Hamahama holela ya wafugaji inavyoachia watoto janga afya

26Mar 2020
Happy Severine
Meatu
Nipashe
Hamahama holela ya wafugaji inavyoachia watoto janga afya
  • Msimu ukifika wanatelekeza chanjo
  • Msimu ukifika wanatelekeza chanjo

KUNA shida ya matibabu kwa watoto kutoka jamii za wachungaji wilayani hapa. Kama ilivyowahi kuripotiwa na gazeti hili, hamahama ya jamii hiyo kwenda kutafuta malisho inavyoathiri elimu, hilo nalo ni janga kwa huduma ya afya.

Wafugaji na wakulima wa wilaya ya Meatu wakijianda na safari kuelekea mikoa mingine. PICHA: HAPPY SEVERINE.

Hadi sasa inaelezwa, wakazi wa Meatu, wameshindwa kudhibitiwa katika mwenendo huo, hata kuzua madhara makubwa kwa watoto wengi, wahusika wakuu ni familia za wafugaji.

Namna madhara yalivyo, inaelezwa muda mrefu wanakosa huduma za msingi za afya watoto wao, ikiwamo chanjo mbalimbali zinazotolewa kwao, pia wajawazito.

SERIKALI YAONGEA

Charles Manota ni Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mwamanimba, anataja sababu kubwa ya wananchi kuhama kila mwaka, ukame unaoikumba wilaya hiyo, hata inasukuma watu kuhama kwa kukosa mashamba ya kilimo, wakielekea mikoa ya Morogoro, Katavi, Rukwa na Tabora.

Ofisa Mtendaji huyo anaeleza hilo, zaidi linatokea katika miezi Julai, Agosti, Septemba, Oktoba hadi Novemba, makundi makubwa ya wananchi wanakimbia, kusogelea mikoa hiyo.

Manota anabainisha moja ya eneo ambalo watoto wadogo wamendelea kukosa haki hizo za msingi kwenye wilaya hiyo, ni katika kata ya Mwamanimba, ambayo mwaka jana kaya nyingi zilihama.

Manota anataja sekta inayoathiriwa zaidi na hamahama ya wananchi wilayani, ni afya ambayo watoto na wajawazito wengi wanakuwa hawajamaliza chanjo na dawa za kinga mbalimbali.

Analalamika serikali imekuwa ikitumia pesa nyingi kunusuru vifo vya watoto wachanga na wajawazito, kwa kuanzisha chanjo kama kinga kuu na kuwahudumia kwa karibu wajawazito, lakini ni tofauti kwa jamii ya ufugaji.

Mganga Mfawidhi wa zahanati ya kijiji cha Mwamanimba, Victor Moshi, anasema kwa chanjo za watoto wenye umri chini ya miaka mitano wanaathirika zaidi, kwani wengi hawamalizi dozi kutokana na wazazi wao kuhama.

Moshi anasema, serikali imekuwa ikitoa chanjo ya kutibu maradhi ya tumbo, kifua kikuu, pepopunda, kifaduro, pumu, surua, lubera na polio, kwa ajili ya kuwakinga watoto wadogo.

Anasema, inawakinga watoto hao na maradhi ili wasipatwe na magonjwa, lakini watoto hao wa wafugaji wamekuwa wakikatishwa kupata huduma hizo.

Moshi anasema, mwaka jana familia nyingi zilihama katika kijiji hicho, malengo yao yalikuwa kuwafikia watoto 324, lakini waliopata chanjo kwa usahihi ni asilimia 64 ya malengo.

“Wengi wamehama na wazazi wao, hakuna mzazi hata mmoja ambaye amekuja kuaga ili tuweze kumwandikia barua ya kumtambulisha mtoto wake kule anakokwenda, ili wajue amepata chanjo gani kwa kiasi gani na aweze kuendelea,” anasema Moshi.

Pia, anasema kuwa asilimia zaidi ya 30 ya watoto hao hawajamaliza chanjo husika, hivyo wana hatari katika siku za baadaye kupata magonjwa hayo na yakawaletea matatizo zaidi ikiwemo vifo.

