Dodoma Sekondari yawaita wahitimu kuchanga mil. 200/- za uzio wa shule

19Mar 2019
Yasmine Protace
Dodoma
Nipashe
Dodoma Sekondari yawaita wahitimu kuchanga mil. 200/- za uzio wa shule
  • Kishindo cha Jafo chawezesha kazi kuanza
  • Yalia tangu zama hizo mpaka haukujulikana
  • Eneo shule lageuka kijiwe, njia ya magari

NI shule kongwe, inayojulikana kwa wengi. Sasa ina umri unaotimu miaka 60. Ni mahali ambako pamezalisha majina makubwa ya nchi. Lakini hali yake ya leo ikoje? Hali si nzuri kiasi kwamba waliowahi kusoma hapo sasa wanaombwa kuikumbuka shule hiyo.

Ni shule inayokabiliwa na changamoto ya uzio, mahali iliko katikati ya Jiji la Dodoma.

Tayari uongozi wa shule unalalamika kwamba, kuna matatizo ya kibinadamu kama vile utoro, magari kupita ndani ya shule, baadhi ya watu wasiostahili wakiwamo wafanyabiashara wanaoendesha biashara zao katika eneo hilo.

Mbali na kutokuwapo uzio, Mwenyekiti wa Bodi wa Shule hiyo, Phillibert Bugenda, anataja changamoto nyingine ni mahitaji ya mabweni, maabara na vitanda.

Hilo ni tamko lake katika kikao cha kawaida kilichowakutanisha wazazi mwanzoni mwa mwezi huu, kuhusu kuchangia ujenzi wa uzio huo.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo wa bodi, shule hiyo haina mipaka bayana kutokana na ukosefu wa uzio, hali inayowapa walimu mtihani wa kiusimamizi dhidi ya wanafunzi.

Anasema:"Kutokana na ukosefu wa uzio shule imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo kuibiwa mali za shule.”

Bugenda anataja matatizo mengine ni kuingiliwa na mifugo, kutoroka kwa baadhi ya wanafunzi, kushindwa kudhibiti uchelewaji wa wanafunzi, kuingiliwa na wafanyabiashara, pia wenye magari kugeuza maegesho yao na watu wenye matatizo ya akili kupageuza makazi yao.

Bugenda anasema, uwepo wa uzio, utaisaidia kuiepusha shule na changamoto tajwa, jambo analoamini litaleta mchakato tija kwa mchakato mzima wa ufundishaji shuleni.

Anataja faida kubwa ya uzio ni kuimarisha nidhamu ya wanafunzi, inayoangukia katika kuinua kiwango cha ufaulu shuleni.

Kampeni zilikoanzia

Mwenyekiti huyo anarejea mchakato wa ujenzi wa uzio ulianza mwaka 1978 bila ya mafanikio, japo zilitolewa fedha Shilingi 340,000 na Wizara ya Elimu.

Anafafanua: “Novemba 16 mwaka 1978, pesa hiyo ilitolewa kwa ajili ya ujenzi wa uzio na Chama cha Ushirika na Ujenzi Dodoma, kilipewa jukumu la ujenzi kwa mkataba wenye namba Dd/ RDB/ 6/78/79/1/86 wa tarehe 5, Desemba 1978.”

Anafafanua kuwa, kampuni hiyo haikufanikisha ujenzi huo licha ya kununua vifaa vyote vilivyohitajika kwa ajili ya mradi, kwa sababu ya kukosekana mipaka sahihi katika eneo la shule.

Bugenda anasema, ni hali iliyomlazimu aliyekuwa Mkuu wa Shule, kumwandikia Mkurugenzi wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) barua ya kudai ufafanuzi wa mipaka hiyo.

Mwenyekiti Bugenda, anasema tangu wakati huo kumekuwapo na mafanikio mbalimbali ya kupatikana mipaka ya mawe ya shule hiyo.

"Novemba 24, 2018, baada ya agizo la Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, katika mahafali ya kidato cha nne, Novemba 2, mwaka 2018, Halmashauri ya Jiji ilitoa ufafanuzi juu ya eneo la shule na mipaka," anasema.

Aidha, kibali na ramani ya ujenzi vimetolewa, kwa ajili ya mchakato na ujenzi kuanza na shule inafuatiliwa kwa karibu, huku uandaaji gharama za ujenzi wa uzio wa ukuta na kamati ya ujenzi ya uzio huo kwa ngazi ya shule imeshaundwa.

Bugenda anasema, kumeshafanyika makadirio ya gharama ya ujenzi, ambayo ni wastani wa zaidi ya shilingi milioni 200.

Anasema, ni ujenzi unaotarajiwa kuendana na mahitaji ya kisasa ya Jiji la Dodoma na msimamzi wake atakuwa, Mkurugenzi wa Jiji, kupitia Ofisi ya Mhandisi wa Jiji.

Vyanzo mapato

Anataja vyanzo vya mapato vya kutekeleza mradi huo ni kupitia Kamati ya Ujenzi wa Uzio, inayoratibu kupata mapato kutoka kwa wadau wa shule, wizara na taasisi zake, watu waliosoma shule hiyo walioko ndani na nje ya nchi.

Wengine ni wadau wa elimu, wazazi na wanafunzi, mashirika ya umma, taasisi za fedha, wafanyabiashara wakubwa, kampuni za simu na watu wote watakaoguswa na mradi huo.

Anasema bodi kupitia uongozi wa shule, hasa Kamati ya Ujenzi wa Uzio, imepanga kuwafikia wadau kwa nyakati tofauti, ili kuomba ushirika katika kupata kiwango cha fedha tajwa, kuufanikisha mradi.

Anasema serikali kuu imewapatia shilingi bilioni 1.3, pesa zitakazotumika kununua vitanda, ujenzi wa mabweni mawili ya wasichana, ukarabati wa shule nzima na maabara.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Bodi, kikao cha tarehe 2, mwezi huu, kilikutana na wazazi wenye watoto katika shule hiyo, ambao waliahidi kuchangia mradi huo wa ukuta wa shule.

Anasema katika kikao hicho, ahadi kutoka kwa wazazi ilikuwa shilingi milioni sita na pesa taslimu shilingi 730,000 zilikusanywa.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Bodi, tarehe 30, mwezi huu, wamepanga kukutana na watu waliosoma Dodoma Sekondari, kuchangia ujenzi wa ukuta huo.

Anasema ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za serikali kuwasomesha watoto bure na kuboresha miundombinu iliyochakaa katika shule.

Habari Kubwa