Elimu zaidi yahitaji kuitambulisha Kitulo ‘bustani ya Mungu’ iliyotele

21Jun 2016
Cynthia Mwilolezi
Arusha
Nipashe
Elimu zaidi yahitaji kuitambulisha Kitulo ‘bustani ya Mungu’ iliyotele

HIFADHI ya Taifa ya Kitulo yenye ukubwa wa kilometa za mraba 465.4 ni moja ya hifadhi zenye sifa za kipekee. Upekee wa hifadhi hii ni kuwa ipo juu zaidi ya hifadhi zote nchini.

Ipo umbali wa mita 3,000 toka usawa wa bahari huku hali ya hewa ikiwa ni ya baridi Ili kufika hifadhini unapandisha milima na maporomoko ya maji, mabonde yenye mvuto wa kipekee na uwanda wa nyasi zilizotapakaa , na mito ambavyo ni vivutio na fahari ya Tanzania.

Upekee mwingine mkubwa unaoibeba hifadhi hii ni maua ya kila aina. Kuna aina za maua zaidi ya 40 yanayopatikana hifadhini na si kwingineko duniani. Kwenye miezi ya Novemba na Aprili hupamba milima iliyo katika hifadhi hiyo yenye mianzi ya milimani.

Mvuto mwingine ni bonde la Nhumbe, ambalo huitwa pambo la hifadhi ya Kitulo.

Vijito vingi hutiririka chini ya uoto wa nyasi na kutengeneza maporomoko madogomadogo na kuunda mto Nhumbe, pia miti mirefu inayofikia kimo cha mita 50 ndani ya bonde ambalo inasemekana kuwa miongoni mwa miti mirefu duniani.

Mazingira hayo huvutia ndege wa aina mbalimbali kutoka Afrika Kusini, Australia na Ulaya hasa kipindi cha majira ya baridi hutua na baadhi yao kutengeneza mazalia yao.

Vivutio vingine ni nyani wa pekee anayepatikana katika hifadhi hiyo tu aitwaye Rungwecebus Kipunji ambao wana nywele ndefu aliyegundulika na mwana biolojia kutoka hirika llitwalo Wildlife Conservation Society (WCS).

Makabila manne yanayozunguka Hifadhi hii ni Wakinga, Wawanji, Wasafwa na Wanyakyusa.

Pamoja na kuwa na hazina kubwa ya vivutio , hifadhi hiyo haitangazwi kiasi kufahamika sana ndani na nje ya nchi , ili kuvutia watalii na kuchangia kukuza mapato ya jamii na taifa kwa ujumla kupitia uitalii.

Hifadhi hiyo iliyoanzishwa Septemba 16, 2005 na ina ukubwa wa Kilomita za Mraba 465.4.

Ili kuifikia hifadhi hiyo kutoka mkoani Mbeya kupitia Chimala ni umbali wa kilomita 210.

Na ukitokea Mbeya kupitia Isyonje ni umbali wa kilomita 170.Na kutoka Dar es Salaam – Makambako-Njombe- Makete hadi hifadhini ni umbali wa kilomita 963..

Mkuu wa hifadhi ya Kitulo, Pius Mzimbe anasema, kutokana na hali halisi ya mvuto wake watu wengi wa eneo la hifadhi huiita bustani ya Mungu , kutokana na maua ya asili yaliopo.

Anasema hifadhi hiyo hutembelewa na wastani wa watalii 466 kila mwaka na tangu ianzishwe mwaka 2005 hadi sasa imetembelewa na watalii 2,329.

Mzimbe anasema idadi ya watalii inaongezeka mwaka hadi mwaka.Takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2013 walipokea watalii 470 , mwaka 2014 watalii 644 namwaka 2015 watalii 662.

Pamoja na jitihada za kuitangaza hifadhi hiyo bado idadi ya watalii sio ya kuridhisha, kutokana na ubovu wa miundo mbinu ya kufika hifadhini.

Mathalani barabara ya kupitia Chimala ina kona kona 52 ambayo ni mbovu kupita kiasi. Hali hiyo inafanya wageni wanaokwenda huko hulalamika ubovu huo na iwapo itatengenezwa yatarajiwa kuchangia kuongeza idadi ya watalii.

