Fahamu umuhimu wa hati ya tabia njema (Police Clearance Certificate)

14May 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Fahamu umuhimu wa hati ya tabia njema (Police Clearance Certificate)

NI Cheti/Hati ya uthibitisho ambayo hutolewa na Jeshi la Polisi ikithibitisha kuwa mtu aliyepewa hati hiyo hajawahi kutiwa hatiani na Mahakama kwa makosa ya jinai.

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) nchini, Robert Boaz. PICHA: MTANDAO

MATUMIZI YAKE

Hati ya Tabia Njema hutumika kwa shughuli mbalimbali za uthibitisho kama ifuatavyo:-

Kuomba VISA katika Balozi mbalimbali za nchi za nje  zilizopo hapa nchini kwa ajili ya mtu kusafiri kwenda katika nchi hizo kikazi, kimasomo, kibiashara au vinginevyo.

Pili, kuomba ajira ndani ya nchi au nje ya nchi.

Lakini kusajili kampuni na kumiliki bunduki.

Vilevile kuomba uraia wa Tanzania pamoja na Taasisi au mwajiri kumchunguza mtumishi wake.

Aidha, kuomba kibali cha ukaazi katika nchi ya kigeni (Residence permit).

Pia kuomba kibali cha kufanya kazi nchi ya kigeni (work permit) na hatimaye kuomba kibali cha kusoma nchi ya kigeni (study permit).

 

KIGEZO CHA KUPEWA

HATI YA TABIA NJEMA

Ili mtu aweze kupewa Hati ya Tabia Njema, inampasa kufika Forensic Bureau Makao Makuu Dar es salaam, kwa ajili ya kuchukuliwa alama za vidole ambazo zitachunguzwa kitaalamu ili kutambua kama alishawahi kutiwa hatiani au hapana.

 

Pia, mbali na Makao Makuu kwa watu walioko mikoani wanaweza kufika katika ofisi za wakuu wa Upelelezi wa Mikoa au Ofisi za Polisi za Wilaya waliko kwa ajili ya kuchukuliwa alama za vidole ambazo zitatumwa Forensic Bureau Makao Makuu kwa ajili ya uchunguzi na utolewaji wa Hati ya Tabia Njema ambayo itatumwa kwa mhusika aliyeomba hati hiyo.

 

UMUHIMU WA HATI

 YA TABIA NJEMA

 

Katika dunia ya leo yenye shughuli nyingi na mwingiliano mpana na ulio wazi kwa kiasi kikubwa kati ya watu wa mataifa mbalimbali, hakuna nchi ambayo ingependa kupokea mtu ambaye haeleweki au mtu mwenye historia mbaya ya uhalifu.

 

Halikadhalika, hakuna kampuni au taasisi yeyote ambayo ingependa kumwajiri au kumpa jukumu lolote mtu ambaye ana historia chafu ya kiuhalifu.

 

Nchi na kampuni au Taasisi mbalimbali zinahitaji watu wenye tabia na mwenendo mwema katika maisha ambao hawawezi kuwa chanzo cha matatizo katika nchi au taasisi zao.

 

Hivyo, ni jukumu la kila mtu kujitunza na kutojihusisha na uhalifu wa aina yoyote ili asije akakosa huduma hii muhimu kwa sasa ambayo ukiikosa ni dhahiri unaweza kushindwa kufikia malengo.

 

Hayo yaweza kuwa ni ya kielimu, ajira, biashara, safari za kikazi, kibiashara, kiutalii, kusajili kampuni n.k.

 

MAMLAKA YA KUTOA

HATI YA TABIA NJEMA

Hati ya Tabia Njema hutolewa na Jeshi la Polisi kupitia kurugenzi ya Forensic Bureau ambayo ni Taasisi ya Uchunguzi wa kisayansi ndani ya Jeshi la Polisi.

 

Mojawapo ya huduma muhimu zinazotolewa na Taasisi hii ni Hati ya Tabia Njema (Police Clearance Certificate) ambayo kwa kiasi kikubwa ni kwa matumizi ya kiraia.

 

VIAMBATANISHO MUHIMU KATIKA MAOMBI YA HATI YA TABIA NJEMA

Pamoja na alama za vidole, viambatanisho muhimu katika maombi ya Hati ya Tabia Njema baadhi vinatofautiana kulingana na sababu ambayo mtu au Taasisi inaombea Hati ya Tabia Njema kama ifuatavyo:-

 

VISA YA MASOMO NJE YA NCHI

Kunahitajika Nakala ya hati ya kusafiria, Nakala ya barua ya kukubaliwa chuo (ADMISION LETTER).

Pia Picha Passport size 1 na Barua ya maombi.

 

VISA YA MAKAZI/KUFANYA KAZI NJE.

Kunahitajika Nakala ya hati ya kusafiria na Picha Passport size 1.

 

Aidha, Barua ya maombi na Nakala ya mkataba wa kazi.

 

URAIA WA TANZANIA.

Kunahitajika Barua kutoka ofisi ya uhamiaji, Nakala ya Hati ya kusafiria na Picha passport size 1.

 

MAOMBI YA KAZI/AJIRA NDANI YA NCHI

 

Kunahitajika Barua ya ofisi anayotarajia kuajiriwa k.m Benki, Kampuni za ulinzi n.k.

 

Nakala ya kitambulisho cha mhusika na Picha passport size moja pamoja na Barua ya maombi kama mhusika hatoki kwenye Taasisi.

 

MAOMBI YA HATI YA TABIA NJEMA KWA WAGENI WALIO NJE YA NCHI.

 

Kunahitajika Nakala ya Hati ya kusafiria na Picha passport size 1.

 

Lakini Alama za vidole zilizochukuliwa kutoka Kituo chochote cha Polisi katika nchi ambapo mhusika anaishi na Barua ya maombi.

 

Imetolewa na:

Ofisi ya uhusiano

Makao Makuu ya Jeshi la Polisi

Dar es Salaam.

[email protected]