Dk. Omari Ali Juma: Mwasisi mkakati Tanzania kuufikia uchumi wa kati

28Jul 2021
Gaudensia Mngumi
Dar es Salaam
Nipashe
Dk. Omari Ali Juma: Mwasisi mkakati Tanzania kuufikia uchumi wa kati
  • *Shujaa kuondoa umaskini,

ULIKUWA mwezi Julai mwaka 2001, Watanzania walipotangaziwa kifo cha Makamu wa Rais wa wakati huo, Dk. Omar Ali Juma, haikuwa jambo rahisi kuzikubali taarifa hizo.

Kwa mujibu wa maelezo ya Rais wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa, Makamu wake alifariki saa 5:45 usiku wa Jumatano Julai 4 kutokana na matatizo ya moyo.

Hata sasa Watanzania wanamwomboleza kwa kuziangalia kazi zake nyingi alizofanya kwa miaka mitano ya utumishi, kwa ajili ya maendeleo ya taifa na kwa matumaini wanashuhudia masuala muhimu yanayoonekana kuwa na matumaini na mafanikio makubwa leo, ambayo yeye ndiye aliyeanza usimamizi na utekelezaji wake.

Kazi ya kulinda mazingira na kupunguza umaskini ndicho alichokisimamia hata leo Tanzania inatajwa kuwa nchi ya uchumi wa kati, jukumu hilo lilianza na Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk. Omar.

Alianza kupunguza umaskini kwa mtu mmoja mmoja hadi taifa lakini heshima yake inabakia kwa mafanikio yanayoonekana kwa mamilioni ya Watanzania ambao wanaendelea kulinda na kuhifadhi mazingira yao na kupunguza umaskini.

Licha ya kuwa Makamu wa Rais alikuwa na tatizo la moyo, kifo chake kilikuja ghafla mno, wakati kiongozi huyo siku ya Julai 3, alionekana kwenye vyombo vya habari akimuaga Rais wa DRC, wakati huo Joseph Kabila.

Mkapa ndiye aliyetangaza kifo chake, akimsifu kuwa alikuwa msaidizi wake mahiri, mwenye sifa za kutukuka, akiwa mwaminifu, mwadilifu na mchapakazi hodari, ambaye aliacha pengo kwenye uongozi wa taifa.

Kwa wengine Makamu wa Rais alionekana kuwa pengine angekuwa mrithi wa Rais Benjamin Mkapa, mwaka 2005 kwenye uchaguzi mkuu.

Dokta Omari Ali Juma, hakuwa mtumishi wa Watanzania peke yao bali pia alikuwa mshiriki mkubwa wa kutafuta amani ya Congo na hata siku alipofariki usiku wa Jumatano Julai 4, jijini Dar es Salaam, mchana huo alikuwa naRais Kabila kufanikisha juhudi za kusaka amani ya Congo.

Mkapa alipotangaza kifo cha Makamu wake, alisema alifariki ghafla saa 5: 45 usiku wa Jumatano. Kiongozi huyo alizaliwa Juni 26,1941.

Kitaaluma alikuwa mtaalamu wa mifugo na mahali anapotokea alikuwa mzaliwa wa kisiwani Pemba na historia yake ya uongozi imeandikwa pia kwenye Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), alipokuwa Waziri Kiongozi.

Waziri Kiongozi Dk. Omar, alifanya kazi hiyo kuanzia Januari 25, 1988 hadi Oktoba 1995 alipoanza rasmi kazi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.

Mwaka 1988 alikuwa Waziri Kiongozi wakati huo SMZ ilikuwa ikiongozwa na Rais Abdul Idris Wakil na ulipowadia muda wa kuondoka madarakani mwaka 1995 Zanzibar ilikuwa chini ya Salmin Amour Juma.

Dokta Omar pamoja na Mkapa walikuwa wamechaguliwa kuongoza tena Tanzania kwenye uchaguzi wa Oktoba 2000 na alianza kuwa Makamu wake rasmi mwaka 1995.

Jumatano mchana ambayo jioni aliaga dunia, Dk. Omar alikuwa pamoja na Mkapa kwenye mazungumzo ya amani ya Congo yaliyokuwa baina ya viongozi wa Tanzania, Rais wa Uganda Yoweri Museveni na Kabila wa Congo. Katika mkutano huo, Uganda ilidaiwa kuhusika na kuwaunga mkono waasi wa Congo waliokuwa wakipambana na serikali ya DRC.

TUNU ALIZOACHA

Dokta Omar anakumbukwa kwa mengi hasa suala la ulinzi, utunzaji wa mazingira pamoja na mikakati ya taifa ya kupunguza umaskini.

Sera ya Taifa ya Mazingira (NEP) iliyoanza kuandaliwa tangu mwaka 1996 na kukamilika mwaka 1997 ni mambo yaliyofanywa chini ya uongozi wa Ofisi ya Makamu ya Rais, Dk. Omar.

Akiwa na jukumu la kufanikisha Mkakati wa Kupunguza Umaskini Tanzania (MKUKUTA), Makamu wa Rais, Dk. Omar pamoja na Mkapa, majina yao hayawezi kusahaulika kwenye kuundaa na kuutekeleza mpango huo ulioanza mwaka 2001 hadi 2002, kisha 2004 hadi 2005.

Watanzania watakumbuka kuwa kuanzia katikati ya miaka ya 1990 kipindi ambacho awamu ya tatu iliingia madarakani, suala la kupambana na umaskini lilikuwa ajenda ya dunia na hilo likawa moja ya malengo muhimu ya kuondoa umaskini ili kufikia maendeleo endelevu.

TANZANIA YA VIWANDA

Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk. Omar ilibeba ajenda ya kuondoa umaskini ambayo kwa Afrika inaanzia kwenye mkutano wa Cairo uliofanyika mwaka 1994.

Baada ya mkutano huo jukumu la kuondoa umaskini lilibebwa na Ofisi ya Makamu wa Rais, na mikakati mingi kama MKUKUTA ilioandaliwa kuanzia 1997, kisha kufuatiwa na Tanzania Development Vision 2025.

Mpango huo wa muda mrefu ulilenga kuiona Tanzania mwaka 2025 ikiwa ni taifa la uchumi wa kati, taifa la viwanda na lisilo na kiwango kikubwa cha umaskini.

Maono hayo ya Dk. Omar yalitimia mwaka 2020 July, wakati awamu ya tano ilipotangaza kuwa Tanzania imeingia kwenye orodha ya mataifa ya uchumi wa kati.

Japo hakuishi na kuliona taifa likiingia kwenye zama mpya za maendeleo fikra na kazi zake zilizotukuka zinaendelea kuiongoza nchi kujipatia mafanikio zaidi.