Haikande Hichilema atinga Ikulu

25Aug 2021
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
Haikande Hichilema atinga Ikulu
  • *Mtihani mkubwa unaomngoja, ukosefu ajira, fedha mfukoni

RAIS Haikande Hichilema (59), ameapa kuwatumikia Wazambia jana, baada ya kuibuka mshindi dhidi ya mpinzani wake Edgar Lungu.

Rais Haikande Hichilema, maarufu ‘HH’ amechukua uongozi wa nchi hiyo rasmi baada ya kushinda kwa kishindo. PICHA: MTANDAO

Wakati anaingia ikulu, matarajio ya waliompigia kura ni makubwa hasa kumaliza ukata mkubwa unaowakabili na ukosefu wa ajira ambao ulipelekea baadhi ya wapigakura kwenda kwenye vituo vya kura wakiwa wamevalia majoho ya kuhitimu elimu ya juu lakini hawajapata kazi.

Hichilema kiongozi wa chama cha United Party for National Development (UPND), ana sifa nyingi ikiwamo ujasiri kwani alijaribu kugombea mara tano bila mafanikio, ni mhanga wa kesi za uhaini, alikamtwa na kuwekwa ndani wakati wa kampeni, amevamiwa na kufanyiwa vurugu wakati wa mahojiano na chombo cha habari.

Akiwa na wenzake 14 walinyimwa kufanya kampeni kwa kisingizio cha kuwapo corona inayozuia mikusanyiko, huku chama tawala cha Patriotic Front (PF) kikiendeleza kazi majukwaani, kuwazuia kulilenga kudhibiti ushindani mkubwa ulikuwapo kati yake na rais aliyeshindwa.

Kwa sasa matarajio ya wananchi wa Zambia ni mabadiliko ya kiuchumi kwa kuwa na mzunguko wa fedha, ukuaji wa sekta binafsi, ongezeko la ajira na uhuru wa maoni na wa vyombo vya habari.

Aidha, Rais huyo, ameamsha furaha baada ya kuahidi kutolipa kisasi kwa watesi wake, kuahidi uhuru wa vyombo vya habari kufanyakazi yake kwa mujibu wa sheria na kuacha upendeleo kama ilivyofanyika wakati wa uongozi wa Lungu.

Takwimu za nchi hiyo zinaonyesha ukuaji wa uchumi unabadilika kila mwaka, wakati 2018 ulikuwa asilimia nne, 2019 ulishuka hadi 1.5, na kupanda hadi asilimia 2.3 mwaka 2020.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Benki ya Dunia mwaka 2020, uwapo wa corona ulishusha thamani ya Kwacha fedha ya Zambia kwa asilimia 30, kuongeza madeni ya nje huku taasisi za fedha zikiwa taabani na mamia kupoteza ajira.

HALI ILIVYOKUWA

Siku ya kupiga kura mitandao ilipunguzwa nguvu na wengi kushindwa kutumia mitandao ya kijamii, kutuma na kupokea picha na video mbalimbali, jambo ambalo lilipingwa vikali na wananchi na baadaye Mahakama Kuu, iliamuru serikali kuifungua.

Aidha, Rais Lungua usiku wa kupiga kura alitoa taarifa kwa vyombo vya habari akimshutumu Hichilema na wafuasi wake kwa kufanya vurugu kwenye jimbo la Mashariki Magharibi mwa nchi hiyo na kusababisha vifo vya maofisa wawili wa chama cha PF na kuahidi kuchukua hatua.

Aidha, siku iliyofuata alitangaza kutoridhishwa na mchakato wa uchaguzi kwa kile alichodai kuwepo kwa rafu nyingi, lakini baada ya matokeo kutangazwa usiku wa Agosti 13, mwaka huu na Tume ya Uchaguzi Zambia, alikubali kushindwa.

Kwa mujibu wa tume hiyo, watu 1,023,499 walijiandikisha kwenye daftari la wapiga kura wengi wakiwa ni wanawake na kundi kubwa ni vijana wenye umri usiozidi miaka 35 ambao walimchagua rais, wabunge 156 , diwani na meya na baada ya serikali kuingia madarakani rais ana nafasi 10 za kuteua na kufanya jumla ya wabunge 166.

Matokeo yaliyotangazwa na chama tawala , PF kilipata majimbo 72 wakati UPND ya Hichilema ikizoa majimbo 83 naye akishinda kwa zaidi ya kura milioni 2.8 , wakati Lungu akiambulia milioni 1.8 kukiwa na tofauti ya kura zaidi ya 1000,000.

Ikilinganishwa na uchaguzi wa nchi nyingi za Afrika, Zambia wananchi wanachagua meya wa serikali za mitaa, lakini pia wafungwa waliwekewa vituo vya kupiga kura na walipata nafasi ya kutimiza wajibu wa kikatiba.

KILICHOMWANGUSHA LUNGU

Wachambuzi wa siasa nchini humo, wanaokutana na waangalizi wa uchaguzi wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA), wanaeleza kuwa makada wa PF walikuwa wakifanya vurugu kwenye vyombo vya habari na takribani radio saba zilivamiwa na vifaa kuharibiwa, huku waandishi wakipigwa.

Aidha, hali ngumu ya maisha hasa kukosekana fedha na ajira ni sababu kubwa ya wananchi kutaka mabadiliko. Kadhalika kukithiri ufisadi serikalini nako kulichangia. Utafiti uliofanywa Julai 2020 na Chuo Kikuu cha Gothenburg’s kwenye serikali kuu na za mitaa ulibaini viongozi walitumia ujio wa corona kujipatia madaraka na kujitajirisha.

Aidha, dola za Marekani milioni 4.3 zilizotolewa na Sweden na Ireland kusaidia watu maskini nchini humo zilipotea katika mazingira tatanishi bila kuwafikia walengwa. Kwa mujibu wa ripoti ya hali ya rushwa (Transparency Internationals’ 2019 Corruption Perception Index) Zambia ilikuwa ya 113 kati ya mataifa 180, huku uwezo wa kupambana na rushwa ukizidi kushuka na wananchi wengi kubakia maskini na wachache wakitajirika.

Aidha, serikali ya Lungu ililaumiwa kwa kufungia vyombo vya habari ikiwamo kuwafukuza kazi walokuwa wanafanyakazi kwenye vyombo vya umma kabla ya Lungu kuingia madarakani na pia kubinya uhuru wa wanahabari na kuvipangia cha kuripoti.

Mwandishi alikuwa mwangalizi wa uchaguzi mkuu wa Zambia.