Duru mpya ya mazungumzo yaanza

15May 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Duru mpya ya mazungumzo yaanza
  • Waandamanaji wasalia Makao Makuu ya Jeshi Sudan

VIONGOZI wa kijeshi wa Sudan na  waandamanaji wameanza duru mpya ya mazungumzo kwa ajili ya kufikia makubaliano ya kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia, huku waandamanaji wakiendelea kupiga kambi nje ya Makao Makuu ya Jeshi.

Jumamosi iliyopita, Muungano wa Uhuru na Mabadiliko ambao ni mwamvuli wa vuguvugu la waandamanaji, ulisema viongozi wa kijeshi walituma mwaliko wa mazungumzo mapya baada ya mkwamo wa siku kadhaa.

Msemaji wa muungano huo Rashid al-Sayed alisema awali mazungumzo hayo yalikuwa yafanyike siku hiyo ya Jumamosi, lakini yakaahirishwa hadi juzi yalipoanza rasmi tena.

Sayed hakufafanua kwanini mazungumzo hayo yalisogezwa mbele, lakini vyanzo tofauti ndani ya muungano vinasema kulihitajika muda zaidi kwa ajili ya mashauriano ya kiutawala.

Msemaji wa Baraza la Kijeshi linalotawala nchini humo, Luteni Shamseddine Kabbash, alithibitisha kuanza kwa duru mpya ya mazungumzo na kuongeza kuwa yanafanyika kwenye mazingira yenye kutia moyo ili kufikia makubaliano ya kipindi cha mpito.

“Tunakubaliana nao juu ya muundo wa jumla wa mfumo wa kiutawala wakati wa kipindi cha mpito kwa kuzingatia baraza huru, mfumo wa serikali, mfumo wa bunge na mifumo mingine,” anasema na kuongeza:

“Tulichogundua ndani ya pendekezo lao lililowasilishwa kwetu ni kwamba waliondoa chanzo cha sheria…maoni yetu ni kwamba Sheria ya Kiislamu na tamaduni katika Jamhuri ya Sudan, viwe ndio chanzo cha sheria.”

Duru hiyo mpya ya mazungumzo inakuja wakati maelfu ya waandamanaji wakiendelea kupiga kambi nje ya makao makuu ya Jeshi jijini Khartoum.

Wanasema wamedhamiria kulishinikiza Baraza la Kijeshi kukabidhi madaraka, kama ambavyo walivyomuondoa Omar al-Bashir.

Viongozi wa kijeshi na waandamanaji wanatofautiana juu ya nani ataliongoza baraza la mpito.

Jeshi linapendekeza baraza jipya liongozwe kijeshi, huku waandamanaji wakitaka uwakilishi mkubwa wa raia ndani ya baraza hilo.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, muungano wa upinzani uliwasilisha mapendekezo yao kwa jeshi kuhusiana na serikali ya mpito, itakayoongozwa kiraia.

Wakati huohuo, waandamanaji wamezuia mtaa mkubwa ulioko kando ya mto Nile kwa kutumia mawe na miti, baada ya vikosi vya usalama kuwazuia kuingia eneo ambalo wenzao wamepiga kambi.

Baraza la kijeshi limelaani kitendo hicho likisema hakikubaliki na kinachochea vurugu, hivyo kufanya maisha kuwa magumu kwa raia wengine. AFP