Familia maskini zawezesha watoto, wachangamkia shule Zanzibar

27Jun 2017
Rahma Suleiman
Zanzibar 
Nipashe
Familia maskini zawezesha watoto, wachangamkia shule Zanzibar

KUNA msemo usemao kuwa mgeni njoo, mwenyeji apone umejidhihirisha katika Shule ya Msingi Kizimbani, kutokana na utekelezaji wa Mradi wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) kufika shuleni hapo na kuchangia kuboresha sekta ya elimu. 

Shule hiyo, yenye wanafunzi wapatao 500 kwa muda mrefu ilikuwa inakabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwamo mahudhurio duni ya wanafunzi, ufahamu mdogo wa masomo na ushirikiano mdogo kati ya wazazi na walimu shuleni hapo. 

Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Issa Kefa Barthazar anasema, baada ya Tasaf kuanza kutatua kero mbalimbali umewezesha kupunguza baadhi ya changamoto shuleni hapo zilizokuwa kero kubwa kwa muda mrefu. 

Hali halisi ilivyokuwa ni kwamba, mahudhurio ya wanafunzi wa shule hiyo yalikuwa duni kwa wakati huo, hivyo kukosa masomo kikamilifu na kujikuta wana ufahamu mdogo na kiwango cha chini cha ufaulu. 

“Ilifika hatua shuleni hapa, mwanafunzi yupo darasa la tano, lakini hajui kusoma wala kuandika. Lakini tangu mradi wa Tasaf uanze utekelezaji wake wanafunzi wamekuwa na muamko wa kuhudhuria shule na kusoma kwa bidii,”anafafanua. 

Ukweli ni kwamba, hali kwa sasa iko tofauti na awali kabla ya mradi wa Tasaf haujaanza utekelezaji. Utoro wa wanafunzi unakadiriwa kufikia asilimia 80, lakini sasa kiwango hicho kimeshuka na kufikia asilimia 30. 

Miongoni mwa sababu zilizokuwa zikichangia utoro wa wanafunzi ni hali ya umasikini katika ngazi ya familia, hata watoto kujikuta wakitumbukia katika ajira za utotoni ikiwamo kutembeza watalii. 

Eneo la kijiji hicho cha Kizimbani ni ukanda wa utalii na kilimo cha viungo (spice) hivyo watalii hufika kwa wingi kjijijini hapo, hata kuwafanya watoto kushawishika kufanya kazi za kuwahudumia watalii ili wapate mapato kwa ajili ya wao kujikimu pamoja na familia zao. 

Issa anasema, wanafunzi hutumia mwanya huo kuwatembeza watalii katika mashamba ya miti ya viungo (spice) kwa lengo la kujipatia fedha. 

Kama hiyo haitoshi, wanafunzi pia hutoroka shule na kwenda kufanya shughuli za biashara ikiwamo kutengeneza vifungashio vya kuwekea viungo(spice) kama mdalasini, hiliki, karafuu, kungumanga na vyenginevyo. Vifungashio hivyo hutengenezwa kwa njia za kiasili ikiwamo majani ya minazi, kili na vifuu. 

“Pia wanafunzi hukimbia masomo na kwenda mitaani kutengeneza mapambo yanayotumia zana za kiasili kwa ajili ya kuwauzia watalii wanaofika kijijini hapo,” anabainisha. 

Tasaf kwa mujibu wa Mwalimu huyo, baada ya kugundua hali hiyo mbaya kwa wanafunzi, kutokana na umaskini ambao baadhi yao walikuwa wanahudhuria shule wakiwa hawana viatu, kuvaa sare za shule zilizochakaa na mazingira wanayoishi wanafunzi hayakuwa ya kuridhisha. 

Tasaf kwa kushirikiana na uongozi wa shule pamoja na uongozi wa Shehia ya Kizimbani, wanafunzi na wazazi walikutana na kujadili namna gani tatizo la umaskini litaondoka au kupungua. 

