ya Usimamizi wa Vifaa (NBMM), kiitwacho CSP (Certified Supplies and Purchasing Proffesion).

Ikumbukwe katika kipindi hicho, NBMM ikiwa ni taasisi changa, Dk. Mahanga ni miongoni mwa walaaluma wachache wa Kitanzania waliokuwa mhimili wa bodi hiyo.

Baadaye katika kujiendeleza, mwanasiasa huyo aliweka rekodi ya kipekee nchini pale alipoamua kuzama kusomea 'fani ndugu' na ugavi ambayo ni uhasibu, hata akakipata cheti cha juu kabisa cha uhasibu kinachofanana na CSP, hicho ni CPA (Certified Public Accountant), kinachotolewa na Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA).

Umaarufu wake ndipo ukaanza kujidhihirisha katika ngazi ya umma, kwani itakumbukwa, mwazoni mwa miaka ya 1990 alipoajiriwa kuwa Mhasibu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Ilikuwa ni rekodi ya aina yake, msomi mwenye vyeti vya pande mbili kuajiriwa kusimamia fedha za wasomi wenzake, tukio la kuajiriwa kwake kwa wasifu huo hata UDSM, ikatoa taarifa katika vyombo vya habari kujigamba imepata mhasibu mkuu aliyetukuka.

Hata hivyo, hakudumu sana chuoni hapo, baadaye alihama na kuajiriwa kama mkuu wa idara mojawapo ya Shirika la Nyumba Tanzania (NHC), huku kitaaluma akipiga hatua zaidi kwa kusomea Shahada ya Uzamili katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), akiwa ni miongoni mwa wanafunzi wa awali kabisa tangu ngazi hiyo ya elimu kutolewa chuoni hapo.

Kuhusiana na wasifu wake, wa Shahada ya Udaktari wa Falsafa (Phd), kulishatokea mjadala wa kisheria, ambao pia uliwahusu baadhi ya wanasiasa wengine, kati yao wapo waliolazimika kurudi darasani tena kuweka sawa uhalali wake.

AJITOSA SIASA

Mwaka 2000, kukiwapo vuguvugu zinazojitosheleza za siasa, katika jimbo jipya la Ukonga, lililogawanywa kutoka Ilala, mara hii Dk. Mahanga, wakati huo akiwa na umri wa miaka 45, aliamua kuweka kando menejimenti aliyokuwa akiitumikia NHC, akiwania utawala wa kisiasa.

Hapo hasa ndipo jina lake lilipea kitaifa. Kwanini? Kwanza hakuna hata mmoja aliyemfahamu kwamba ni machachari hasa wa kisiasa, kuanzia kampeni za ndani za CCM kumsaka mgombea, hata akawapelekesha mbio wenye majina makubwa waliowania nafasi hiyo, wakongwe waliozaliwa ndani ya siasa hata wakiwa katika umri wa kuzeeka, aliwamudu.

Pale alipopitishwa na CCM kuwa mgombea wake jimboni Ukonga, vibweka vyake vya kampeni vinavyodaiwa viliendana na 'uwekezaji' mkubwa, vilikuwa na mafanikio makubwa.

Mtumishi mwenzake kutoka NHC, Khadija Kusaga, ambaye naye ameshatangulia mbele ya haki, alijitosa jimboni Temeke kwa mafanikio ingawa yake yalikuwa tofauti kidogo, kwa maana ya kuyatolea jasho jingi.

Ulikuwa wakati mgumu katika kampeni za Khadija, hata kuna wakati alilazimika kuja na staili mpya ya kuomba kura kwa kupiga magoti, ikiwa ni ishara ya namna fulani ili wapigakura wamuone kwa jicho la huruma kisiasa.

Jimbo la Ubungo nalo safari hiyo lilimpata mgombea wa CCM, mtendaji mwandamizi wa kiserikali katika halmashauri mbalimbali kitaifa, mara ya mwisho akiwa ni Mwenyekiti wa jiji la Dar es Salaam, Charles Keenja, ambalo wakati huo halmashauri ilikuwa imevunjwa, baada ya kukamilisha wajibu akaibukia katika siasa za ubunge.

Kuna wakati kampeni hizo zikiwa 'zimenoga' kila mmoja akifanya tathmini za ndani; Keenja na Dk. Mahanga, wanaona viashiria vya mambo mazuri, walilazimika mara kadhaa kwenda 'kumsapoti' Khadija kwenye kampeni zake Temeke, mshindani wake mkuu akiwa ni Richard Hizza Tambwe wa Chama cha Wananchi (CUF), naye kwa sasa ni marehemu.

