Hatua za kuelekea Tanzania ya Viwanda

23Sep 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Hatua za kuelekea Tanzania ya Viwanda

NIA ya Rais Dk. John Magufuli katika mikakati yake ya kuboresha uchumi wa nchi, ni kuhakikisha Tanzania inakuwa na uchumi imara. Ni ndoto inayotoa matumaini makubwa kwa Watanzania.

Imani anayoitanguliza siku zote ni kwamba, unapofanikishwa uchumi wa viwanda, ina maana kwamba ni hatua ya kuagana na umaskini kitaifa.

Kutokana na msingi ya uchumi, maendeleo ya viwanda yana uhusiano wa moja kwa moja na sekta ya kilimo, ambayo ni uti wa mgongo wa uchumi wa taifa.

Hivyo, mbali na ajira na kupatikana bidhaa kwa ajili ya masoko ya ndani na nje, kuna maana kubwa katika uchumi wa nchi na matokeo ya jumla ni kwamba na msukumo wa kiuchumi kati ya shughuli moja na nyingine.

Katika lugha ya kiuchumi, hutafsiriwa katika lugha ya kitaalam kama “backward and forward linkage,” kwa maana ya shughuli moja ya kiuchumi inasaidia kusukuma nyinginezo zinazohusiana nayo.
Pia kukua kwa shuguli ya kiuchumi, kunasababisha kuongeza kasi uya shughuli nyingine, hali inayoitwa katika lugha ya uchumi kama ‘multiplier effect.”

Mtazamo kama huo alikuwa nao Rais Julius Nyerere, katika mipango yake ya kwanza ya maendeleo ya nchi, aliyoigawanya katika awamu tatu, kila moja ikichukia miaka mitano kuanzia mwaka 1964, yote ilikuwa na mikakati ya maendeleo ya viwanda.

Kwa mfano, Mpango wa Kwanza wa Maendeleo ya Taifa wa 1964 hadi 1969, ililenga kujenga viwanda vya kuzalisha bidhaa za matumizi kitaifa, ili kuondokana na mfumo uliorithiwa kutoka ukoloni wa ‘Kuzalisha tusichotumia na kutumia tusichozalisha.”

Matokeo yake ndiyo kukawapo ujenzi wa viwanda vingi vya nguo kama vile Sunguratex, Mutex,Urafiki na vingine vingi.
Pia katika Mpango wa Maedeleo ya VIwanda wa kuanzia mwaka 1976wa miaka 20 ulioanza, ulikuwa na mikakati ya kujenga viwanda mama. Hata hivyo, ulififia njiani kutokana na mabadiliko ya kisera kitaifa.

Mageuzi yaliyoshuhudiwa tangu kutoka mabadiliko ya kiuchumi na kisiasa nchini mwaka 1985, ni kwamba ndani ya kipindi cha miaka mitano baada ya mabadiliko ya sheria na sera kushuhudiwa, mengi yalibadilika kuhusiana na kukua kwa sekta binfasi na ubifasishaji wa taasisi za umma zilizokuwa za kibiashara.

Walikaribishwa wawekezaji, kuchukua taasisi hizo za umma zilizoshindwa kujiendesha kwa faida. Kwa bahati mbaya, hata viwanda na taasisi zilizobinafsishwa, nyingi zinafanya vibaya.

Katika azma ya Rais Magufuli katika azma yake hiyo ya kuanzisha viwanda vya umma, ni kwamba, vitajenga vipya kutokana na fedha zipi? Na kama vitajenga viwanda kwa fedha za mkopo, zitarudishwaje?
Pia kuna haja ya kujiuliza, viwanda vlivyopo na viko mikononi mwa wawekezaji, vimewasaidiaje Watanzania?
Kama havijawasaidia vya kutosha, matatizo yanayofanya visiwasaidie Watanzania kwa sasa, yameshatatuliwa ili wawekezaji wengine nao wasirudie makosa hayo?

