FFWP inavyopambana na umasikini Tanzania

23May 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
FFWP inavyopambana na umasikini Tanzania

VITA dhidi ya umasikini ni mapambano yanayohitaji nguvu kuishinda kutoka maeneo mbalimbali, kuanzia serikali, taasisi binafsi na mwananchi mmoja mmoja.

Uchangiaji wa damu ni sehemu ya kampeni inayofanywa na EEWP katika kuboresha afya ya wananchi nchini

Katika kupambana na adui umasikini, baadhi ya mashirika yamekuwa na mchango mkubwa katika kusaidia jamii kujikomboa kiuchumi.

Moja ya wadau wanaopambana kuhakikisha umasikini unatoweka hapa nchini, ni Shirika linalofahamika Familia kwa Amani ya Dunia (FFWP). Asasi hii inalenga kugusa jamii na kueneza amani duniani kuanzia kwenye hatua ya kifamilia.

FFWP imekuwa ikitoa elimu ya maadili mema kwa wanafamilia kuanzia malezi ya watoto, uhusiano kwa wanandoa na wajibu wa wazazi kwa watoto.

Pamoja na wajibu wake wa kutoa elimu kwa familia, taasisi imekuwa ikitoa misaada mbalimbali katika maeneo kadhaa.

Akizungumza wakati alipotembelea Kituo cha Habari dhidi ya Umasikini (MeCAP), Mkurugenzi wa FFWP, Stylos Simbabwene,
amesema kwamba Shirika lake limejikita kusaidia kwenye baadhi ya huduma za jamii kwa nia ya kupunguza umasikini kwa vitendo.

Simbamwene, anasema shirika lake limesaidia mradi wa uwekaji wa mfumo wa maji safi na ukarabati wa kisima cha maji katika Kituo cha Polisi Sitakishari wilayani Ilala jijini Dar es Salaam.

Lakini katika kituo hicho, FFWP wamegharamia uwekaji wa umeme katika jengo la Dawati la Jinsia ili wananchi wapate huduma bora na katika mazingira mazuri.

Vituo vingine vilivyonufaika na mradi huo ni Manzese na Kigogo Luhanga.

Anasema kwamba wamekarabati kisima cha maji katika Shule ya Msingi Mji Mpya wilayani Ilala na ukarabati wa lifti kwenye uwanja wa Taifa.

“Katika mradi huu wa kuboresha sehemu za kutolea huduma, tumejenga jengo la ofisi za serikali ya mtaa wa Msigani wilayani Ubungo, na Temeke tumechangia vifaa katika ujenzi wa ofisi ya CCM Azimio” amesema Simbamwene.

Mkurugenzi huyo anaeleza shirika hilo sio tu limetoa misaada katika Jiji la Dar es Salaam, pia wamesaidia baadhi ya miradi katika mikoa mingine.

“Tunafanya kazi zetu nchi nzima. Tumechangia ujenzi wa zahanati ya Engutoto wilayani Arumeru mkoani Arusha lakini pia uchimbaji wa visima wilayani humo”, anaongeza kusema Simbamwene.

“Katika wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro, Shirika letu limejenga zahanati, kuchimba kisima cha maji na ununuzi wa gari la wagonjwa katika kijiji cha Manza”.anazidi kufafanua

Mkurugenzi huyo anaeleza katika mkoa wa Mbeya, wamechimba kisima cha maji katika Shule ya Msingi Mwaheki na kuwezesha vikundi mbalimbali vya ujasiriamali.

Simbamwene amevitaja baadhi ya vikundi ambavyo Shirika lake limeviwezesha kuwa ni pamoja na kikundi cha ushonaji Majohe, kikundi cha kinamama Mvuti , vikundi vya Vicoba vya Kinyerezi, Kinondoni, Kigogo, Malamba Mawili na Mtoni kwa Aziz Ally, vyote vya jijini Dar es Salaam.

Amevitaja vikundi vingine kuwa ni kikundi cha Vicoba Arumeru mkoani Arusha, kikundi cha Vicoba Muungano mkoani Mbeya pamoja na mradi wa kinamama wa vyakula vya mifugo wilayani Arumeru.

“Pamoja na haya yote FFWP ni taasisi ya kwanza kuvunja rekodi ya uchangiaji wa damu nyingi zaidi katika hospitali ya taifa ya Muhimbili, Benki ya Damu na Hospitali ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI:.

Mkurugenzi huyo amesema kwamba Shirika lake limefanya kazi kubwa ya kutoa elimu ya maadili katika mikoa mbalimbali.

Ameitaja mikoa ambayo Shirika hilo limeshatoa elimu katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Mbeya, Arusha, Manyara, Singida, Pwani na Njombe.

“Katika elimu tumetoa udhamini ama ufadhili kwa viongozi wa makundi mbalimbali kuhudhuria mikutano au semina za kimaendeleo katika nchi mbalimbali” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa MeCAP, Mdoe Kiligo, amelipongeza Shirika hilo kwa kuwapunguzia wananchi wengi mzigo wa umasikini wanaokabiliana nao.

“Kwa mfano tunapoambiwa FFWP, wamechimba visima katika maeneo ambako huduma ya maji safi na salama ilikuwa tatizo, wamesaidia sio tu kuwapatia wananchi huduma hiyo, lakini pia kuokoa muda ambao wananchi hao walikuwa wanautumia kutafuta maji, ili kufanya shughuli nyingine za uzalishaji mali. Hawa ni marafiki wa kweli katika mapambano dhidi ya adui umasikini”.

Habari Kubwa