Ubunge wake ulimpatia majibu ya manufaa, hata akakwea kuwa naibu waziri. Ulipofika uchaguzi unaofuata mwaka 2005, Dk. Mahanga alifanikiwa kutetea tena kiti chake, lakini safari hii akipata mchuano mkali kuanzia kura za maoni ndani ya CCM.

Kama kuna kipindi, mwanasiasa huyo alianza kushuhudia ugumu wa siasa za uchaguzi ni mwaka 2010, akiwa katika jimbo jipya la Segerea, kuzipata kura za wakazi wa maeneo anakoishi kwa maana ya Kifuru, Segerea na pande zote za Tabata ilikuwa ngumu kwake.

Kwa kutumia stadi za kisiasa, akishirikiana na wenye weledi kutoka ndani ya chama chake, kwa kiasi kikubwa, aliwekeza katika maeneo ambayo yeye na chama chake walikubalika zaidi, mathalani Buguruni na Vingunguti na kunufaika na idadi kubwa ya wapigakura, alifanikiwa kutetea ubunge wake kwa mara ya tatu.

Zilipofika siasa za uchaguzi ndani ya CCM na sintofahamu katika kumtafuta mgombea urais wa chama hicho, hata kukatokea mgawanyiko, Dk. Milton Makongoro Mahanga, alikuwa miongoni mwa waliomsaidia Edward Lowassa, kuinua jamvi lao wakisonga kuelekea Chadema, kuanza maisha mapya.

Ndani ya zama zote ametumikia nafasi ya naibu waziri, hususan katika Wizara ya Kazi na Ajira.

MSIMAMO WAKE

Mwaka 2015 kulikuwa na wimbi kubwa la wanasiasa na hasa wa CCM wakiwamo vigogo, ambao walihamia Chadema.

Katika uhai wake amewahi kukaririwa na vyombo vya habari akizungumzia hatua ya vigogo wenzake kurudi CCM na kusema, walikosa kilichopeleka upinzani lakini yeye hakuwa na mpango huo.

"Siwezi kurubuniwa, kununuliwa, siwezi kurudi CCM, kwa sababu sijaja Chadema kwa sababu ya cheo, mimi nilikuwa waziri, niliacha uwaziri bado kuna miezi mitatu mbele, mawaziri huwa wanakwenda mpaka Novemba siku wakati rais anaapishwa mimi nilitoka mwezi wa nane kwa hiyo mawaziri wenzangu waliendelea, mwishoni huwa kuna viposho, lakini mimi nikaviacha. Sikuja Chadema kutafuta cheo," alikaririwa enzi ya uhai wake.

Mbali na hilo, hata kwenye uchaguzi ndani ya Chadema uliofanyika Desemba mwaka jana, Dk. Mahanga alitoa neno kuhusu baadhi ya wanachama wa chama hicho waliokosa nafasi na kurudi CCM.

Dk. Mahanga alisema, Chadema imekua na itaendelea kubebwa na viongozi, wanachamana wafuasi mahiri waliokubali kwa dhati itikadi falsafa na dira ya chama hicho bila kuweka mbele maslahi yao binafsi.

"Wao ndiyo wanaojua kama Chadema ni mzigo wa maji kwenye gunia au ni mwamba na jabali unaokwenda kuibomolea mbali CCM mwaka huu. Ati gunia la maji? Ningekuwa bado kijana ningemjibu," alisema.

Hizo ni miongoni mwa kauli zake za mwisho alizotoa mwaka huu akiwazungumzia wanachama waliokosa uongozi ndani ya Chadema na kuamua kurudi CCM huku wakilalamika.

ULIMI WATELEZA

Katika kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo la Ukonga, Dk. Mahanga alikuwa miongoni mwa wapigadebe wa Chadema wakimnadi mgombea wa chama hicho, Asia Msangi, aliyekuwa akichuana na Mwita Waitara.

Jimbo la Ukonga lilikuwa wazi tangu Julai mwaka 2018, baada ya aliyekuwa mbunge wake, Mwita Waitara (Chadema) kuhamia CCM na hivyo kulazimika kufanyika uchaguzi mdogo.

Dk. Mahnga aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa miaka 10 kuanzia mwaka 2000 hadi 2010 akiwa CCM, alikaririwa na vyombo vya habari akitamka ulimi na kudai kwamba aliongoza jimbo hilo 'kwa kununua kura'.

Akawataka wananchi wa Ukonga wasikubali tena kuuza kura zao na badala yake wamchague mgombea kupitia Chadema, lakini kauli hiyo ikapingwa vikali na CCM kwamba anadhalilisha elimu yake.

Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi. Amina.

Habari Kubwa