HALMASHAURI YAJITWISHA ZIGO LA WAZEE

09Sep 2017
Mary Geofrey
Nipashe
HALMASHAURI YAJITWISHA ZIGO LA WAZEE
  • Inawagharamia bakora, miwani, dawa…

MANISPAA ya Ubungo iliyoanza rasmi Septemba mwaka 2016 ni kati halmashauri tano za mkoa wa Dar es Salaam, pamoja na upya ina jambo la kujivunia nalo ni kufanikisha kuanzisha na kutoa kadi za matibabu bure kwa wazee wote.

Meya wa Ubungo, Boniface Jacob anasema wazee hao watapatiwa dawa , miwani, fimbo za kutembelea, fursa ya kumuona dakatri na matibabu yote bure.

Ubungo , ikiwa na vituo 19 vya umma vinavyotoa huduma mbalimbali za afya nyingine zikihusika na msamaha kwa makundi maalum.

Sasa imezindua mpango wa kutibu wazee bure Sepemba 4, mwaka huu na imetoa kadi kwa wazee 7,299 kwa ajili ya kuwapa matibabu.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, akizindua huduma hiyo, mbali na kuipongeza Halmashauri ya Ubungo kwa kuanzisha utaratibu huo muhimu, anasema utasaidia kuondokana na changamoto za kumudu matibabu.

Anasema hiyo ni hatua ya kwanza huku akizitaka Halmashauri nyingine kuiga mfano huo, kwa kuhakikisha wazee wanapatiwa kadi za matibabu bure na kutibiwa kwa wakati.

“Si tu mmefanya kazi nzuri bali mmekuwa halmashauri ya kuigwa, na ziasa nyingine ziige mfano huu. Pia hakikisheni hawa wazee wanapatiwa huduma sahihi kupitia madirisha ya wazeee ambayo tulishaagiza yaanzishwe kwenye hospitali na vituo vya afya vya serikali,” anasisitiza Waziri.

Anawahakikishia pia wazee hao kuwa, huduma za matibabu watapata kuanzia ngazi ya chini ya zahanati hadi taifa kwa kufuata utaratibu wa rufaa.

Pia anasema upo mchakato mwingine ambao unafanywa na serikali wa kuhakikisha wazee wanapatiwa pensheni ya kila mwezi kwa wenye umri kuanzia miaka 70 ili kujikimu na mahitaji mbalimbali ya maisha yao.

“Wenzetu Zanzibar wameshaanza utaratibu wa kuwapatia pesheni wazee ya Sh. 20,000 kila mwezi ni fedha kidogo lakini itawasaidia kujikimu na mahitaji mbalimbali,” anaongeza.

Ummy pia anaahidi kuzitatua changamoto za kiafya zilizopo katika Manispaa hiyo, ikiwamo kujenga wodi ya wazazi na utekelezaji wake utaanza karibuni na pia kuwapa kadi 100 za matibabu kwa watoto wadogo.

Anasema katika Kituo cha Afya cha Sinza, tayari bajeti ya dawa imeongezwa ma kufikia Sh. milioni 69, kutoka milioni 32
Mbali na hilo, pia anawataka watumishi wa vituo vya afya kuacha kuuza maduka ya dawa nje ya vituo vya afya na kuwaelekeza wagonjwa kununua kwa bei kubwa katika maduka hayo.

“Sisemi msiwe na maduka ya dawa lakini muhimu mzingatie dawa zipo hivyo kusiwepo na ubabaishaji wa kuwaandikia dawa ambazo hazipo serikalini ili mradi mgonjwa atoke akanunue katika maduka yenu mkifanya hivyo na kugundulika sitawavumilia,’’ alisema Waziri Ummy.

MPANGO WA HALMASHAURI
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya , Dk. Mariam Majiliwa, anasema katika wilaya hiyo kuna hospitali moja, vituo vya afya vitatu, zahanati 15 na kliniki ya mama na mtoto moja.

“Hadi kufikia Agosti 22, mwaka, Manispaa imeweza kuwatambua jumla ya wazee 7,299 kutoka kata 11 na kata tatu zilizobaki utambuzi unaendelea,” anasema.