Baada ya tafakuri ya kina kwa kutafuta ufumbuzi halisi, jitihada hizo zimefanikiwa kuzaa matunda kwa wanafunzi kuhudhuria Shule kwa wingi wakiwa wamevaa sare nzuri ya shule ambazo ni safi na viatu. 

Kilichofanyika kwa mujibu wa Mwalimu huyo ni Tasaf kutoa elimu kwa familia za wanafunzi wa shule hiyo wanaoishi katika mazingira magumu ya umaskini na kuwawezesha kupatiwa kiwango cha fedha ili wabuni miradi mbalimbali ya maendeleo na fedha ya kujikimu kimaisha. 

Kufutia juhudi hizo, anasema zimewezesha kutekelezwa kwa ushirikiano kati ya wazazi wa wanafunzi na walimu shuleni hapo kwa kufuatilia nyendo na mahudhurio ya watoto wao. 

“Kwa sasa, wazazi na walezi wenyewe muda wa masomo wanafika shueni kutaka kujua mahudhurio ya watoto wao na unapomueleza mtoto wake kuwa amehudhuria shule huwa haridhiki hivyo anakwenda hadi darasani kuhakikisha kama ni kweli yupo,” anasema. 

Anaongeza “hata ufahamu wa wanafunzi umekuwa mzuri kwa sasa, kwani wanajua kusoma na kuandika huku baadhi yao wanajiandaa kwa mitihani ya taifa ya darasa la sita ikiwa ni maandalizi ya kuingia sekondari”. 

Ingawa suala la utoro kwa wanafunzi umepungua, anasema, lakini bado upo kwa kiwango kidogo ambacho kimsingi hakiathiri maendeleo ya masomo. 

Pamoja na mafanikio yaliyopatikana kupitia mradi wa Tasaf, bado shule hiyo inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa madawati hivyo kuwafanya baadhi ya wanafunzi kukaa sakafuni. 

Anasema, shuleni hapo kuna upungufu wa madawati 100 ili wanafunzi wote darasani kuwawezesha kukaa kwenye madawati kuanzia ngazi ya maandalizi hadi msingi. 

Changamoto nyingine anayoitaja ni mahitaji ya majengo mapya ya madarasa kwa ajili ya sekondari ili wanafunzi wanapohitimu elimu ya msingi, kwa sasa hulazimika kupangiwa shule nyingine za sekondari zilizopo umbali mrefu toka hapo. 

Umuhimu wa kuwapo shule ya sekondari kijijini hapo ni kwamba kutawapunguzia kero wanafunzi wanaotembea umbali mrefu kuyafuata masomo, hivyo kuchangia kuwafanya washindwe kuendelea na elimu ya sekondari. 

Pia wanahitaji uzio shuleni kwao ili kuweza kuwadhibiti wanafunzi wanapokuwa shuleni hapo kisha kuondoka hadi muda mwafaka uliowekwa. 

“Ukosefu wa uzio shuleni unatoa mwanya kwa wanafunzi kuingia na kutoka muda wanaotaka wao badala ya muda muwafaka uliowekwa na shule,” anasema. 

Mkazi wa kijiji hicho cha Kizimbani aitwaye Subira Mohammed, ambae amenufaika na Tasaf, anasema kuwa, mradi huo umemwezesha kupata fedha kila muda uliopangwa ambazo zimemsaidia kununua mahitaji ya shule ya mtoto wake. 

Licha ya fedha hizo anazopatiwa kumwezesha kumnunulia vifaa vya shule mtoto wake pia zinamfanya amudu kununua chakula ili mtoto wake anaporudi toka shule ale chakula kwa muda mwafaka.

“Mradi wa Tasaf umenisaidia sana mwanzoni nilipoanza kuwa mlengwa wake nilikuwa napata Shilingi 70,000 zilizonisaidia katika kujikomboa kiuchumi,”anasema.

