Ewura yabuni mbadala vijijini kukabili ‘maduka’ ya madumu

08Nov 2019
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Ewura yabuni mbadala vijijini kukabili ‘maduka’ ya madumu
  • Baada ya ugumu kupata mbadala
  • Wenye madumu siku zinahesabika
  • Tahadhari maegesho malori ya tenki

NISHATI ni nguzo muhimu kwa maendeleo ya binadamu. Ni msemo unaotokana na ukweli kwamba bila ya nishati mambo mengi hayawezi kufanyika, kama vile uendeshaji viwanda vya ngazi tofauti, kwa sababu ni kichocheo kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Wenye madumu katika foleni ya kununua mafuta,. PICHA: MTANDao

Nishati ya mafuta za taa, petroli na dizeli, zinatajwa kuwa kichocheo kikubwa kwa shughuli za kila siku hasa katika kuendesha mitambo mbalimbali yakiwamo magari.

Kutokana na umuhimu huo, serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imekuwa ikifanya jitihada kuhakikisha nishati hiyo inapatikana kwa wingi, ili kupunguza ulanguzi na wananchi wasipate shida katika shughuli zao za kila siku.

KULIVYO VIJIJINI

Pamoja na mafuta kuuzwa katika vituo vinavyojengwa kupitia vibali vya Ewura, hali ya upatikanaji nishati hiyo vijijini imekuwa ngumu, kutokana na hali halisi ya miundombinu.

Hadi sasa kubwa ya Watanzania wanaishi vijijini na kutokana na umuhimu wa huduma, hiyo baadhi ya wafanyabiashara wadogo wanalazimika kununua mafuta kwenye vituo mijini na kuuza reja reja kienyeji kwenye madumu na chupa za maji, kwa ujazo tofauti vijijini.

Mmoja wa wafanyabiashara hao, Joseph Mahindoni, anasema wauzaji wamekuwa wakiuza mafuta kwa ujazo tofauti kwenye maduka ya bidhaa zingine, pia vibanda vya barabarani, ili kurahisisha upatikanaji wake vijijini.

Anasema, kutokana na hali hiyo ya kimiundombinu, wafanyabiashara wa mafuta wamekuwa wakisita kujenga vituo vya mafuta maeneo ya vijijini na matokeo yake kujikita katika miji mikubwa, barabara kuu na miji midogo inayokuwa kibiashara.

Mkazi wa Mwitikira, katika Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma, Manzije Mazengo, anasema hali ya upatikanaji mafuta ni changamoto kwao na wanategemea wafanyabiashara wenye maduka ya vijijini hapo kusafirisha bidhaa hiyo, kutoka jijini Dodoma.

“Hapa unaweza kuishiwa mafuta ya taa, ukasubiri hadi jioni ndio upate, maana wanaouza wanafuata Dodoma mjini na hadi kufika huku ni jioni kabisa giza limeshaingia kwa kuwa magari yanayofanya safari za huku, yanaondoka Dodoma mjini saa nane mchana. Kwa kweli ni changamoto,”anaeleza.

Pia, anasema mafuta yanayotunzwa kwenye madumu kwenye makazi au sehemu za kawaida za biashara na pindi inapotokea moto yanachangia mazingira ya madhara kwa maisha ya watu na mali zao.

VITUO TEMBEZI
Kutokana na kuwapo mazingira hatarishi kwa sababu ya utunzaji na uhifadhi wa mafuta usiozingatia vigezo na masharti, Ewura, imekuwa ikibuni mbinu mbalimbali kuhakikisha nishati hiyo inapatikana vijijini kwa usalama.

Kwa sasa, Ewura inaanzisha utaratibu wa vituo tembezi ili kurahisisha upatikanaji huduma, kutokana na mahitaji yake kuongezeka kwa kushamiri kwa usafiri wa pikipiki maarufu kama bodaboda ambao ndio usafiri wa haraka kwa maeneo mengi.

Akizungumza kwenye semina ya waandishi wa habari mjini Dodoma hivi karibuni, Mkuu wa Kitengo ya Mawasiliano na Uhusiano, Titus Kaguo, anasema Ewura imeibua mkakati mpya wa kuanzisha vituo vya mafuta vinavyotembea, (mobile fuel system) kwa kutumia magari maalumu, yaliyotengenezwa ajili ya kazi hiyo.

