Hakimu anayeongoza magari

15Feb 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Hakimu anayeongoza magari
  • *Mtoto wake aligongwa na gari, aendesha kampeni ya usalama barabarani

NI jambo la kushangaza kumuona hakimu ambaye amepewa mamlaka ya kutafsiri sheria, anasimama katikati ya barabara akiongoza magari.

Lakini kwa Monica Dongban Mensem, kwake si jambo linalompa ukakasi, kwani anapomaliza kazi yake ya kuhukumu watu mahakamani huelekea barabarani na kufanya kazi hiyo ya ziada.

Monica ambaye ni raia wa Nigeria, huongoza magari barabarani katika mji mkuu wa Abuja, kazi hiyo ameifanya ndani ya miaka minane baada ya mtoto wake wa kiume kufa kwa kugongwa na gari barabarani.

Kulingana na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), mwanamke alikutwa akiwa amevalia fulana ya bluu, miguu ikiwa upande, akitokwa na jasho akitumia mikono yake kwa ukakamavu kwa kuongoza magari.

Muda huo magari yalikuwa yamesongamana huku madereva wakipiga honi, kutokana kushindwa kuvumilia kusubiri kwa muda mrefu.

"Wanaigeria wengi huwa hawana subra na inaonekana katika uendeshaji wao wa magari ," Hakimu Dongban-Mensem aliiambia BBC
Hajafahamu ni nani aliyehusika na kifo cha mwanae, lakini anataka kukabiliana na baadhi ya uendeshaji mbaya wa magari anaoushuhudia katika nchi hiyo.

Kabla ya kuingia barabarani, alianza kwenda kwenye vituo vya magari kuongea na madereva juu ya usalama barabarani nchini Nigeria.

Anasema kilichomshtua ni idadi kubwa ya madereva hawakua wamepata mafunzo yanayofaa juu ya sheria za barabarani.

Monica ambaye ana umri wa miaka 62, ameanzisha shirika lisilo la kiserikali lililopewa jina la marehemu mtoto wake, Kwapda'as Road Safety Demand , kwa lengo la kutoa elimu kwa madereva juu ya usalama barabarani.

Kutokana na kutoridhika na hilo, hakimu Dongban-Mensem alitaka kushiriki katika kudhibiti uendeshaji wa magari mwenyewe.

Baada ya wiki kadhaa za mafunzo ya tume ya usalama barabarani alipata ujuzi wa ofisa usalama barabarani wa kuongoza magari.

Ilipofika mwaka 2016, miaka mitano baada ya ajali , alijaribu kwenda eneo alipofia kijana wake katika mji wa kati mwa Nigeria wa Jos.

"Lengo langu lilikua ni kumpata mtu ambae angalau angeniambia au kunielezea jinsi mwanangu alivyokufa." Anasema Monica
Lakini alipofika, alipata uoga, huzuni na hasira kutokana na ghasia alizoziona.

Makutano ya Miners, katika eneo la Tundun Wada mjini, ni moja ya maeneo yenye msongamano mkubwa wa magari , ikiunganisha wilaya kadhaa za kibiashara katika eneo tambarare la mji mkuu Abuja.

Aligundua miundombinu ya barabara ulikua duni, aliona jinsi zilivyoharibika na hakuna alama za kuwaongoza madereva na watembea kwa miguu.

TUKIO LA KUTISHA

Ilikua ni miundombinu hatari ambayo husababisha ajali nyingi na hiyo ni moja ya sababu zilizomuua mtoto wake wa kiume wakati huo alikuwa kijana wa miaka 32.

"Kwa maoni ya mtu wa kawaida, ninaweza kusema muundo wenyewe wa barabara ni hatari na tuligundua kuwa watu wengi wameuawa katika maeno mengi ya barabara na hakuna utatuzi uliotolewa na serikali ," anasema.

Maofisa mjini Jos wanasema kuwa wanakarabati barabara na kuongeza kwamba wanatoa pole kwa waliowapoteza wapendwa wao katika ajali za barabarani. Lakini ofisa mmoja anasema kuwa wanaotembea kwa miguu na madereva wanapaswa kuwajibika kuhusu namna wanavyotumia barabara.

Watu katika eneo hilo walimwambia Monica kwamba walimuona mtoto wake akiwa amelala barabarani, lakini hawakuweza kumsaidia.

"Miguu yake miwili ilivunjika na majirani katika eneo hilo waliangalia wakati mwanangu akipata maumivu, kuvuja damu iliyotiririka toka upande mmoja wa barabara hadi mwingine ," Hakimu Dongban-Mensem alisema kwa hasira.

"Alikata roho katika dimbwi la damu yake lakini nina uhakika angenusurika na kifo kama angekimbizwa hospitalini ."

Kijana wake alikua amehitimu shahada ya sheria katika chuo kikuu cha Jos muda mchache na alikua amerejea mjini humo kwa ajili ya kuchukua cheti chake.

"Mwanangu alitaka kuwa mwendesha mashtaka bora duniani lakini alikufa kama kuku mtaani baada ya kugongwa na gari ." aliongeza kusema huku akilia.

Tangu Kwapda'as Dongban alipogongwa na gari, idadi ya watu ambao wameuawa katika barabara za Nigeria imesalia kuwa ni ile ile.
Juhudi za kutaka haki

Kwa mujibu wa mamlaka ya shirikisho ya usalama wa barabarani nchini Nigeria, idadi ya vifo ilishuka kidogo mwaka 2013, lakini tangu wakati huo kati ya watu 5,000 na 6,000 wanakufa kila mwaka kutokana na ajali za barabarani.Hii inamaanisha kuwa watu 13 hufa kila siku.

Nyingi kati ya ajali husababishwa na madereva wasio na leseni, ni tatizo la mara kwa mara, kwa mfano zaidi ya watu 60,000 mjini Lagos walikua wakiendesha gari bila leseni.

Zaidi ya hayo, hakuna taarifa za usajiri wa magari au kamera za kunasa utambulishi wa madereva wa magari yanayotoroka
Hii inaleta ugumu wa kufuatilia madereva wanaogonga watu na kukimbia, kama aliyemgonga mtoto wa hakimu Dongban-Mensem.

Kama maderava wanaogonga watu na kukimbia wakikamatwa wanaweza kushitakiwa kwa kuua na kukabiliwa na kifungo cha miaka 14 jela , iwapo watapatikana na hatia.

Hakimu Dongban-Mensem anahisi hii haitoshi. Anasema wale wanaopatwa na hatia wanapaswa kufungwa kifungo cha maisha na familia za waliouawa wapewe fidia ya pesa.

Lakini hii bado huenda isitoshe kukabiliana na maumivu ya kumpoteza mpendwa wako.

"Nilishindwa kulala, nikiwa na matumaini kwamba kijana wangu atapita mlangoni na kunikumbatia. Anasema na kisha anaendelea "Pia niliacha sahani ya chakula mezani nikitumai atarejea nyumbani akiwa na njaa," alisema.

Hataki mama mwingine apitie haya na ameazimia kupeleka ujumbe wa usalama wa barabarani katika kila mtaa wa nchi ya Nigeria.

Habari Kubwa