Fahamu mamlaka upekuzi

16Apr 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Fahamu mamlaka upekuzi

UPEKUZI ni kitendo cha kuingia aidha maungoni kwa mtu, ndani ya nyumba au kwenye makazi ya mtu kwa nia ya kutafuta kitu, vitu vilivyofichwa au vitu ambavyo vinahusiana na kosa la jinai.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro.PICHA: MTANDAO

Kwamba kitu au vitu hivyo vinaweza kusaidia katika upelelezi wa Polisi, au katika kesi inayoendelea mahakamani kama sehemu ya ushahidi wa kuthibitisha au kukanusha kosa linalojadiliwa.

Upekuzi unaweza kufanyika kwa namna mbili kwa kutumia hati ya upekuzi au Upekuzi unaofanyika bila hati ya upekuzi kulingana na mazingira husika.

Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kifungu cha 24 kinampa mamlaka na uwezo Ofisa wa Polisi kufanya upekuzi maungoni mwa mtu yeyote aliyemkamata na upekuzi huo unafanyika mara baada ya mtu kukamatwa na kuwa chini ya ulinzi.

Sheria hiyo pia, inampa uwezo wa kuchukua toka maungoni mwa mtu huyo kitu chochote cha hatari au kitakachosaidia upelelezi wa tuhuma zilizosababisha kukamatwa.

Aidha, sheria hiyo imetoa umuhimu wa kipekee kwa wanawake pale tendo la upekuzi linapotakiwa kufanyika dhidi yake. Aidha iwe maungoni au hata kwenye makazi yake.

Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kifungu cha 26 kinatoa ufafanuzi wa jinsi mwanamke atakavyopekuliwa, kwamba upekuzi huo lazima ufanywe na Polisi Mwanamke au mwanamke yoyote ambaye anaaminika.

MAMBO YA KUZINGATIWA

Mambo muhimu ya kuzingatiwa katika upekuzi, kulingana na unyeti wa tendo la Upekuzi, ni vyema kabla na baada ya upekuzi kufanyika Ofisa wa Polisi au mtu mwingine anayefanya upekuzi akawa na mashahidi wa kushuhudia upekuzi huo.

Ni haki ya msingi kwa mmiliki wa nyumba, jengo au eneo linalotakiwa kupekuliwa kuonyeshwa na kuona hati inayoidhinisha upekuzi, pia ni muhimu mashahidi waione hati hiyo kabla ya utaratibu wa upekuzi kuanza.

Aidha, jamii na wananchi kwa ujumla wana haki ya kutambua Mamlaka zilizopewa uwezo wa kuidhinisha upekuzi, ambazo ni Mkuu wa Kituo cha Polisi na Hakimu.

Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, inampa uwezo na mamlaka ofisa wa Polisi ambaye ni Mkuu wa Kituo cha Polisi (OCS) anapokuwa amepokea taarifa za kuaminika kwamba ndani ya nyumba, jengo au eneo fulani au kwenye chombo cha usafiri kuna vitu ambavyo anavitilia shaka ambavyo kwa sababu ya msingi vinasadikiwa kutumika kutenda kosa.

Mkuu wa Kituo anaweza kuidhinisha upekuzi kama anaamini kwamba ucheleweshaji wowote wa kufanyika upekuzi unaweza kusababisha utoroshwaji au uharibifu wa kitu au vitu vinavyotafutwa au vinaweza kuhatarisha maisha ya binadamu au mali.

Kwa upande wa Hakimu naye ana uwezo na mamlaka ya kuamuru upekuzi ufanyike kwenye nyumba, jengo au eneo lolote baada ya kupokea malalamiko au taarifa za kuaminika kwamba kwenye nyumba, jengo au eneo fulani kuna kitu au vitu visivyo halali au vielelezo muhimu.

Amri hii hutolewa kwa maandishi na hujulikana kama hati ya upekuzi. Pia kifungu cha 43 cha sheria ya mwenendo wa Makosa ya Jinai kinampa uwezo Ofisa wa Polisi kuvunja na kuingia kwenye nyumba au jengo au mahali popote kwa madhumuni ya kufanya upekuzi, iwapo patakuwa pamefungwa na mmiliki anakataa kutoa idhini baada ya kuonyeshwa hati ya kuamuru upekuzi ufanyike.

Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai inampa uwezo Ofisa wa Polisi kufanya upekuzi kwa dharura kwenye nyumba, jengo au mahali popote endapo anazo sababu za msingi za kutaka kufanya upekuzi wa dharura.

Upekuzi wa dharura ufanyika bila hati ya kuidhinisha upekuzi yaani search order au search warrant. Upekuzi huu hufanyika baada ya mazingira kulazimu uharaka na kwamba kutokufanya hivyo kutasababisha uharibifu au utoroshwaji au kitu au vitu au mtu anayetafutwa kuhusiana na shaka au tuhuma.

Ni vizuri jamii ikaelewa kuwa, Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai haitamki saa ya kufanya upekuzi, ila inasema upekuzi utafanyika kuanzia mawio hadi machweo ya jua na chini ya kifungu cha 42 upekuzi unaweza kufanyika hata usiku.

Imetolewa na Kitengo cha Uhusiano Polisi Makao makuu Dar es salaam.

Habari Kubwa