Gonjwa la Manula halikuanzia Mbabane

03Dec 2018
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Gonjwa la Manula halikuanzia Mbabane

PAMOJA na kuwa na kikosi ghali na wachezaji wa kiwango cha hali  ya juu, baadhi ya wanachama na mashabiki wa Simba wameonyesha  kutoridhishwa na kiwango cha sasa cha kipa Aishi Manula hasa kwenye kuokoa mashuti ya mbali.

Golikipa klabu ya Simba, Aishi Manura

PAMOJA na kuwa na kikosi ghali na wachezaji wa kiwango cha hali  ya juu, baadhi ya wanachama na mashabiki wa Simba wameonyesha  kutoridhishwa na kiwango cha sasa cha kipa Aishi Manula hasa kwenye kuokoa mashuti ya mbali.

Jumatano iliyopita kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Mbabane Swallows, Manula aliendelea na tabia iliyoanza kuzoeleka ya  kufungwa mabao kwa mashuti ya mbali.

Manula, kipa namba moja wa Simba na timu ya Taifa ya Tanzania,  Taifa Stars msimu huu amekuwa akifungwa mabao yanayoonekana ni yao aina moja.

Kipa huyo amekuwa akifungwa mabao ya mashuti ya mbali ambayo wengi wanadai kuwa kwa kiwango na hadhi yake hapaswi kufungwa mabao ya aina hiyo.

Hizi ni baadhi ya mechi ambazo kipa huyo amefungwa mabao  yanayoonekana kufanana na kwa kiasi kikubwa ni kutokuwa makini...

 

1. Simba vs Mtibwa (Ngao ya Jamii)

Ilikuwa ni dakika ya 33, wakati straika wa Mtibwa, Kelvin Sabato alipoupata mpira nje kidogo ya eneo la mita 18 na kuachia shuti kali la juu. Manula wala hakuhangaika kuufuata, bali alisindikiza kwa macho  ukajaa wavuni na likawa bao la kusawazisha la Mtibwa. Ilikuwa ni mechi ya Ngao ya Jamii iliyochezwa Agosti 18, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza na Simba ikashinda mabao 2-1, ya  Meddie Kagere na Hassan Dilunga.

 

2. Simba vs Mwadui (Ligi Kuu)

Manula alifungwa bao na straika wa Mwadui Charles Ilamfya dakika ya 81. Alitoka golini, ikiwa haijulikani kama alikuwa anaufuata mpira  au alitaka kulipunguza goli. Ni baada ya mpira mrefu uliopigwa  kuelekea kwenye goli la Simba. Mfungaji aliyekuwa akikimbizana na  Paschal Wawa akiwa mbali na goli aliubetua juu na ukatinga wavuni mwa lango likiwa tupu. Lilikuwa ni bao la kufutia machozi la Mwadui  iliyochapwa mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Kambarage Shinyanga,  mechi ya Ligi Kuu ikichezwa Septemba 22, mwaka huu. Ni mabao ya  John Bocco mawili na Meddie Kagere moja.

 

3. Simba vs African Lyon (Ligi Kuu)

Oktoba 6, mwaka huu kwenye mechi ya Ligi Kuu, Manula aliendelea kuwakera Wanasimba alipofungwa tena bao aina ile ile. Wakati Simba ikiongoza mabao mawili ya Shiza Kichuya na Emmanuel Okwi,  wachezaji wa African Lyon walifanya shambulizi, lakini mabeki wa Simba walikaa imara na mpira ukarudishwa nyuma kiasi cha mita 25 hivi, nje kabisa ya eneo la 18. Mpira huo ulimkuta Awadh Salum  ambaye aliachia kombora kali. Kilichoonekana ni kama vile Manula alitimiza wajibu tu wa kuruka kwani alikuwa mbali na mpira na ni kama  hakutegemea mpigaji kama atapiga. Mpira ukajaa wavuni, Simba ikishinda mabao 2-1.

 

4. Simba vs Alliance (Ligi Kuu)

Japo Simba ilishinda mabao 5-1, lakini wanachama na mashabiki wa Simba hawakupendezwa na bao walilofungwa kwenye dakika tatu za nyongeza likiwekwa wavuni na Zabona Hamisi.

Mechi hiyo ya Ligi Kuu ilichezwa Oktoba 24, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa,  Manula akiruhusu bao hilo kwa shuti lililopigwa nje kidogo ya mita  18. Ilivyonekana ni kwamba hakuruka kwenda mbele 'diving', bali  aliufuata na kuanguka chini akitegemea kuupata, lakini alipishana nao. Na kama angeruka kwenda mbele 'diving' angeweza kuupangua.

 

5. Simba vs Mbabane Swallows (Ligi ya Mabingwa)

Manula aliendeleza rekodi yake ya kufungwa mabao ya aina hiyo aliposhindwa kupangua shuti kali la Guivane Nzambe alilopiga akiwa nje kabisa ya eneo la hatari na mpira huo ukajaa wavuni. Ilikuwa ni  mechi ya Ligi ya Mabingwa kwenye Uwanja wa Taifa, mechi ikichezwa Novemba 28. Lilikuwa ni bao la kusawazisha, ingawa kwa bahati nzuri  dakika 90 zilipomalizika Simba ilishinda mabao 4-1.

 

 

Habari Kubwa