Kuna la kurejea kwa sasa ni kwamba kuna viwanda na miradi ya wawekezaji ambao inapaswa kuwahakikishia Watanzania soko la uhakika la bidhaa zao, hasa ya kilimo yatakayotumika kama malighafi, ili waiuze kwa faida.

Itakumbukwa kuna wakati viwanda vya miwa viliingia katika mgogoro wa masoko na wakulima binafsi wazalishaji na hata kufanya miwa yao ioze shambani, huku wakulima hao walitumia mikopo kuwezesha uzalishaji.

Baadhi za viwanda hivyo vinavyozalisha sukari, vilifikia hatua ya kuamua kuzalisha sukari vyenyewe ili vipate faida maradufu.
Nao wananchi wakaanza kufanya mabadoliko na kuacha kulima miwa, wakahamia kwenye mazao mengine kama vile mahindi. Ni mazingira yaliyowarudisha nyuma kwenye kilimo cha kimaskini.

Dhana hiyo ndiyo iko kwa wakulima wengine wa mazao kama vile pamba, korosho na wanaohitaji sana viwanda vya ndani, vya kuwahakikishia soko, walime kwa bidii na matumaini.
Hiyo ndiyo inaaminika kuwa njia pekee ya kuwasaidia Watanzania masikini, ambao kwa sehemu kubwa wameajiriwa na sekta ya kilimo.

Hivyo, mtazamo wa wadau wote kitaifa kuhusiana na suala hilo, ni kwamba hata vinapoanzishwa viwanda vya ndani, dhana kuu ni kulinda masoko ya nyumbani, ili wafaidike na jasho lao.

Hilo lilitumika sana katika mipango mitatu ya maendeleo ya nchi kuanzia mwaka 1964, ambayo viwanda vilvyobuniwa wakati huo, vyote viliangalia pia kupatia soko la bidhaa za mkulima wa Kitanzania.

Kwa mfano, viwanda vingi vya nguo vilivyoanzishwa wakati huo, kama vile Tabotex (Tabora), Mutex (Musoma), na Mwatex ya Mwanza vilikuwa ni neema kwa wazalishaji pamba nchini .

Pia kuna viwanda vya nguo vya jijini Dar es Salaam, kama vile Urafiki, Sunguratex, Kiltex na Polytex ya mjini Morogoro.
Kuwa na viwanda vya namna hiyo, kunasaidia kunufaika katima mapato yanayotokana na jasho lao.

Kutokana na kauli ya Rais Magufuli, kuna matumaini kwamba, neema inawajia Watanzania ya ajira na soko la bidhaa zao, kutokana na ujio wa viwanda hivyo.

Kwa ujumla, ujenzi wa viwanda si kitu kidogo. Unahitaji muda na rasilimali nyingine nyingi, kufanikisha hatua inayotarajiwa na umma.

Serikali katika Mpango Miaka Mitano ya Maendeleo uliotangazwa miezi michache mjini Dodoma, ilionyesha kuwapo fedha zinazotengenezwa kufanikisha hilo.

Ni mafanikio ya kuivusha Tanzania kutoka kwenye maisha ya mikopo na misada yenue masharti yanayowauliza kwa sasa na baadaye.

WAWEKEZAJI WANAHITAJIKA?
Kutoa kauli nzito dhidi ya wawekezaji, hakumaanishi kwamba hawahitajiki. La hasha! Wawekezaji wana faida nyingi, kwani kwani iwapo wanawekeza mitaji yao itakuwa na manufaa mengi.

Inapendeza sana, iwapo kwa kiasi kikubwa cha fedha za ndani zitatumika na kutoathiri wafanyabiashara wazalendo.
Kama idadi ya viwanda vitaongezwa kwa wingi katika utekelezaji wa Sera ya Viwanda, matunda yake yanapaswa kulenga sasa na baadaye.