Kwa sasa anasema kuwa bado, anaendelea kupokea ruzuku ya fedha ya Tasaf ingawa kiwango hicho kimepungua, lakini ana ushukuru sana ufadhili wa taasisi hiyo kwa msaada huo. 

“Mtoto anaporudi shule na kukuta chakula tayari, unamjengea mazingira mazuri na kumuepusha kushawishika kwa ajira za utotoni,”anasema. 

Anabainisha kuwa yeye ni miongoni mwa wazazi ambao watoto wao walikuwa wanatoroka shule na kwenda kufanya biashara mbalimbali lengo likiwa ni kujipatia fedha za kujikimu. 

Hatua za pamoja za Tasaf, shule na Shehia zimekuwa ni msaada mkubwa kwake na sasa mtoto wake ambae yupo darasa la sita anaendelea vyema na masomo. 

Kaimu wa Shehia hiyo ya Kizimbani (Kiongozi wa kijiji ) Mariyam Suleiman, anasema amefarijika sana baada ya kushuhudia mahudhurio mazuri ya wanafunzi katika shule ya Kizimbani. 

Mahudhurio hayo yametokana na ushirikiano mzuri uliopo katika ya uongozi wa mradi wa Tasaf, walimu na wananchi wa kijiji hicho, baada ya kufahamu umuhimu wa elimu kwa watoto. 

Kiongozi huyo anasema, matarajio yake kuwa, mafanikio hayo yatazidi kuendelea ili kuhakikisha kuwa watoto wanapata elimu inayostahiki ambayo ndio msingi wa maendeleo. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania, Ladislas Mwamanga anasema kuwa, mradi wa Tasaf awamu ya tatu ni mpango wa kitaifa unatekelezwa Tanzania Bara na Zanzibar. 

Mpango huo anasema umezinduliwa rasmi na rais mstaafu wa awamu ya nne wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete kwa lengo kuu la kuziwezesha kaya maskini kuondokana na umaskini uliokithiri na kuongeza kipato. 

Uwezeshaji kaya maskini kifursa na kiuwezo kwa kugharamia mahitaji ya msingi ya kimaisha yanayojumuisha chakula, elimu na afya. 

Mkurugenzi huyo anasema kuwa upo ushahidi wa fedha zinazotolewa na Tasaf kutumika katika utaratibu maalum uliowekwa. 

Mojawapo ya matumizi ya fedha hizo ni ujenzi wa nyumba za kudumu, upatikanaji wa sare za shule kwa wanafunzi, uanzishwaji wa vitalu vya miti ya kudumu na ujenzi wa majengo ya shule ambayo ni mfano wa matumizi hayo sahihi ya fedha hizo. 

Benki ya Dunia kupitia washirika wake wa Maendeleo wamekuwa wakitoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa Tasaf, imeridhishwa na hatua kubwa iliyochukuliwa na wananchi wa Zanzibar  katika kusimamia miradi yao kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (Tasaf) awamu ya tatu. 

Viongozi wa ujumbe wa Benki hiyo ulitoa tathmini ndogo, baada ya kumaliza ziara yao visiwani Zanzibar ili kukagua miradi ya Tasaf katika maeneo mbalimbali. 

Kiongozi wa Ujumbe huo kutoka Benki ya Dunia, Moderes Abdullah, anasema ujumbe wao umeshuhudia maendeleo makubwa yaliyopatikana katika Jamii kwa kundi kubwa la wananchi kuamua kutekeleza kwa ufanisi mkubwa miradi waliyoianzisha. 

Moderes anasema Zanzibar imeonyesha mfano bora katika uendelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia (Tasaf ) awamu ya tatu kiasi kwamba, uongozi wa Benki ya Dunia kupitia washirika wake umefurahia hatua hiyo ya mafanikio. 

Benki ya Dunia na washirika wake inaunga mkono miradi ya Maendeleo kwa wananchi maskini katika nchi zinazoendelea ikilenga kuona ufanisi wa kudumu unapatikana katika kustawisha maisha yao ya kila siku. 

Habari Kubwa