Donald Trump: Kasi yake kuwania tiketi ya Republican yazidi kutisha

27Feb 2016
Na Mwandishi Wetu
Las Vegas, Nevada
Nipashe
Donald Trump: Kasi yake kuwania tiketi ya Republican yazidi kutisha

BAADA ya chaguzi ndogo nne kwenye jimbo moja moja, kinyang’anyiro cha kuwania urais kwa tiketi ya Republican sasa kinakwenda kwenye ngazi ya kitaifa kikiwa na kinara asiyepingika: Donald Trump.

Donald Trump.

Trump - ambaye ameshinda chaguzi tatu kati ya hizo nne, ukiwemo ushindi wa kishindo kwenye Jimbo la Nevada – sasa anajiandaa kukabiliana na mahasimu wake kwenye chaguzi 11 wiki ijayo katika kile kinachojulikana kama mapambano ya Jumanne Kuu, yakifuatiwa na mlolongo wa chaguzi ndogo ndogo kwenye kipindi chote cha Machi na Aprili.

"Itakuwa miezi miwili ya kusisimua," Trump aliwaeleza wafuasi wake mjini Las Vegas baada ya ushindi wake wa Nevada. "Tunaweza tusihitaji hiyo miezi miwili."

Wakati huo huo, wapinzani wake Marco Rubio, Ted Cruz, John Kasich, na Ben Carson wanaendelea kupambana wao kwa wao kumpata mmoja wao wa kumkabili mfanyabiashara huyo tajiri wa New York. Lakini hakuna dalili kwamba yeyote kati ya hao wanaopambana na Trump anapanga kuachia ngazi hivi karibuni.

Rubio, ambaye alimng’oa Cruz na kushika nafasi ya pili kwenye uchaguzi wa Nevada, Jumatano iliyopita aliieleza Fox & Friends kwamba sehemu kubwa ya wafuasi wa Republican walikuwa hawataki mfanyabiashara huyo mtata awe mteule wao, lakini "hadi kutakapokuwepo na aina fulani ya mshikamano, hamuwezi kuwa na mbadala wa wazi wa Donald Trump."
Baada ya kupoteza uchaguzi wa Iowa kwa Ted Cruz uliofanyika Februari mosi, Trump hivi sasa ameshashinda chaguzi zilizofanyika New Hampshire, South Carolina, na Nevada.

Cruz, akizungumza na wafuasi wake mjini Nevada kwenye usiku wa uchaguzi huo, aliuelezea ushindi wake wa Iowa kama ushahidi kwamba yeye pekee ndiye ‘mhafidhina thabiti’ anayeweza kumshinda Trump, na kwamba kinyang’anyiro hicho kinapaswa kuwa cha watu wawili – kati yake na Trump.

"Majimbo hayo manne ya kwanza yamefanya kazi muhimu sana ya kupunguza kinyang’anyiro hiki na kuwasilisha chaguzi la wazi," Cruz alisema.

Cruz na wengine ndani ya Republican wamekuwa wakihoji dhamira ya Trump linapokuja sula la uhafidhina, wakikumbushia kwamba hapo nyuma aliwahi kuunga mkono wagombea na sera za chama cha Democratic.

Wafuasi wengine wa Republican wanasema mapendekezo ya Trump - kama vile kujenga ukuta kwenye mpaka wa Marekani na Mexico na uzuiaji wa muda wa Waislamu kuingia Marekani – yatawafanya wapiga kura wa kawaida kutowapigia kura kwenye uchaguzi mkuu, kama ilivyo pia kauli zake tata juu ya wanawake, wahamiaji, wanaharakati, na wengine wanaomshutumu.

Mjini Nevada na kwenye majimbo mengine, wafuasi wake wanasema Trump ni kiongozi imara na mtu wa ‘nje’ ambaye ataufanyia mabadiliko mfumo wakati yatakapokuja masuala kama vile uchumi, sera ya nje, na uhamiaji haramu.

Awamu mpya ya kampeni hii inaanza Jumanne kwa chaguzi kwenye majimbo 11, zaidi ya nusu kati ya hayo yakiwa kusini na kusini magharibi – likiwemo Texas, jimbo la nyumbani kwa Cruz, ambako atakabiliwa na kile kinachoweza kuwa kinyang’anyiro chake cha kufa au kupona dhidi ya Trump.

Cruz alipata uungwaji mkono mwingine Jumatano iliyopita kutoka kwa Gavana wa Texas, Greg Abbott, ambaye alimuelezea seneta huyo kama "kiongozi tunayeweza kumuamini kurudisha tena heshima yetu."

Kwenye taarifa moja ya video, Abbott alisema wahafidhina wa Texas walikuwa "wanahitaji kufanya kweli. Huu ni wakati wetu. Ted Cruz ni mgombea wetu.

Kwa upande wake, Trump ameshakejeli dhana kwamba wahasimu wake wakiweka mgombea mmoja tu hatimaye huyo mtu ataweza kumfikia, akisema yeye pia atakuwa akizidi kupata wapiga kura kila pale wagombea wengine wanapojitoa.

Na kama haitoshi, wakati akizungumza na wafuasi wake mjini Las Vegas, Trump aliweka bayana utabiri wake kwamba atafanya vizuri kwenye Jimbo la Texas.

Bilionea huyo pia anawania kuwagalagaza Rubio na Kasich kwenye majimbo yao ya nyumbani ya Florida na Ohio, huku yote mawili yakifanya chaguzi zake Machi 15.

Yeye ndiye anayeongoza kwenye kura za maoni kwenye majimbo hayo hadi sasa.

Akizungumza Jumatano kwenye kipindi cha televisheni cha Good Morning America cha CBS, Trump alisema ilikuwa bado ‘mapema sana’ kuanza kuzungumzia juu ya kuchagua mgombea mwenza wake.

Kwa upande mwingine, Kasich na Carson, ambao wote wawili walimaliza wakiwa na tarakimu moja kwenye uchaguzi wa Nevada, wanasema sasa wanapanga kuanza kampeni zao kwa kufanya vizuri kwenye majimbo yatakayofanya chaguzi siku ya Jumanne Kuu.

Ushindi huo wa maajimbo matatu unampatia Trump uongozi wa mapema miongoni mwa viti ambavyo ndivyo haswa vitaamua uteuzi wa mgombea wa tiketi ya Republican.

Makadirio yanampa mfanyabiashara huyo wa New York viti 79, akifuatiwa na Cruz (16) na Rubio (15). Jumla ya viti 1,237 vinahitajika kumteua mgombea huyo.

Rubio, akionekana kwenye kipindi cha CBS cha This Morning, alisema watu wanapaswa ‘kuwa na ujasiri’ kwenye hatua hiyo ya kampeni.

“Haitegemei ni majimbo mangapi utakayoshinda," alisema. "Inategemea ni viti vingapi utachukua."

Habari Kubwa