Hakuna mgawo, maji yanapatikana ndoo ya lita 20, kwa bei shilingi 10

26Mar 2020
Mary Mosha
Siha
Nipashe
Hakuna mgawo, maji yanapatikana ndoo ya lita 20, kwa bei shilingi 10
  • Kutoka safari ndefu dhiki ya maji

NI miaka takribani 20 sasa, tangu kuachwa shilingi 10 ya Tanzania kutumika kununua vitu mbalimbali, ikiwemo peremende. Leo, maeneo mengi hayana nguvu ya kufanya chochote katika ununuzi wa vitu, huku baadhi ya watoto wa vizazi vya sasa hawatambui kabisa.

Shilingi hiyo yenye muonekano wa sarafu ya shaba, zamani ilipokuwa na nguvu, ilikuwepo shillingi 10 ya noti iliyotumika katika ununuzi.

Hali ya sasa na kwa wenye vilivyopo sasa, ni vigumu kuifahamu. Ila, unapoenda wilayani Siha,kuna maajabu ya nguvu ya kiasi hicho cha fedha na mtu akiwa na kiasi cha shilingi 10, anajipatia maji lita 20.

Nipashe hivi karibuni ilitua katika kijiji cha Kiruwa , kwenye Kata ya Lawate, wilayani Siha na kukutana na mkazi Nicholaus Msalo, anayeanza kwa majigamho kwamba wilaya haina changamoto ya maji vijijini, kutokana na serikali kuanzisha utaratibu maalumu wa upatikanaji maji kupitia bodi za maji zilizoundwa.

Anasema, katika miaka ya hivi karibuni, walikuwa wanakabiliwa na ukosefu wa maji safi na salama na ikawalazimu kuchota katika makorongo ambayo hayakuwa safi na salama, hali iliyowaingiza katika mlipuko wa maradhi ya tumbo.

“Serikali kupitia Bodi ya Maji ya Makiwaru Magadini na Fuka Lawate, zilisaidia katika kuwezesha kutatua changamoto kubwa iliyowakwamisha wananchi wengi katika kupata maendeleo,” anasema.

Mkazi mwingine, Nora Lyimo, anasema bodi hizo za maji ziliweza kumsaidia mwananchi asitembee umbali mrefu na badala yake ajikite katika shughuli za maendeleo.

“Mimi kama mama kwa sasa naweza kujikita katika kuhakikisha nashiriki katika shughuli za kimaendeleo badala ya kuanza kutembea umbali mrefu katika kuleta maji,” anasema.

Amina Mhando, ni mmoja ya wanaouza maji katika vilula hivi, anasema mwanzoni waliteseka sana kupata maji safi na salama tulikuwa tunapata magonjwa ya mlipuko kama homa ya matumbo.

Pia, mkazi huyo anakumbusha kwamba, walipata matatizo makubwa ya kiafya yaliyosababisha kupoteza pesa nyingi kwa ajili ya matibabu.

Inawezekanaje?

Wenyeviti wa bodi za maji zinazotoa huduma katika wilaya hiyo ya Siha, kuanzia na Mwenyekiti Yohana Laizer, wa Bodi ya Lawate Fuka, anasema katika miaka ya 1970 hadi 1980 miradi hiyo yote ilikuwa chini ya Mkandarasi wa Wilaya ya Hai.

Laizer anasema, wiliaya hiyo baadaye haijagawanjwa na kupatikana wilaya mpya ya Hai, ikiwa na miradi 15 ikiwa chini ya Mhandisi wa Mkoa.

Anaeleza kwamba, mirani hiyo ili shindwa kuendelea kutokana na ukosefu wa fedha za kufanya matengenezo na kuajiri wataalamu wa kuiendesha.

Mwenyekiti huyo anaeleza kuwa, katika mwaka 2002/2003, mradi uliweza kufanyiwa ukarabati na kupanuliwa na serikali ya Ujerumani kwa kushirkiana na serikali ya Tanzania, ikigharimu zaidi ya Sh. bilioni 3.6.

“Sehemu ya pili ya mradi huo ni Levishi ambao uligharimu zaidi ya Sh. bilioni 1.7, katika vijiji vya Mese, Ngaroni, Mowo, Njamu, Samaki maini, Nrao, Kisangara, Nsherehehe, Ngirinyi na Koboko,’ anafafanua.

“Mradi huo ulilenga kuwafikia wananchi zaidi ya 42,000 ifikapo 2015, ingawa hadi mwaka 2014 wananchi 41,850 walifikiwa na maji safi na salama,” anasema Laizer.

Katika miaka 12 ya kuwepo mradi, unaelezwa kufanikiwa kuwahudumia maji bila ya mgawo kwa wananchi hao.

Meneja Mradi

Meneja wa mradi huo, Elihuruma Masaoe, anasema kuwapo mradi, kumechangia maisha kuboreka kwa kuwa na nyumba za kisasa, umasikini nao kupungua, shughuli nyingi za kiuchumi kuibuka, ufaulu wa wanafunzi shuleni kuwepo na watu 26 kuajiriwa katika mradi.

