Fenicha nyeupe zinaifanya nyumba iwe ng’aring’ari

18Jun 2016
Vivian Machange
Nipashe
Fenicha nyeupe zinaifanya nyumba iwe ng’aring’ari

HEBU fikiria muonekano wa ndani ya nyumba utavutiaje unapoamua kupendezesha maeneo ya wazi kwa fenicha nyeupe!Sehemu za wazi ndani ya nyumba ninazozingumzia ni zile ambazo mgeni au mwenyeji anaweza kuingia nazo ni pamoja na sebuleni, jikoni na chooni.

Wengi wanapenda kubadili mionekano ya ndani ya nyumba zao ambapo mabadiliko hayo lengo lake ni kuboresha ili kupendeze na kuwe kupya na kuonekane kwa kisasa zaidi.

Fikiria makabati haya yatakavyomvutia mwenyeji na mgeni yakiwa meupe. Kwanza kabati la runinga, la vyombo, shelfu za vitabu, meza ya kahawa na hata makabati ya jikoni, ni lazima kutishe kwa mvuto kwasababu rangi nyeupe haipitwi na wakati.

Muulize mbunifu wa ndani yeyote atakuambia kuwa nyeupe ni chaguo sahihi kwa chumba chochote ndani ya nyumba.
Fenicha nyeupe zinaleta hisia ya usafi, zinafanya chumba kionekane kikubwa , tena king’are kutokana na mwanga wa kutosha. Hii inasaidia sana hasa kwa vyumba vidogo ambavyo kuwa na rangi za giza kunavifanya vionekane vidogo zaidi.

Hebu tuliza fikra zako kwenye uzuri wa kabati la runinga jeupe halafu ndani ipo televisheni nyeusi. Wote tunajua namna nyeupe na nyeusi zinavyopendeza pamoja. Kabati hili jeupe pamoja na mashelfu havikosei kwani vinaendana na rangi nyingi zozote za vitu ulivyo navyo sebuleni.

Au kabati la vyombo jeupe kwenye chumba cha chakula huku ukiwa umetandaza sahani zako za rangi, maua na michoro mbalimbali kwenye zile shelfu za wazi.

Tafiti miundo mbalimbali ya makabati meupe ya runinga au vyombo na uwe mbunifu wa jinsi ya kuboresha ndani mwako.Makabati ya runinga ambayo yanakuja na mashelfu yanaweza kutumiwa kupata eneo la kutandaza picha za familia, sanaa na vitabu.

Pia zinakuwa na droo za kufunga kwa kuhifadhia vile vitu usivyopenda vionekane wazi. Hakika kabati jeupe la runinga linaweza kuvutia sana. Chaguo ni lako wewe unayetaka kupendezesha nyumba yako.

Mashelfu meupe yawe ni ya vitabu au ni yale madogo ya kutundikwa ukutani kwa ajili ya kuwekea picha, maua na vitupio mbalimbali vya kupendezesha ukuta yana mvuto wa kipekee. Shelfu nyeupe zinaposimamishwa mbele ya ukuta ambao nao una rangi ya mwanga chumba kinaleta hisia za kuvutia na kuongeza umaridadi.

Makabati meupe jikoni na kwenye bafu za kisasa ni kwa ajili ya kuhifadhia karatasi za chooni na vitu vingine vinavyohitajika na huko wakati yale ya jikoni yakihifadhia vitu vikavu ikiwa ni pamoja na vyombo na vyakula, si hivyo tu inaongeza uzuri na mvuto wa jiko.

Aina gani ya fenicha nyeupe utumie ni chaguo lako binafsi. Kutegemea na vitu ulivyonavyo iwe ni vitabu, vitupio vya mapambo, vitu vya burudani au chochote kile. Wengi mtagundua kuwa kutumia nyeupe ni chaguo zuri kwani ni rangi ya wakati wote. Na hata pale unapoamua kubadili rangi inakuwa rahisi zaidi kama rangi ya awali ni nyeupe.

Yeyote anayetaka kuwekeza kwenye fenicha za ndani rangi nyeupe ina mvuto usiopingika.Zaidi kutana na mtaalamu kwa kutembelea www.vivimachange.blogspot.com

Habari Kubwa