Dk. Majiliwa anasema, kati ya wazee 7,299, wanaume ni 3,454 na wanawake ni 3,845.

Anabainisha kuwa, jumla ya wazee 2,051 wakiwamo wanaume 1,214 na wanawake 837 tayari wameshapigwa picha na kazi ya kudurufu vitambulisho vyao inaendelea na 5,248 waliobaki kazi ya upigaji picha inaendelea katika kata husika.

Wazee hawa wametambulika kupitia kata zao husika kwa vigezo vya wasiojiweza kuanzia umri wa miaka 60 na kuendelea na mkazi wa Manispaa ya Ubungo, mkoa wa Dar es salaam.

Dokta Majiliwa alitaja sifa nyingine kuwa ni awe amejiandikisha kupitia Mtendaji wa kata husika na awe amepigwa picha.

Pia alieleza matarajio ya Manispaa hiyo ni kukamilisha kazi ya utambuzi na utoaji wa vitambulisho vya msamaha wa huduma za Afya kwa wazee wote 7,299 ifikapo Septemba 30, mwaka huu.

CHANGAMOTO
Majiliwa anasema, pamoja na utekelezaji huo Manispaa ya Ubungo imekuwa ikipambana na changamoto mbalimbali katika utoaji wa huduma za afya.

Anataja changamoto hizo kuwa ni gharama za uendeshaji wa huduma za msamaha ambazo zimekuwa kubwa hususani katika Hospitali ya Wilaya Sinza.

“Mwaka wa fedha 2016/17 ilikuwa ni Sh. bilioni 1.8 ambazo ni zaidi ya ukomo wa bajeti ya hospitali ya Shilingi bilioni zinazotokana na vyanzo vyake vyote vya mapato ,” anasema Dk. Majiliwa.

Anaeleza sababu za gharama za uendeshaji kuzidi ni kutoka na idadi kubwa ya wagonjwa wanaohitaji msamaha, wakiwemo wajawazito, watoto chini ya miaka mitano na wazee.

Anataja changamoto nyingine kuwa ufinyu wa nafasi ya wodi za kulaza wagonjwa pamoja na kutokuwa na chumba cha kuhifadhi maiti.

Pia anasema wana changamoto ya watumishi wa afya 268 katika Halmashauri hiyo na kwamba waliopo ni watumishi 564 wakati ikama ikielekeza watumishi 832.

Pia alitaja changamoto nyingine kuwa ni upungufu wa magari ya kubeba wagonjwa na upungufu wa gari kwa ajili ya huduma za chanjo na usimamizi shirikishi.

MIKAKATI
“Pamoja na changamoto hizo zinazoikabili halmashauri yetu ya Ubungo kwa Idara ya Afya na Ustawi wa Jamii, tumekuwa na mikakati mbalimbali ya kutatua changamoto hizi,” anasema Dk. Majiliwa.

Awali , wanaomba kuongezewa mgawo wa ruzuku ya dawa kutoka serikali kuu kwa hospitali ya Sinza. Aidha wametenga Sh. milioni 200 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa ghorofa nne za hospitali hiyo. Pia wana mpango wa kujenga chumba cha maiti mwaka wa fedha wa 2018/19.

Pia anasema wana magari mawili kwa ajili ya huduma za kiofisi hivyo wanahitaji magari kwa ajili ya huduma za chanjo ili kuweza kuongeza ufanisi wa utoaji huduma za afya kinga.

NASAHA ZA MEYA
Meya wa Ubungo, Boniface Jacob, mbali na kushukuru Waziri Mwalimu kwa kuwazindulia huduma hiyo, anasema mradi huo imegharimu zaidi ya Sh. bilioni 1.8.

Anasema walipanga kutekeleza mradi huo, katika kikao cha Baraza la Madiwani, Aprili mwaka huu na walipitisha na baadaye kazi hiyo kuanza.

Anasema waliamua kama halmashauri kutokutoa zabuni kwa watu wengine na badala yake walinunua mashine zao ambazo zinatumika kuwasajili wazee hao na baada ya kazi hiyo zitatumika kwa shughuli nyingine za halmashauri.

Habari Kubwa