Haya hapa maisha mapya ukusanyaji ushuru wa maegesho magari jijini Dar

14Jan 2022
Maulid Mmbaga
Dar es Salaam
Nipashe
Haya hapa maisha mapya ukusanyaji ushuru wa maegesho magari jijini Dar
  • Kumebainika udokozi, dawa iko jikoni

MFUMO mpya wa kidigitali wa ukusanyaji ushuru wa maegesho ya magari unaotumika mkoani Dar es Salaam, unatajwa kuzaa matunda idadi ya mapato yanayotokana na makusanyo hayo, kuongezeka na kuinufaisha serikali.

Mtoza ushuru katika Jiji la Dar es Salaam, akipiga picha gari kwa ajili ya kuliingiza katika mfumo wa ulipaji ushuru wa maegesho kidigitali. PICHA: MTANDAO

Katika Mkoa wa Dar es Salaam mfumo huo wa ukusanyaji ushuru kidigitali unaoratibiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) ulianza rasmi Desemba Mosi 2021 na unatajwa kuwa na mafanikio kutokana na kusaidia katika kuzuia upotevu wa mapato.

Awali ukusanyaji ushuru wa maegesho ya magari ulikuwa ukiendeshwa kwa mfumo wa kutoa risiti za kawaida ‘risiti za kitabu’ njia inayodaiwa kuwa na mianya mingi ya upotevu wa mapato serikalini, kutokana na baadhi ya watumishi wasio waaminifu kuutumia kama kichochoro cha udanganyifu.

Kwa Mkoa wa Dar es Salaam, mtumiaji wa maegesho anatakiwa kulipa Sh. 500 kwa saa na Sh. 2,500 kwa siku kutoka 4,000.

MAFANIKIO YA MFUMO

Meneja wa Wakala wa Barabara wa Mijini na Vijijini (TARURA) Mkoa wa Dar es Salaam, Geofrey Mkinga, anabainisha kuwa mfumo huo wa ukusanyaji ushuru wa maegesho ya magari kidigitali, unawawezesha kukusanya zaidi ya Sh. milioni 32 kwa siku, huku kiwango cha makusanyo yakitarajiwa kuongezeka.

Anasema mfumo huo mpya wa ukusanyaji mapato ni muhimu katika kuzuia kuvuja kwa mapato, hali inayodhihirika baada ya kuanza rasmi kwa  matumizi ya mfumo huo ambao mapato yanayokusanywa yanaonekana.

“Katika jitihada za uelimishaji hadi sasa tumeyafikia makundi mbalimbali na kuyaongezea uelewa na elimu juu ya mfumo huo wa ukusanyaji wa mapato kidigitali,” anasema Mkinga.

Anakumbusha kuwa katika mfumo huo mmiliki wa chombo cha usafiri anapaswa kulipa ushuru wa maegesho kidigitali baada ya kupatiwa namba ya malipo (control number) na atatumia kumbukumbu hiyo kulipia huduma hiyo, kwa kutumia mtandao wowote wa simu au benki za NMB na CRDB, au kupitia mawakala wa huduma za fedha.

Rai yake ni kwa watoa huduma za maegesho zaidi ya 900 katika mkoa huo kujiepusha na udanganyifu na kutoa lugha chafu kwa wateja, akitahadharisha watakaobainika kukiuka taratibu za ukusanyaji mapato, wataondolewa kazini.

MIONGOZO ILIVYO

Aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu, alishatamka kwamba mtumiaji maegesho atatakiwa kulipa ushuru ndani ya siku 14 badala ya siku saba tangu alipotumia maegesho.

Waziri huyo amefafanua kuwa endapo atashindwa kulipa ndani ya muda huo, atatakiwa kulipa ushuru wa maegesho pamoja na faini ya Sh. 10,000 badala ya Sh. 30,000 zilizokuwa zilitozwa awali, baada ya kufuta adhabu za kiwango hicho cha fedha.

Anaeleza kuwa, miongoni mwa changamoto wazozifanyia kazi ni pamoja na wateja kupatiwa taarifa za kudaiwa ushuru wa maegesho kwa wakati, kupunguza gharama za maegesho, kuongeza muda wa kulipa ambao awali mtumiaji maegesho awali alitakiwa kulipia ndani ya siku saba tangu alipotumia maegesho.

