DRC na `safari ya matumaini’ Kujiunga na Jumuiya ya EAC

03Jul 2019
Mashaka Mgeta
Dar es Salaam
Nipashe
DRC na `safari ya matumaini’ Kujiunga na Jumuiya ya EAC

NI dhahiri kwamba Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) inayoongozwa na Rais Felix Tshisekedi, imedhamiria kujiunga katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), yenye nchi wanachama sita.

Nchi hizo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini ambazo kwa sehemu zimepakana na taifa hilo lenye utajiri wa madini yanayokisiwa kuwa na zaidi ya aina 1,100.

Barua ya Rais Tshisekedi aliyomwandikia Mwenyekiti wa EAC, Rais Paul Kagame Juni 8 mwaka huu, kauli yake na ile ya Rais John Magufuli kuhusu Tanzania kuunga mkono kusudio la DRC ni miongoni mwa vielelezo vinavyoashiria utayari wa nchi hiyo kuwa mwanachama wa EAC.

Tayari Rais Kagame ameshawasilisha maombi hayo kwa Sekretarieti ya EAC ili yajadiliwe katika mkutano wa wakuu wa nchi wanachama utakaofanyika Novemba mwaka huu.

Akizungumza kwenye hafla aliyomuandalia Rais Tshisekedi, Rais Magufuli alisema Tanzania inatambua uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya nchi mbili hizo na kwamba itakuwa tayari kuunga mkono maombi yake (DRC) ya kujiunga EAC.

Akiwa nchini Tanzania, Rais Tshisekedi alisema nchi yake inatamani kuwa mwanachama wa EAC ili pamoja na mambo mengine, kukuza fursa za masoko, biashara, uchumi na kuimarisha hali ya utulivu kwenye ukanda huo.

Rais Magufuli alisema takwimu za mwaka jana zinaonyesha kuwa DRC na Tanzania zinafanya biashara yenye thamani ya Sh. bilioni 305 wakati uwekezaji wa nchi hiyo kwa Tanzania ukiwa ni Dola milioni 5.77 uliozalisha ajira 418.

Pia DRC imekuwa ikiitumia bandari ya Dar es Salaam kwa kupitisha mizigo yake inayokadiriwa kuwa tani milioni 1.18, hivyo kuibua umuhimu wa kuondoa vikwazo vya biashara kwa nchi hizo.

KWA NINI DRC KUINGIA EAC

Zipo sababu nyingi zinazotumika kama kigezo kwa DRC kutaka kuwa mwanachama wa EAC, miongoni mwa hizo ni kukuza na kuendeleza uhusiano uliopo katika nyanja tofauti na mataifa yaliyo mwanachama wa EAC.

Itakumbukwa kwamba katika mkutano wa kimataifa wa wawekezaji uliofanyika jijini Kigali, Rwanda hivi karibuni, Rais Tshisekedi alishiriki na kuelezea fursa nyingi zilizopo nchini mwake, lengo likiwa ni kuwavutia wawekezaji zaidi.

Lakini pia ni kwamba DRC inapakana karibu na nchi zote za EAC kiasi kwamba miongoni mwa hizo zimewahi kuwa katika uhusiano mbovu wa kidiplomasia unaotokana na madai ya kusaidia vikundi vya wanamgambo na wizi wa madini nchini humo.

Johnson James ni mtaaluma wa uhusiano wa kimataifa, anasema ingawa DRC ipo kwenye jumuiya nyingine kama ilivyo kwa baadhi ya wanachama wa EAC, lakini kuingia katika ukanda huo (Mashariki), kutainufaisha kwa karibu na haraka.

“Kwa mfano DRC ni mwanachama wa SADC kama ilivyo Tanzania, lakini hauwezi kuyaona manufaa ya nchi nyingine ya SADC kama Lesotho kwa mfano, kuwa na athari za karibu na moja kwa moja kwa Tanzania ama nchi nyingine za EAC,” anasema.

Anasema kama DRC ikifanikiwa kuwa katika EAC, itachagiza ukuzaji wa fursa za kiuchumi kwa taifa hilo lakini pia kurahisisha uingizaji bidhaa na huduma kutoka nchi nyingine zilizo kwenye jumuiya hiyo na ambazo pia ni majirani zake wa karibu.

FURSA ZA KIUCHUMI

James anasema DRC itakapoingia kwenye EAC itakuwa imetanua wigo wa soko kwa bidhaa zake hasa zinazotokana na madini na vito, ili kuwafikia watu wa ukanda huo.

Pia DRC ina sehemu kubwa ya ardhi yenye rutuba hasa katika ukanda wa Mto Congo na hivyo kuwa sehemu inayofaa kwa uzalishaji wa chakula na viungo vinavyoweza kupata soko kubwa na la karibu katika ukanda wa EAC.

Hatua ya DRC kuingia EAC italiwezesha taifa hilo kujiunga katika miradi ya pamoja kama ujenzi wa miundombinu ya usafiri na usafirishaji, hivyo kuifanya sehemu yake kufikika kwa urahisi zaidi.

Mchambuzi wa masuala ya siasa aliyepo Nairobi nchini Kenya, Jeremiah Owiti, aliliambia gazeti moja hivi karibuni kuwa hatua ya DRC kujiunga EAC, kutatanua wigo wa biashara na mawasiliano kutoka ukanda wa Afrika ya Kati.

Tangu alipoapishwa Januari mwaka huu kuchukua nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Rais (mstaafu) Joseph Kabila, Rais Tshisekedi amekuwa akionyesha dhamira ya wazi kutaka DRC ijiunge EAC.

EAC ina masharti kadhaa kwa mwanachama mpya kujiunga, miongoni mwa hayo ni kuheshimu misingi ya demokrasia, utawala wa sheria, uwajibikaji, uwazi na haki za binadamu.

Mkataba ulioanzisha jumuiya hiyo unaelezea pia kuwa, mbali na sababu za kijiografia, usawa katika fursa, usawa wa kijinsia na kutambua, kuendeleza na kulinda haki sawa kwa mujibu wa tamko la Umoja wa Afrika (AU) kuhusu haki za binadamu, ni miongoni mwa vigezo vya kuwa mwanachama wa EAC.

Mkurugenzi wa kampuni ya TradeMark East Africa nchini Rwanda, Patience Mutesi, alikaririwa na gazeti moja akisema ukubwa wa kijiografia na idadi ya watu katika ukanda wa EAC kunatoa fursa pana za biashara na wateja.

BIASHARA

Katika kipindi cha mwaka jana, takwimu zinaonyesha kuwa Uganda inauza bidhaa zenye thamani ya dola za Marekani milioni 398 kwenda DRC huku ikipanga kukuza biashara hiyo kufikia dola bilioni 2 ifikapo 2020.

Wakati huo huo, Uganda iliiingiza bidhaa za DRC zinazokadiriwa kuwa na thamani ya dola milioni 2.5.

Kwa upande wa Rwanda, takwimu zinaonyesha kuwa nchi hiyo iliuza bidhaa zenye thamani ya dola milioni 456 wakati ikinunua bidhaa zenye thamani ya dola milioni 11.2 kutoka DRC.

Tanzania iliuza bidhaa zenye thamani ya dola milioni 153 kwa mwaka 2017 na kuingiza zenye thamani ya dola milioni 1, kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Makala haya yameandikwa kwa msaada wa vyanzo mbalimbali. Mwandishi anapatikana kwa simu namba 0754691540 ama barua pepe:[email protected]