Kaguo anasema ni mpango unaolenga kurahisisha upatikanaji mafuta katika maeneo mbalimbali nchini, yakiwamo ya vijijini.

“Nishati ya mafuta inatakiwa kuuzwa kwa utaratibu unaokubalika na kwa kuwa kujenga visima vikubwa ni gharama, njia hiyo ni bora na itakuwa ni rahisi kuwafikia wateja walio wengi,” anasema Kaguo.

Anasema, katika maeneo mengi nchini wafanyabiashara wadogo wamekuwa wakisafirisha na kuuza mafuta kwa njia ambazo si sahihi na zinazohatarisha usalama wa vyombo vya watumiaji na maisha yao wenyewe.

Kaguo anafafanua kwamba, watu hivi sasa wanatakiwa kufahamu kuwa kusafirisha kuuza mafuta kwa njia zisizo rasmi kwa kutumia madumu, ni kosa kisheria na hatari kubwa inayoweza kusababisha majanga kama milipiko ya moto.

“Kutokana na ongezeko la vyombo vya usafiri kama pikipiki, tumeamua kupunguza gharama za kuanzisha vituo vya uuzaji mafuta ili viweze kujengwa katika maeneo mbalimbali hasa vijijini ili kuepuka uuzaji mafuta katika vidumu,” anasema.

Anaongeza: “Kwa sasa tunakuja na vituo vya mafuta vinavyotembea ambavyo vitatoa huduma vijijini, kwa mfano mtu anakuwa na gari ndogo, unaweka tenki ambalo litakuwa limepimwa halina ‘risk’ au pikipiki za Guta mtu anabeba lita 50 anapita njia labda ya Mtera (Dodoma- Iringa) anakuuzia pikipiki itasaidia ‘gap’ (pengo) la kutokuwa na vituo vijijini.”

Anaeleza kwamba, Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM), hivi sasa kinafanyia utafiti wa suala hilo na lipo katika hatua za juu, hivi karibuni watatoa taarifa ya kuanza kwa biashara hiyo.

“Tuna imani itapunguza ‘risk’ (hatari) za watu kujenga vituo vikubwa kwenye vijiji.Usafirishaji mafuta kwenye madumu ni ‘risk’ sana hatuwezi kuruhusu vitu vya aina hii kutokana na uhaba wa vituo,”anasema.

Aidha, Kaguo anasema kuna mfumo wa ujenzi wa vituo vya vijijini, kwa lengo la kumsaidia mtu asiye na uwezo wa kujenga kituo kikubwa, ili aweze kujenga kidogo kinachogharimu si zaidi ya Sh. milioni 50.

“Kujenga kituo ni gharama. Kituo kikubwa kama pale Dar es salaam, unaweza kukuta kati ya Sh. milioni 800 hadi Sh. bilioni moja.

“Ndio maana tumekuja na mfumo unaoendana vijijini, kwa mfano kituo cha pampu moja ambacho kina uwezo wa kuwa na lita za mafuta laki moja. Huwezi kuweka lita milioni mbili wakati wewe unauzia pikipiki ambazo zinatumia lita 12,” anasema.

TAHADHARI MAGARI

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Nzinyangwa Mchany, anatoa tahadhari mbalimbali muhimu kuhusu matumizi ya mafuta, ikiwamo magari ya kubebea mafuta ama kutoegeshwa au kulazwa pasipohusika.

Badala yake anashauri yawekwe sehemu maalumu ilizotengwa, huku akitaja tahadhari nyingine ni kuwa shughuli zote zinazohusu mafuta ya petrol, ni lazima zifanyike kwa umakini na uangalifu mkubwa, kuepuka madhara yanayoweza kutokea.

Anasema ni muhimu kuzingatia na kufuata sheria, kanuni, viwango vya ubora na masharti ya leseni wakati wote, huku kukizingatiwa utunzaji, usafirishaji na utumiaji na uuzaji wa bidhaa za petroli.

Habari Kubwa