Fahamu ilikuwaje jiwe Bismarck kuwa kitambulisho Jiji la Mwanza

04May 2021
Christina Mwakangale
Dar es Salaam
Nipashe
Fahamu ilikuwaje jiwe Bismarck kuwa kitambulisho Jiji la Mwanza

UTAMBULISHO wa Jiji la Mwanza kwa wageni na wenyeji ni jiwe la Bismarck, lililopo ndani ya Ziwa Victoria eneo la bustani ya Kamanga Feri.

Jiwe la Bismarck linaloelea kwenye maji ya Ziwa Victoria ni kivutio kikubwa katika Jiji la Mwanza. PICHA: MTANDAO

Mwamba huo ulipewa jina la Mjerumani kwa vile inadaiwa alikuwa mtu wa kwanza (mgeni, Mzungu) kuliona jabali hilo na kulishangaa, huyu alikuwa Otto Von Bismarck, ambaye baadaye alikuwa Kansela wa Ujerumani.

Baada ya kuondoka Mwanza jiwe hilo lililochomoza juu ya maji ya Ziwa Victoria, lilipewa jina lake. Yote hayo yalitokea wakati wa utawala wa Kijerumani takribani miaka 137 iliyopita.

Akizungumza na Nipashe, wakati alipotembelea Mwanza baharia Thomas James, anasema maajabu ya jiwe hili ni pamoja na kuzungukwa na maji, lakini ndani kuna pango lenye ukubwa kama chumba cha kuishi.

Maajabu yanazidi kwa kuangalia namna lilivyokaa ni la kipekee kutokana na jinsi mawe yalivyobebana yanaonekana kama vile yatadondoka, lakini kwa karne nyingi hayajatikisika.

Anasema jiwe la Bismarck ni kati ya chanzo cha mapato kwa mkoa huo. Fedha zinazokusanywa zinatoka kwa watalii wa ndani na nje wanaolizuru eneo hilo huku Ziwa Victoria lililo mama wa jiwe hilo likizalisha kitoweo mujarabu cha samaki wakiwamo sangara, sato na dagaa.

Historia ya jiwe na jina au mwamba huu uliopo ndani ya ziwa hili, liliopo jirani na bustani ya Kamanga Feri ni eneo ambalo hufikiwa na wageni kutoka jijini humo lakini hasa mikoa tofauti achilia mbali watalii kutoka mataifa tofauti.

JIWE LENYEWE

Mwamba huo unaelezewa kwa namna mbalimbali na wakazi wanaoishi jirani na ufukwe wa Ziwa Victoria ambalo ni ziwa kubwa barani Afrika na chanzo cha Mto Nile.

Baharia Thomas James, anayeishi jirani na mwalo anasema: “Ni sehemu ambayo inavutia wageni wanaofika Mwanza. Zaidi tunapokea watalii kutoka nchi tofauti kama Ujerumani na Uingereza. Ninawaongoza nawatembeza katika jiwe hili na maeneo jirani kwa kutumia boti.”

Baharia huyo, ambaye ana uzoefu wa takribani miaka 20 katika kufanya shughuli hiyo Ziwa Victoria anasema jiwe hilo awali lilikuwa makazi ya aliyekuwa mtemi wa Wasukuma miaka takribani 100 iliyopita, aliyeitwa Mwanamalundi, ambaye aliongeza zaidi umaarufu wa jiwe hilo.

Kuhusu wanaotembelea eneo hilo, kiimani James anasema, jiwe la Bismarck ni sehemu ya utamaduni wa wenyeji na wengi hufika kutambika kulingana na kile wanachoamini.

“Chifu Mwanamalundi katika jiwe hili aliishi baada ya wakoloni kumtafuta akikimbilia kujificha hapa, ameacha alama za nyayo zake juu ya jiwe hili. Ndani ya pango hili alifanya malazi, kuna jiwe kama kitanda kwa ndani, ambako maji hayaingii hata siku moja wala mvua haifiki,” anasema baharia James.