Mkinga anasema, wamebaini udanganyifu unaofanywa na baadhi ya wakusanya ushuru na wateja wanaotumia huduma hiyo. Baadhi ya wakusanya ushuru hufanya mazungumzo haramu na wateja wao wakilipana fedha nje ya mfumo ambazo hazifiki ofisini.

Anasema, baadhi ya wenye magari nao ‘hubambikiwa’ madeni baada ya wakusanya ushuru kuyapiga picha magari na kuyaingiza kwenye mfumo kuwa yanadaiwa, katika maegesho ya TARURA.

Mkinga anafafanua: “Wanamwambia mteja tupe ‘buku’ (Sh. 1000) ili asiipige picha gari yake kwa ajili ya kuiangalia na kuingiza katika mfumo wa malipo kwa njia ya mtandao.

“Kufanya hivi ni kuikosesha mapato serikali na kuwaingiza kwenye madeni wasiostahili, tumeshaijua hii mbinu baada ya kupata taarifa kutoka kwa wateja wema.”

HATUA ZILIZOCHUKULIWA

Meneja huyo wa TARURA anaeleza katika kulishughulikia hilo wanashirikiana na mzabuni na wamewaondoa baadhi yao wamethibitika kujihusisha na udanganyifu huo katika vituo vyao vya kazi kwenye maeneo ya Posta kuelekea Feri-Kigamboni, jijini Dar es Salaam.

Maeneo mengine walipoondolewa ni katika vituo vyao ni Kariakoo, Millenium Tower na Lumumba, akidai wanawafahamu baadhi ya wakala hawaupendi mfumo huo, kwasababu hauwapi mianya mingi ya kufanya udanganyifu.

Anaeleza, katika kukomesha vitendo hivyo, TARURA imeunda mkakati na timu ya wataalamu, inayofanya tathmini na usimamizi kwa kupita katika maegesho yao yote ili kubaini vyombo vya moto ambavyo havijaingizwa kwenye mfumo wa ulipaji.

Pia anadokeza TARURA imebaini kuwapo vitendo hivyo, baada ya kupata taarifa zenye ushahidi kwa nyakati tofauti kutoka kwa wasamaria wema, akitoa wito kwa wananchi kuendelea kuwapa ushirikiano ili kuvikomesha vitendo hivyo alivyovifananisha na uhalifu.

“Tunaomba wananchi wasikubali vitendo au makubaliano yaliyo kinyume na utaratibu kati yao na wakusanya ushuru hao kuhusu ulipaji wa ada za maegesho,” anasisitiza Mkinga.

WAHUSIKA WATHIBITISHA

Mkurugenzi wa Kampuni ya Uwakala ya Asceric Limited inayofanya kazi ya kukusanya ushuru wa ada za maegesho ya (TATURA), Mathayo Nungu, anathibitisha kuwapo kwa baadhi ya wafanyakazi wao wanaokusanya ushuru kujihusisha na vitendo hivyo vya udanganyifu.

“Ni kweli kuna vitendo hivi na tuna wafanyakazi zaidi ya 400 ndiyo maana kuna hii changamoto, si wote wanaweza kuwa waaminifu, tayari wameshafukuzwa kazi zaidi ya wakusanya ushuru 10 baada ya kuthibitika kukiuka utaratibu wa kazi,” anasema Nungu.

Kwa upande wake Ibrahim Said, mtoa huduma ya kutoza ushuru katika maegesho ya magari yaliyoko Mwenge mkoani Dar es Salaam, anakiri kuwapo tuhuma hizo dhidi yao, akisema yao wameshasimamishwa kazi.

“Wanaojihusisha na vitendo hivyo ni baadhi wasiokuwa waaminifu ambao wanaingiwa na tamaa, pasipo kufikiria kuwa wakibainika wataingia matatizo na kuharibu kazi zao. Kama bado kuna ambao wanajihusisha na vitendo hivyo nawasihi waache kwani vinatia doa utendaji wetu,” anashauri Said.

Habari Kubwa