'Hat-trick' 7 zavunja rekodi msimu uliopita

29Jun 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
'Hat-trick' 7 zavunja rekodi msimu uliopita

MABAO matatu yaliyofungwa na straika wa Biashara United, Atupele Green, Jumatano iliyopita kwenye Uwanja wa Karume mjini Musoma, timu hiyo ikiichapa KMC ya Kinondoni mabao 4-0, kumeifanya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu kufikisha 'hat-trick' saba na kuvunja rekodi ya msimu uliopita.

Msimu uliopita 2018/19, Ligi Kuu Tanzania Bara ilimalizika kukiwa na 'hat-trick' sita, ambazo zilifungwa.

'Hat-trick' sita za msimu uliopita zilipatikana kwa wachezaji Alex Kitenge wa Stand United, Emmanuel Okwi wa Simba aliyefunga 'hat-trick' mara mbili kwa msimu mmoja, Salum Aiyee wakati huo akiwa Mwadui, Fully Maganga wa Ruvu Shooting na Meddie Kagere wa Simba.

Atupele alipata mabao matatu 'hat-trick', kwenye dakika ya 69, 73 na 90 dhidi ya KMC na kuvunja rekodi hiyo ya msimu uliopita.
Hawa ni wachezaji waliofunga magoli matatu, 'hat-trick' saba msimu huu pamoja na mechi zake.

1. Ditram Nchimbi (Polisi Tanzania 3-3 Yanga)

Mchezaji wa kwanza kwenye Ligi Kuu msimu huu kufunga 'hat-trick' ni Ditram Nchimbi, wakati huo akiichezea Polisi Tanzania, kabla hajahamia kwenye klabu ya Yanga kipindi cha dirisha dogo la usajili.

'Hat-trick' yake aliipiga kwenye mechi dhidi ya Yanga, Oktoba 2 mwaka jana zilipocheza kwenye mzunguko wa kwanza kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam na timu hizo kutoka sare ya mabao 3-3.
Ditram alifunga magoli hayo dakika ya 33, 55, na 57, huku ya Yanga yakifungwa na Mrisho Ngassa na David Molinga aliyefunga mawili.

2. Daruwesh Saliboko (Lipuli 5-1 Singida United)

Huyu ni straika wa Lipuli, ambaye ni mchezaji wa pili kufunga magoli matatu kwenye mechi moja msimu huu 'hat-trick'.

Ilikuwa ni Novemba 6 mwaka jana, alipofunga magoli hayo kwenye mechi ambayo timu yake ilicheza dhidi ya Singida United. Katika mechi hiyo Lipuli ilishinda mabao 5-1.

Alifunga kwenye dakika ya 43, 72 na 87, huku Paul Nonga akifunga mawili, Jonathan Daka, aliifungia Singida United bao la kufutia machozi.

3. Obrey Chirwa (Azam 5-0 Alliance)

Mzambia Obrey Chirwa ya Azam FC, naye msimu huu ameingia kwenye kitabu cha kumbukumbu, baada ya kufunga 'hat-trick' yake Novemba 25 mwaka jana kwenye Uwanja wa Nyamagana.

Ilikuwa ni dakika ya nne, 25 na 68, akiipa ushindi timu yake dhidi ya Alliance kwa mabao 5-0.
Mabao mengine ya Azam FC yalifungwa na Shaaban Chilunda, aliyefunga magoli mawili.

4. Kelvin Sabato (Kagera Sugar 3-0 Singida United)

Straika wa timu ya Kagera Sugar, Kelvin Sabato naye alifunga 'hat-trick' yake msimu huu kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba wakati timu yake ikicheza dhidi ya Singida United na kushinda mabao 3-0, Februari Mosi mwaka huu.
Magoli yote yalifungwa na Sabato, dakika ya 26, 88 na 90.

5. David Richard (Alliance FC 4-1 Mwadui)

Hata jina kubwa kwenye ulimwengu wa kandanda nchini, lakini ameingia kwenye rekodi ya kuwa mchezaji aliyefunga 'hat-trick' msimu huu.

Huyu ni David Richard ambaye ni straika wa Alliance. Yeye alifanya hivyo Februari 19 kwenye mechi ambayo timu yake ilicheza dhidi ya Mwadui kwenye Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza.

Alifunga dakika ya tatu, 18 na 83, goli lingine likifungwa na Sameer Vicent, Ottu Samuel akiifungia Mwadui bao la kufutia machozi.

6. Meddie Kagere (Simba 8-0 Singida United)

Mnyarwanda Meddie Kagere ndiye straika pekee ambaye amerejea tena kwenye orodha ya wafunga 'hat-trick' msimu huu, huku wenzie wa msimu uliopita wakiwa bado hajafanya hivyo.

Ilikuwa ni Machi 11 kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam alipofunga 'hat-trick' kwenye mechi ambayo Simba iliifunga Singida United mabao 8-0.

Kagere aliyefunga magoli manne, aliyapata dakika ya kwanza, 25, 41 na 70.
Magoli mengine ya Simba yalifungwa na Deo Kanda aliyefunga mawili, John Bocco na Sharaf Shiboub.

7. Atupele Green (Biashara United 4-0 KMC)

Atupele alifunga magoli yake dakika ya 69, 73 na 90, akiisaidia timu yake ya Biashara United kushinda nyumbani mabao 4-0 dhidi ya KMC. Bao lingine ya Biashara lilifungwa na Justine Omari na kuwa 'hat-trick' ya saba msimu huu wa 2019/20 mpaka sasa.

Habari Kubwa