“Ubovu wa barabara na kutokuwa na barabara ya uhakika zinazopitika kila wakati ikiwemo barabara za kuingilia milango mikuu hifadhini na njia za matembezi zikiboreshwa tunatarajiwa ongezeko litakuwa kubwa,”anasema.

Matatizo mengi katika hifadhi ni pamoja na ukosefu wa hoteli zinazokidhi huduma za utalii katika maeneo ya hifadhi na jirani na hifadhi, hivyo vyote vinachangia kushindwa kuvutia watalii na wageni wa uhakika.

Kama hiyo haitoshi pia watumishi ni wachache katika idara nyingi za hifadhini ikiwemo waongoza watalii na wasaidizi wengine katika idara.

Pamoja na changamoto hiyo kuna tatizo la ujangili kwa mmea aina ya Chikanda, ambao hufanana na kiazi mviringo au kiazi ulaya.

Wakazi wengi wa vijiji jirani na hifadhi hiyo, anasema hupenda kuingia hifadhini ili kukichimba na kwenda kukiuza, kwa sababu kinapendwa na zaidi na watu wa nchi jirani ya Zambia na mpakani Tunduma.

“Kiazi hiki huuzwa kwa debe.Kila debe huuzwa kati ya Sh.150,000 hadi 300,000 na kinapendwa sana huko,” anabainisha

Matumizi makubwa ya kiazi hicho ni hutengenezwa siagi ya kuwekwa kwenye mikate,pia kuna baadhi ya imani iliyozagaa kuwa kinaongeza kwa kasi CD4 kwa wenye maambukizi ya Virusi vya Ugonjwa wa Ukimwi.

“ Sisi kama wahifadhi hatufahamu ukweli wa hili, kwani hakuna uchunguzi uliofanyika kisayansi.Kukichimba ndani ya
hifadhi ni ujangili kama ujangili mwingine wowote,” anasema.

Hali halisi ilivyo ni kwamba, kila siku lazima mtu akamatwe akiwa anachimba viazi hivyo na shida iliopo viazi hivyo huota ndani ya hifadhi tu na hata vikipandwa nje ya hifadhi haviwezi kuzaa sana, kama mbegu moja itazaa moja tu.

“Kutokana na hali hiyo watu hawataki kupanda maana havizai faida, ukinunua kumi vitazaa viazi kumi tu.Lakini pia uwezekano wa kuzaa ni
mdogo, sababu hali ya hewa nje ya hifadhi tofauti na ndani ya hifadhi,”anasema.

Aina nyingine ya ujangili uliopo hifadhini humo ni ukataji wa kuni, fito na mbao kwa ajili ya kujengea nyumba, jambo ambalo kama wahifadhi wanajitahidi kuelimisha wananchi madhara ya kufanya hivyo.

Baadhi ya wananchi huchoma moto hifadhi kwa lengo la kulipiza kisasi wanapokamatwa wakifanya uvunaji wa viazi au mbao na mwezi ambao hupenda kuchoma ni Septemba na Agosti.

Naye Geofrey Kyando, Ofisa Utalii Hifadhi ya Kitulo, anasema hifadhi yao imeweka mikakati na malengo ya kukabiliana na changamoto zilizopo kama vile kushawishi wawekezaji kuwekeza ndani ya hifadhi na maeneo ya jirani kujenga hoteli.

Pia kuitangaza hifadhi ndani na nje ikiwemo kushiriki maonyesho mbalimbali ya utalii na yasiyo ya utalii kama Sabasaba na Nanenane.

Naye Fredrick Chuwa mmoja wa watumishi wa hifadhi hiyo, anasema hifadhi inakabiliwa na changamoto lukuki za migogoro, sababu awali lilikuwa shamba la serikali la mifugo Dafco na sehemu ilimegwa bonde la Nhumbe na msitu wa Livingstone.

“Hivyo kutokana na kugeuzwa kuwa hifadhi, baadhi ya vijiji wanaleta fujo na kudai sehemu ya hifadhi imeingia kwenye vijiji vyao, hivyo hujikuta usuluhishaji wa migogoro ikifanyika kila mara,”anasema.

Habari Kubwa