EAC imsaidie Tshisekedi kukamilisha miradi ya Kabila

20Mar 2019
Mashaka Mgeta
Dar es Salaam
Nipashe
EAC imsaidie Tshisekedi kukamilisha miradi ya Kabila

SERIKALI mpya ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imeingia madarakani kutokea ‘chama kipya’ cha Union for Democracy and Social Progress (UDPS) kinachoongozwa na Rais Felix Tshisekedi, huku taifa hilo likigubikwa na migogoro na vitendo vya uporwaji rasilimali za taifa hilo.

Rais mstaafu Kabila pamoja na Felix Tshisekedi, mara baada ya kuapishwa kuongo Congo. PICHA:MTANDAO.

Rais Tshisekedi alishinda nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Desemba 30, mwaka jana, kwa kupata kura milioni 18 (kabla ya maeneo mengine kupigwa na kuhesabiwa) ikiwa ni sawa na asilimia 38.57 na kumpita mshindani wake wa karibu, Martine Fayulu aliyepata kura milioni 6.4.

Mgombea wa chama tawala cha People's Party for Reconstruction and Democracy (PPRD), Emmanuel Ramazani Shadary, aliyetarajiwa kushinda kutokana na kuungwa mkono na Kabila, aliambulia kura milioni 4.4.

HALI YA DRC

Inapotajwa DRC, fikra inayojitokeza kwa haraka ni kuwapo kwa vikundi vya waasi, mapigano yanayosababisha vifo na majeruhi na madai ya kuwapo askari kutoka nchi jirani wanaokwenda kusaidia harakati za waasi nchini humo.

Ingawa ni hivyo, DRC iliyoachwa na Rais mstaafu Joseph Kabila, inaendeleza miradi kadhaa ya maendeleo ya nchi na ustawi wa watu.
Miradi hiyo kama ilivyo kwa mataifa mengine yanayoendelea ni mingi, ikiwategemea washirika wake wakiwamo wadau wa maendeleo na nchi majira zikiwamo zile za kikanda.

Miongoni mwa washirika wakubwa wa DRC ni kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zilizowahi kuonyesha nia ama kusaini mikataba ya kushirikiana na serikali ya Kabila.

Kuimarika kwa ushirikinao kati ya DRC na nchi za EAC ni jambo lisilokwepeka kwa kuwa licha ya kukuza biashara, uchumi na uzalishaji, pia unachangia kuimarisha usalama wa ukanda huo.

MAENEO YA USHIRIKIANO

DRC ina maeneo mengi yenye umuhimu wa kukuza ushirikiano na hivyo kuifanya serikali ya Rais Tshisekedi kuhitaji msaada endelevu kutoka kwa wanachama wa EAC.

Oktoba 2016, Kabila alifanya ziara ya kikazi nchini na kusaini mikataba kadhaa na mwenyeji wake, Rais John Magufuli, hatua hiyo inakuja wakati ujazo wa biashara kati ya Tanzania na DRC ukiwa umekua kutoka shilingi bilioni 23, mwaka 2009 hadi bilioni 394 mwaka 2016.

Kwa mujibu wa ripoti ya Wakala wa Uwezeshaji wa Usafiri wa Ukanda wa Kati (CCTTFA) ya mwaka 2015, DRC ilipitisha tani milioni 11 za shehena kupitia bandari ya Dar es Salaam ikiwa ni sawa na asilimia 10 ya bidhaa zote zinazoingizwa kupitia bandarini hapo.

Kiwango cha asilimia ya bidhaa za nchi nyingine bandarini hapo ilikuwa ni wenyeji Tanzania asilimia 62, Rwanda 7.0, Burundi 3.0 na Uganda moja nyingine zisizokuwa kwenye ukanda huo zilikuwa na jumla ya asilimia 17.

Pia katika kipindi cha mwaka huo (2005) kiasi cha asilimia 25 ya bidhaa zilizosafirishwa nje kupitia bandari ya Dar es Salaam, zilitokea nchini DRC wakati asilimia 65 zilitokea hapa nchini.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, bidhaa za kutoka nchi za Rwanda, Burundi na Uganda zilikuwa katika kiwango cha asilimia 1.6, wakati bidhaa kutoka mataifa yasiyokuwa katika ukanda huo zikiwa na asilimia 9.4.

Katika mazungumzo ya wakuu wa nchi hizo, ilikubaliwa kwamba Tanzania itaongeza muda wa msamaha wa tozo kwa bidhaa zinazoingizwa Dar kwenda DRC kutoka siku 14 hadi 30.

Aidha, ilikubaliwa kwamba Tanzania itatenga eneo la bandari kavu huko Ruvu mkoani Pwani na Dodoma kwa mizigo inayokwenda DRC ili kurahisisha utoaji na usafirishaji wake.

Rais Magufuli akaihakikishia Congo kwamba Tanzania itajenga reli ya kisasa ya standard gauge (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma ili itumike kufikisha mizigo DRC kupitia bandari ya Ziwa Tanganyika mkoani humo.

