Duwasa inavyojipanga kwa mji mpya unaobeba serikali kamili

29Jun 2017
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Duwasa inavyojipanga kwa mji mpya unaobeba serikali kamili

NYUMBANI hakuna kitakachopikwa bila ya maji;hakuna atakayeoga bila ya maji na mengine mengi. Hiyo ndiyo inazaa msamiati ‘Maji ni uhai.’

Katika kutambua umuhimu huo,serikali imeanzisha mamlaka mbalimbali za maji katika sehemu zote nchini kutetea ‘uhai’ wa maeneo hayo.

Manispaa yaDodoma, tangu mwaka 1998, ilishaanzishiwa Mamlaka ya Majisafi na MajitakaDodoma (Duwasa), ambayo uwepo wake umeleta mabadiliko chanya katika huduma za maji na majitaka.

Jukumu rasmi la Duwasa ni kutoa huduma bora na endelevu za usambazaji majisafi na usafi wa mazingira, kwa wakazi, wateja wake kutoka manispaa hiyo na maeneo jirani.

Hivi karibuni, serikali ilitangaza azma yake ya kuhamia Dodoma, kupitia mpango ambao awamu yake ya pili ya watumishi wa umma kuhamia, inatarajiwa kuingia mwishoni mwa mwezi huu.

Hapo maana yake ni ongezeko la kuwapo majukumu zaidi ya kuhudumia ongezeko la mahitaji ya kibinadamu.

Mkurugenzi Mkuu wa Duwasa, Mhandisi David Pallangyo, anaeleza mikakati mbalimbali ya Duwasa,kwamba imejipanga kuhakikisha mji una maji yanayokidhi mahitaji hayo.

Uwezo wake

Anasema kiasi cha maji safi kinachozalishwa sasa katika visima vya Mzakwe, Duwasa kina uwezo wa kuhudumia wanaohamia mji huo.

Mhandisi Pallangyo, anasema kwa sasa Duwasa inazalisha mita za ujazo 61,500 za maji, kiasi kinatosha mahitaji ya wakazi wote wa Dodoma na ziada kupatikana.

Anasema uimarikaji huo unaokidhi mahitaji, unatokana na kutekelezaji miradi miwili mikubwa ya maji walio nayo.

Mhandisi Pallangyo anaitaja miradi hiyo kuwa ni, pamoja na uboreshaji huduma za maji mjini Dodoma, uliotekelezwa kwa mkopo wa masharti nafuu kutoka serikali ya Korea kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Kiuchumi (EDCF).

Kwa mujibu wa Mhandisi Pallangyo, ni mradi unaogharimu Dola za Marekani milioni 48.7sawa na Sh. bilioni 108.8.

Mradi mwingine unahusu ujenzi wa Mfumo wa Majisafi na Majitaka wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), uliogharimu Sh. bilioni 27.679.

Mhandisi Pallangyo anaeleza kuwa, kupitia mradi wa kuboresha huduma za maji mjini Dodoma uliotekelezwa kuanzia Januari 2013 hadi Aprili 2015, umeongeza uwezo wa kuzalisha na kusafirisha maji kutoka Chanzo cha Maji Mzakwe, kufikia mita za ujazo 61,500 kwa siku kutoka mita 32,000 za mwanzo.

Ni maboresho yenye tija ya kuongeza muda wa upatikanaji maji kwa siku, kutoka saa 16 hadi saa 22 za sasa.

Utafiti wa mahitaji

Anasema utafiti na stadi za karibuni kuhusu mahitaji ya maji kwa wakazi wa Dodoma, ulifanywa kati ya mwaka 2002 na 2003, Seurecea/Netwas na COWI Consult, mahitaji ya maji mjini hapa ni wastani wa mita za ujazo 46,000 kwa siku.

Anasema kiasi hicho, kinajumuisha mahitaji ya chuoni Udom, yanayofika wastani wa mita za ujazo 4,000 kwa siku.

Vyanzo na uwezo

Mkurugenzi huyo anasema, chanzo pekee cha uzalishaji maji kwa matumizi ya wakazi, ni visima virefu vilivyochimbwa katika bonde la Makutupora, nje ya mji.

