Fri-kiki 4 kali zaidi Ligi  Kuu Bara msimu huu

04Dec 2017
Adam Fungamwango
Nipashe
Fri-kiki 4 kali zaidi Ligi  Kuu Bara msimu huu

WAKATI Ligi Kuu Tanzania Bara 2017/18 imefikia raundi ya 11,  kuna mengi yaliyojitokeza ya kufurahisha na ya kujifunza.

Ni msimu ambao moja kati ya mambo yaliyojitokeza ni matumizi  mazuri ya mipira ya adhabu ndogo 'fri-kiki' (mipira iliyokufa) kwa baadhi ya wachezaji kuzitumia ipasavyo.

Kwenye miaka ya hivi karibuni, kumekuwa hakuna wachezaji wazuri wa kupiga mipira iliyokufa inayoweza kuleta hatari golini na  kusababisha mabao.

Hiyo ilikuwa zamani wakati wa kina Ahmed Amasha, Ramadhani  Lenny, Mohamed Kajole, Hamisi Gaga Fred Felix Miziro na  wengine wengi ambao walikuwa na uwezo wa kupiga 'fri-kiki' kali  zilizoweza kuzaa mabao wakati mwingine.

Lakini msimu huu kuna baadhi ya wachezaji wamejitokeza kuwa  wapigaji wazuri.

Mpaka sasa kuna 'fri-kiki' nne zilizopigwa na kuzaa mabao, zimekuwa gumzo kwa mashabiki wa soka nchini Tanzania  waliozitazama kwenye televisheni, wengine wakishuhudia uwanjani.

Imefikia wakati hadi umeanza ubishi kwenye mitandao ya kijamii ni  'frii-kiki' ipi iliyokuwa kali zaidi kuliko nyingine. Lakini ukiziangalia zote, wapigaji walitumia ufundi na hesabu za hali ya juu hadi kutumbukiza mpira ndani ya wavu.

1. Ibrahim Ajibu (Yanga vs Njombe Mji)

Frii-kiki kali ya kwanza kwenye Ligi Kuu, ilipigwa Septemba 10  kwenye Uwanja wa Sabasaba mjini Njombe wakati wa mechi kati ya wenyeji Njombe Mji dhidi ya Yanga.

Ibrahim Ajibu ndiye aliyeifanya kazi hiyo na kuipatia Yanga bao  pekee kwenye mechi hiyo na kuondoka na ushindi wa bao 1-0.

Ilikuwa ni dakika ya 16, alipopiga faulo hiyo karibu na kibendera cha  kona ya kushoto ya goli la Njombe Mji na mpira huo ukawapita  vichwani wachezaji wa timu hiyo waliokuwa wamejenga ukuta.  Mpira huo ulipofika karibu na goli ukikatika na kuingia upande wa  kulia kwa kipa David Kisu ambaye aliruka eneo la tukio wakati  mpira ukiwa umeshapita.

2. Emmanuel Okwi (Simba vs Mtibwa Sugar)Zilikuwa zimebaki dakika za nyongeza. Tayari baadhi ya mashabiki  wa Simba walikuwa wameshaanza kuondoka uwanjani.

Beki wa Simba, Erasto Nyoni, alifanyiwa madhambi kwenye mstari wa eneo la hatari na mwamuzi kuamuru mkwaju wa fri-kiki.

Ilikuwa ni Oktoba 15, mwaka huu, Okwi aliuchukua mpira huo roho za Wanasimba zikiwa juu.

Akiwa pembeni kushoto kuelekea kwenye goli la kaskazini mwa uwanja wa Uhuru, aliupiga mpira kwa kuuzungusha ukapita juu ya bega la mchezaji wa mwisho wa Mtibwa aliyeweka ukuta na ukajaa wavuni upande wa kulia kwa kipa Benedict Tinoko ambaye pamoja  na kuruka, lakini mpira ulikuwa kasi zaidi kuliko kasi ya mwili wake, mechi ikaisha kwa sare ya bao 1-1.

3. Asante Kwasi (Lipuli vs Simba)Beki wa Lipuli Asante Kwasi alifunga fri-kiki kali kwenye mechi  dhidi ya Simba, Novemba 26, mwaka huu kwenye Uwanja wa Uhuru  jijini Dar es Salaam dakika ya 19.

Ilikuwa ni nje kidogo ya eneo la hatari, beki huyo raia wa Ghana,  aliupiga mpira kwa mguu wa kushoto ukaenda kwenye kona ya mlingoti wa juu.

Kipa Aishi Manula alitumia uhodari wake wote, lakini kasi ya mpira  na eneo ambalo mpira ulipita nyuzi 90 kushoto kwake kwenye goli la Kusini, ilifanya asiufikie kwa urahisi na mpira ukajaa wavuni likiwa bao la kusawazisha na mechi ikaisha kwa sare ya bao 1-1.

4. Kelvin Sabato (Mtibwa vs Azam)Mechi ilichezwa Novemba 27 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam. Huko nako ilipigwa frii-kiki matata sana na straika wa Mtibwa Sugar, Kelvin Sabato.

Tayari Mtibwa ilikuwa nyuma kwa bao 1-0, ilikuwa ni dakika ya 75 wakati wakiwa nyuma kwa bao 1-0  ilipatikana fri-kiki. Illionekana kama ya kawaida tu, lakini mpigaji aliupiga kiufundi mno mpira wa juu na kumhadaa kipa bora na  mjanja Razak Abalora aliyebaki amesimama tu na mpira ukajaa  wavuni.

 

Habari Kubwa