Katika utekelezaji wa makubaliano hayo na kuongeza ufanisi, Tanzania iliahidi kuziboresha bandari ya Kigoma ili ishirikiane na zile za Kalemie, Kalundu na Moba nchini DRC kusafirisha shehena.

Pia, Tanzania ikapunguza vituo vya upimaji uzito wa magari ya mizigo yakiwamo ya DRC kutoka vinane kufikia vitatu vilivyopo Vigwaza, Manyoni na Nyakahura.

Wakati wa mazungumzo hayo, Kabila alisisitiza kuwa Dar es Salaam ndiyo bandari chaguo kwa ajili ya kuingiza na kusafirisha shehena ya Congo.

Kwa upande wa Uganda, mradi wa SGR unajengwa kutokea Pakwach kupitia vituo vya forodha vya Goli na Vurra huko Arua, haya ni maeneo muhimu ya kuingilia kaskazini mashariki mwa DRC.

Mradi wa SGR unagharimu mabilioni ya dola za Marekani, ukitarajiwa si tu kuunganisha nchi zilizo katika ukanda wa kaskazini, lakini pia kupunguza gharama za kufanya biashara.

UGANDA NA DRC

Gazeti la Monitor la nchini Uganda ni miongoni mwa vyombo vya habari vilivyochambua kwa kina nafasi ya Uganda katika kushirikiana na serikali ya Tshisekedi na kwamba hali hiyo inapaswa kuwapo kwa nchi zote za EAC.

“Kutangazwa kwa Tshisekedi kuwa mshindi wa urais kunachagiza matumaini miongoni mwa marafiki zake waliokuwa wakimfanyia kampeni kwa zaidi ya miaka mitano ili aachiwe huru, utawala huo mpya utakuwa tofauti?” Lilihoji gazeti hilo.

Mwaka 2005, Mahakama ya Kimataifa ya Haki iliiamuru Uganda kulipa fidia DRC baada ya kupatikana na hatia ya kuhusika na vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu. DRC ilikuwa ikidai fidia ya Dola bilioni 10 za Marekani.

Licha ya madai hayo, DRC na Uganda zimekuwa katika mgogoro wa mara kadhaa unaohusu kuingiliwa kwa ardhi zao na majeshi yanayotoka upande mwingine. Kwa hali hiyo, Uganda bado inaendelea kuwa na umuhimu wa pekee katika kupata suluhu ya changamoto zake kwa DRC.

KENYA

Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta inajenga SGR kutoka Mombasa hadi Kisumu mahali lilipo Ziwa Viktoria ili kuiungaisha nchi hiyo na mataifa mengine hususani katika nyanja za uchukuzi kwenye uchumi, biashara na uzalishaji.

ALIPOANZIA KABILA

Mwaka 2016, Rais huyo mstaafu wa DRC, Joseph Kabila, alitangaza nia ya taifa hilo kuwekeza katika ujenzi wa SGR na kwa mujibu wa jarida la Star Africa, kusudio hilo lilitamkwa pia na Balozi wa DRC nchini Uganda, Jean Pierre Massala, katika mkutano wa 13 wa miradi ya utengamano wa kaskazini (NCIP) uliofanyika jijini Uganda Aprili, 2016.

Miradi ya utengamano ya ukanda wa kaskazini ni jitihada ambazo pamoja na mambo mengine, zinapunguza gharama za kufanya biashara na kuboresha miundombinu kwa nchi zinazotumia bandari ya Mombasa.

Nchi zilizosaini mkataba wa ushirikiano katika ukanda huo ni Uganda, Rwanda, Sudan Kusini na Kenya, wakati DRC, Tanzania na Ethiopia zilikuwa waangalizi.

Jarida hilo lilieleza kuwa mradi wa SGR kwa DRC unahusu ujenzi wa reli ya kisasa, yenye uwezo mkubwa itakayoanzia bandari ya Mombasa nchini Kenya, kupitia Nairobi, Kampala -Kigali hadi Juba nchini Sudan Kusini.

Nchi nne za Jumuiya ya Afrika Mashariki zimekubailiana kutumia viwango sawa vya SGR ingawa kila taifa litajenga kwa upande wake, hivyo ilikuwa mara ya pili kwa DRC kuelezea nia hiyo, ikitanguliwa na tamko lake ililolitoa kwenye mkutano wa 11 wa NCIP uliofanyikia jijini Nairobi, Kenya.

Ingawa taarifa hizo ni kati ya nyingi zinazoyahusu mataifa hayo, umuhimu wa nchi wanachama wa EAC kuisaidia DRC ili ifikie malengo ya maendeleo hasa yaliyoanzishwa na mstaafu Kabila, ambayo yana maslahi kwa pande zote, si jambo la kubeza bali la kulifanyia kazi kwa nguvu zote.

Makala haya yameandikwa kutoka vyanzo mbalimbali.

Maoni 0754691540 ama barua pepe: [email protected].

Habari Kubwa