Katika suala la uendeshaji mradi huu una wajumbe za bodi, wajumbe wa kwanzia ngazi za vijiji, hadi wilaya za kamati za maji hali ambayo wameona umuhimu wa uwepo wa vilula zisivyozidi mita 400 na kuviboresha kwa kuondokana na uzio wa majani na kujenga uzio wa matofali ya kuchoma.

Kutokana na ubora wa maji yanayotolewa na bodi za maji zilizopo Siha, kumechangia kupungua kwa magonjwa ya mlipuko, ingawa bodi hiyo ya Fuka Lawate, inakabiliwa na changamoto mbalimbali, zikiwemo ongezeko la watu, mabadiliko ya tabianchi yaliyochangia, kukauka kwa baadhi ya vyanzo vya maji, ikiwemo mto Mese.

Anasema, kumekuwapo ukataji miti ya asili kwenye hifadhi ya msitu wa Kilimanjaro pamoja na maamuzi ya kujenga taasisi kubwa za kiserikali na za binafsi bila kushirikisha bodi hizo.

Julius Moleli, ni Mwenyekiti wa Bodi ya Maji Magadini Makiwaru, anasema mradi natoa huduma kwa wananchi kwa mfumo wa mita na kuna vilula (public tabs) zaidi ya 313 vinavyotoa huduma ndani ya mita 400, pia wateja 3012 wamefungiwa na kuna taasisi 400 jumla yao 3425.

Anasema, kuwa wateja wa vilula 750 kwa mita ya ujazo lita 20 kwa 15 tu, taasisi shule za msingi na sekondari, taasisi za dini, hospitali na vituo vya afya bei ya maji ni Sh.12 kwa ndoo ya ujazo wa lita 20.

Masaoe, wateja wa majumbani ni Sh. 900 kwa mita, wafanyabiashara, waosha magari na vyenye viwanda vidogo vidogo 1000 kwa mita.

"Mradi huu unaweza kujiendesha bila ruzuku ya serikali au wafadhili tangu ulipoanzishwa hadi sasa na walengwa wanatambua, mradi huo hulipa ankara zao kwao za maji kwa wakati kwa asilimia zaidi ya 97 ambapo shule zaidi ya 32 za msingi na nane za sekondari katika eneo la mradi," anasema.

Anasema, mradi huo unahudumia skimu za umwagiliaji nne, ikiwemo Gararagua inayohudumia wakazi zaidi ya 22,000, sikimu ya pili Rozylin/Mjimwema, inayotarajia kuhudumia watu zaidi ya 6000 na ya tatu ikiwa ni Lemosho (West Kilimanjaro) yenye uwezo wa kuhudumia watu zaidi ya 19,000 na ya nne ni North west Kilimanjaro unaotarajiwa kuhudumia watu 15,000.

Pamoja na mafaniko ya mradi, bado unakabiliwa na changamoto mbalimbali, zikiwamo ongezeko la maji katika skimu ya umwagiliaji ya Magadini, ambayo kwa sasa ina idadi ya watu 40,000 wakati mradi huo, ulisaini kuwa na watu 22,000 ifikapo 2015.

Anasema, kutokana na changamoto hiyo Halmashauri ya Wilaya ya Siha, kwa kushirikiana mradi kuongeza tanki la maji kwa ajili ya kuongeza skimu ya Gararagua na kulaza bomba jipya lenye urefu wa kilomita 6.5.

DC wa Siha

Mkuu wa Wilaya Siha, Onesmo Buswelu, anasema utekelezaji huo umekuwa rahisi, baada ya bodi hizo za maji kushirikiana na serikali katika kuwafikia wananchi.

"Katika wilaya ya Siha kuna bodi mbili za maji ambazo zinashirikiana na serikali katika kuwahudumia wananchi, hali iliyosaidia kufikisha maji kwa wananchi kwa asilimia 87.

“Hivyo, tumevuka malengo yaliyowekwa na wizara ya vijijini kufikishe maji kwa asilimia 85, "anasema Mkuu wa Wilaya, Biswelu.
Aidha, mkuu huyo aliwataka wananchi kutunza vyanzo vya maji pamoja na miundombinu, iliyowekwa na miradi hiyo, ili waweze kupata maji bila ya mgawo.

Pia, kiongozi wa kisiasa – CCM, Wilfred Mosi, anasema katika wilaya hiyo imewasaidia wananchi kupata maji kwa vijiji 60, ingawa bado kuna vijiji 12 hawapati maji ya kutosha, ingawa serikali imechukua jukumu na kushirikiana na bodi katika kuhakikisha wanamtua mama ndoo kichwani.

"Katika wilaya hii kunamiradi ya maji miwili ya Fuka Lawate na Magadini Makiwaru, iliyosaidia kumtua mama ndoo kichwani ambayo kwa kushirikiana na serikali na kusambaza maji kwa asilimia 85 kwa vijijini,” anasema Mosi.

Habari Kubwa