“Bonde hili lipo kilomita 30 kutoka mjini Dodoma. Kuna jumla ya visima vya uzalishaji maji 24 na visima vitano vya kuchunguza mwenendo wa maji ardhini, Uwezo wa visima vilivyopo kwa sasa pamoja na uwezo wa usafirishaji maji ni mita za ujazo zipatazo 61,500m3 kwa siku,”anasema.

Mhandisi Pallangyo anasema, katika mwaka 2000,serikali ilifanya tathmini ya kulipa fidia wananchi waliokuwa wakazi ilikochimbwa visima - Makutupora na mwaka 2002 ilizilipa fidia kaya 2048 zilizoishi ndani ya mabonde ya vijiji vya Mzakwe, Gawaye, Mchemwa na Mamba.

“Mnamo mwaka 2007, serikali ilitekeleza uamuzi wa kuzihamisha kaya hizo,”anasema na kuongeza kuwa
eneo hilo lenye chanzo cha maji linatunzwa na haliingiliwi na shughuli za kibinadamu.

Mnamo Septemba 21,2012, Waziri mwenye dhamana ya sekta ya maji, kupitia Gazeti la Serikali, alilitangaza Bonde la Mkutupora kuwa eneo Tengefu/lililohifadhiwa, hivyo kuzuia shughuli zozote za kibinadamu kufanyika mahali hapo.

“Kwa sasa ulinzi na utunzaji wa chanzo hiki unafanyika kwa ushirikiano na Jeshi la Kujenga Taifa la Makutupora, DUWASA na Ofisi ya Bonde la Wami/Ruvu,”anasema.

Usambazaji maji mjini

Mhandisi Pallangyo anasema, maji yanaposukumwa kutoka visimani, hukusanywa kwenye matanki mawili yenye mita za ujazo 680 na lingine 800, yaliyopo Mzakwe.

“Ndani ya matanki hayo, maji hutibiwa kwa kutumia (dawa)chlorine iliyo katika mfumo wa Calcium Hypochlorite. Baada ya kutibiwa, maji huruhusiwa kuingia kwenye vituo vya kusukuma maji kwenda mjini.

“Kuna mabomba makuu mawili ya kusafirishia maji kutoka kwenye chanzo eneo la Mzakwe kuja mjini, yenye vipenyo vya milimita 600 (inchi 24) kila moja.

“Mabomba hayo yana uwezo wa kusafirisha zaidi ya mita za ujazo 60,000 kwa siku kwa pamoja,”anasema.

“Mtandao wa kusambazia majisafi kwa sasa una jumla ya urefu wa kilomita zipatazo 427.6 Mtandao huu,” anasema na kuongeza kuwa hadihatua ya mwisho, jumla ya matenki yote yana mita za ujazo 92,030.

Inaelezwa kwamba, mtandao huo unawezesha kukidhi asilimia 82 ya wakazi wote 500,000 kupata maji ya Duwasa, ambayo ina jumla ya wateja 35,413 wa majisafi,

Mgawanyo wao ni wateja wa majumbani wanachukua asilimia 94; taasisi asilimia 2.7; wateja wa biashara, asilimia 2.7; na wengineo ni asilimia 0.6.

Mradi mpya

Mhandisi Pallangyo anasema, Duwasa kwa kushirikiana na Wizara ya Maji na Umwagiliaji, inatarajia kutekeleza mradi wa kuzalisha majisafi kwenye bwawa la Farkwa lililopo Wilayani Chemba.

Anasema ni mradi utakaoongeza upatikanaji wa huduma ya maji na utakapokamilika, utaiwezesha Duwasa kuwahudumia watu milioni, maji yatanayoelekezwa katika mji wa kiserikali unaoandaliwa.

“Pindi uzalishaji wa maji katika bwawa la Farkwa utakapokamilika, kiasi cha mita za ujazo zipatazo 120,000 zitatumika kwa ajili ya Dodoma. Mradi utahudumia pia wilaya nyingine za Bahi, Chamwino na Chemba,”anasema Mhandisi Pallangyo.