Anasema, wamekuwa wakifanya jitihada kubwa ya kuwaelimisha wananchi umuhimu wa wajawazito na watoto kupata chanjo zote kwa wakati, lakini jamii hiyo ya kifugaji bado haijaona umuhimu unaosisitizwa.

“Binafsi naumia sana pale ninapoona watoto wadogo na wajawazito wanashindwa kupata chanjo wa uzembe, wakati serikali inajitahidi sana kuboresha huduma zao,” anasema.

Moshi anaiomba serikali ya wilaya na kata kwa umoja wao, kutafuta namna sahihi ya kuwajengea mazingira mazuri wafugaji, ili wafuge kisasa na kuachana na tabia ya kuhama, hali inayoyumbisha maisha ya familia zao.

Kwa mujibu wa Moshi, mwaka jana idadi kubwa ya wananchi katika kata hiyo walihama katika kipindi hicho cha ukame mkubwa zaidi, kuliko miaka yote.

“Anasema kwa mwaka 2019, kata nzima yenye vijiji vitano na jumla ya kaya 12 zimehama na kwenda katika mikoa mbalimbali, kwa ajili ya kutafuta maeneo ya kilimo, malisho ya mifugo na makazi.

“Kwa wastani kila kaya moja ina watu kuanzia sita na kati ya hao wanafunzi ni wanne, hivyo kuna zaidi ya watu 100 wamehama kwa mwaka huo na hao wameondoka na watoto wadongo ambao wangetakiwa kupatiwa huduma za afya hususani chanjo mbalimbali,” anasema.

WANANCHI

Dai la wananchi waliozungumza na Nipashe, ni kwamba kinachohitajika zaidi ni elimu kwa jamii ijue athari zinazoweza kutokea, endapo watashindwa kuwapatia haki ya msingi ya huduma za afya (chanjo) watoto wao.

Ngasa Jisenge, ni wanakijiji cha Mabambasi, anasisitiza haja ya elimu kutibu tatizo hilo, wananchi hawana uelewa kuhusiana na madhara yanayoweza kutokea, endapo mtoto atashindwa kupata chanjo zote.

“Elimu itolewe zaidi kwani kuhama siyo jambo baya, lakini mtoto akienda na taarifa zake muhimu, hata huko ambako anaenda ataendelea na huduma hizo hizo vizuri. Ni elimu tu inahitajika kwa wingi,” anasema Jilala.

Aidha, dai lingine la wananchi hao wanataka kuwepo sheria ya kuwabana wanaohama, kuhakikisha wanawapatia watoto huduma zote zinazohitajika, hata kama watahama, bali liwepo hitaji lia kuwafuatilia.

“Elimu imekuwa ikitolewa, lakini wengi hawaelewi. Ni vyema serikali ikaweka sheria kali, watu wandelee kuhama lakini wahakikishe zile haki za msingi za mtoto zinaendelezwa na siyo kumpeleka porini kulima au kuchunga,” anasema Masunga John.
Serikali.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwamanimba, Jilala Mahona, anasema elimu wanaitoa kila mara, lakini mazingira na hali ya hewa ya wilaya hiyo, ndiyo msukumo mkuu wa watu hao kuhama.

“Hata kama tatizo ni ukame, tunawaambia kutoa taarifa ni muhimu na watoto wawachukulie uhamisho, lakini wengi hawajali hilo, na sisi kuwafuatilia hatuna uwezo huo kwani kunahitaji gharama kubwa,” anasema Jilala.

Ofisa Mtendaji wa Kata, Manota, anasema wamekuwa wakiwasiliana na viongozi wenzao kwenye mikoa wanakohamia, lakini tatizo limekuwa gharama ya kufuatilia.

Manota anasema, hivi karibuni wamefanikiwa kumrudisha mwanafunzi mmoja aliyetakiwa kuanza kidato cha kwanza mwaka huu, kwani wazazi wake walihama naye, baada ya kufanya mtihani.

“ Tumefanikiwa kumrejesha kwa kushirikiana na viongozi wenzatu huko walikokuwa na ameanza shule. Tatizo ni kubwa, lakini kuweza kupamba nalo hapo kuna ugumu kidogo,” anasema Manota.

Habari Kubwa