Hadaa ‘foxnews’changamoto kwa vyombo vya habari

19Mar 2017
Ibrahim Mkamba
Nipashe Jumapili
Hadaa ‘foxnews’changamoto kwa vyombo vya habari

SIKU chache kabla ya mtandao wa uongo uitwao foxnews.com kuwaponza wafanyakazi kadhaa wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kwa kunukuu taarifa yake ya uongo na kuirusha kama habari,

Alifika ofisini kwangu binti mmoja aitwaye Neema Adrian, mwanafunzi wa uandishi wa habari kwenye chuo kimoja jijini Dar-es-Salaam. Binti huyo alifika kwangu kupata huduma inayotolewa na taasisi ninayofanyia kazi.

Aliniambia ni mpenzi na msomaji wa safu yangu ya Nasaha kila Jumapili kwenye kona hii ya gazeti la Nipashe, kisha akaniuliza, “kwenye uandishi wako ‘brand’ yako ni ipi?” Alitumia neno la Kiingereza ‘brand’ akimaanisha kitu cha kipekee kinachonitofautisha na waandika makala wengine. Nilimjibu kwamba ‘brand’ yangu ni kukemea yanayotendwa bila usahihi dhidi ya Utanzania.

Baadaye akataka tena kufahamu afanye nini afanye ili awe mwandishi wa habari bora akimaliza masomo? Nami nikamjibu kwa ujumla ni kufuata maadili yote ya uandishi habari na nikaweka msisitizo wa kuchimba kwa nguvu zote ukweli wa taarifa anayopokea.

Akiridhika na ukweli wake ndipo aitumie kama habari lakini baada ya kuiwianisha na upande wa pili ikigusa maslahi ya pande mbili au zaidi.

Siku chache baadaye ndipo likajitokeza sakata la foxnews.com Kwa sasa waandishi wa habari wanapaswa kuongeza umakini maradufu wa taarifa wanazopata kabla ya kuzitumia kama habari kwa sababu dunia sasa imejaa upotoshaji kwa lengo lolote mitandaoni.

Upotoshaji huo umekuwa sehemu ya maisha yetu kwani sasa hivi kunaanzishwa mitandao mingi ya kudanganya inayotoa taarifa za kusisimua za kutengeneza habari kubwa.

Nilichomshauri Neema ni kwamba asiwe na haraka ya kuitumia taarifa, hasa ya kusisimua, kuwa habari bali ajenge utaratibu wa kuhoji sana.

Nikampa mfano kama nimeita waandishi wa habari kuwajulisha naanzisha kituo kikubwa cha kimataifa cha kufundisha michezo mbalimbali ndani ya manispaa ya Morogoro kwa watoto wa rika tofauti wenye vipaji mbalimbali vya michezo asikimbilie kuandika habari hiyo nzito bila kunihoji uwezo wangu kifedha.

Kama nina wahisani, wafadhili na washirika, kina nani na wanapatikana wapi na aniombe njia za mawasiliano yao.

Akishapata vyote hivyo, awatafute watu hao awahoji kuhusu mradi huo. Majibu yangu yakiwa ya kukatisha tamaa, uchaguzi ni wake; kuandika kuhusu uongo wangu kwa mrengo wa kueleza nilivyo mzushi au kutoandika kabisa kuhusu suala hilo.

Kwa msingi huo, mtandao wowote ukieleza chochote cha kusisimua kuhusu jambo lolote, wanaodaiwa kutoa taarifa hiyo watafutwe wahojiwe kuhusu ukweli wa jambo hilo.

Kama ni kauli ya Rais wa nchi fulani aulizwe Balozi wa taifa hilo ukweli wa kauli hiyo kabla haijafanywa kuwa habari.

Waandishi wapeni wasomaji habari si taarifa. Acheni kuripoti matukio. Leo hii kila mara utasikia shehena ya viroba vya thamani ya Shilingi milioni kadhaa imekamatwa mahali fulani.

Hii si habari bali ni taarifa. Ili iwe habari mnapaswa mhoji mtu ana mzigo mkubwa wa viroba ghalani haviuzi kwa sababu vimepigwa marufuku, ili asikutwe na mzigo mzito hivyo akautose baharini au afanyaje? Hamuulizi kodi inayopotea kwa kutouzwa mali hiyo inatazamwaje.

Hamfuatilii shehena inayokamatwa inapalekwa wapi, kufanywa nini. Wala hamuulizi vyombo vya dola vimejipangaje kupambana upya na gongo iliyopotezwa na viroba.

Je mnafuatilia kuona kiwanda kinachotengeneza viroba hakina mzigo huo maghalani. Mtupe habari wanashughulikiwaje nao hao. Mtueleze kama hawazalishi tena bidhaa hiyo.

Mnatupa taarifa tu. Hii si sawa jamani. Chimbeni.

Habari Kubwa