Anaeleza kuwa kutokana na uelewa mdogo kuhusu kuhifadhi maeneo ya kihistoria baadhi ya wakazi hufika eneo hilo wanakwangua sehemu ya unyayo na kwenda kufanyia shughuli mbalimbali zikiwapo ibada na matambiko.

“Pale juu ya jiwe kuna mikuki ambayo aliichomeka siku nyingi. Tumeikuta na tunaamini hivyo, inabidi tupatunze kwa ajili ya utalii kwa kuwa inatuingizia kipato na kuupa umaarufu mkoa wa Mwanza,” anabainisha mwongoza watalii huyo.

FURSA YA AJIRA

Kuhusu namna jiwe hilo kuwa sehemu ya utalii na chanzo cha mapato, anasema ili kufika eneo lililopo jiwe la Bismarck, watalii hulipia fedha ili kufikishwa hapo.

Anabainisha kwamba kabla ya kupanda boti ya kukodi, watalii hutoa kiingilio cha Sh. 1,000 kuingia kwenye geti la bustani ya Kamanga ambayo inasimamiwa na Halmashauri ya Mwanza.

Kadhalika anasema fedha hizo ni maalumu kwa ajili ya kutunza bustani, iliyopo chini ya halmashauri ya manispaa hiyo na kwamba mtunza bustani ana jukumu la kuweka mazingira ya eneo hilo katika hali ya usafi kila wakati.

Anasema kwa watalii ambao wanahitaji kutembezwa maeneo tofauti yaliyo jirani na jiwe hilo, wanatozwa Dola 100 au Shilingi 230,000 kwa saa moja mpaka saa 1.30, kwa kutumia usafiri wa boti ya kukodi kulifikia jiwe la Bismarck lililo umbali wa takribani mita 200 kutoka bustani hiyo.

“Wageni wa ndani ya nchi wanalipia Sh. 10,000 kwa mtu mmoja kwenda kutembezwa na boti kwenye maeneo tofauti yaliyo jirani na jiwe la Bismarck,” anaeleza, James.

Jessica Masanja ambaye anafanya shughuli za kuuza samaki sokoni anasema eneo hilo ni makumbusho ambayo yanahitaji kuhifadhiwa.

Anasema historia ambayo ameikuta na kupata simulizi ndani ya jiwe hilo inasemekana mtemi Mwanamalundi aliishi miaka mingi na kupata huduma za kibinadamu za kila siku ikiwamo kujipikia ndani ya pango hilo.

HISTORIA JINA BISMARCK

Kansela Otto von Bismarck, kwa mujibu wa mtandao alizaliwa Aprili 1, 1815 na kufariki Julai 30, 1898 na kwamba alikuwa mwanasiasa mashuhuri wa Ujerumani katika karne ya 19 na kuwa Waziri Mkuu wa Prussia.

Inaelezwa kuwa alijenga Umoja wa Wajerumani katika vita tatu dhidi ya Denmark ya mwaka 1864, Austria 1866 na Ufaransa iliyoanza 1870 hadi 71.

Kama Kansela wa Dola la Ujerumani aliongoza siasa ya nchi hadi 1890 alipoondolewa ikulu na Kaisari kijana Wilhelm wa II.

MTEMI WA WASUKUMA

Mwanamalundi alikuwa mcheza ngoma mashuhuri kutoka kabila la Wasukuma ambaye alipewa jina hilo kama utani likimaanisha miguu myembamba na mirefu, alizaliwa katika Kijiji cha Mwakubunga Nera katika Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza mwaka 1846.

Umahiri wake wa kucheza ngoma mara nyingi alifuatwa na kundi la watoto kwa sababu ili kumshuhudia. Wazazi wake hawakufurahia hilo, kutokana na kwamba watoto ambao waliwategemea katika kupeleka mifugo machungani,
waliitelekeza mifugo na kumfuata Mwanamalundi na kusababisha kupotea kwa watoto na mifugo yao.

Habari Kubwa