Haya ni magonjwa ya ngono unayotembea nayo bila kujua

09Jun 2018
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Haya ni magonjwa ya ngono unayotembea nayo bila kujua

“UMEKUWA na tatizo la kuwa na vidonda mdomoni mara kwa mara. Ni kama vilengelenge , vina maji. Hutokea hata kwenye kona za midomo.

Vipele midomoni au vidonda vya homa, si ugonjwa mdogo kama wengi wanavyodhani ni matatizo ya virusi vinavyotokana na magonjwa ya ngono. PICHA: MTANDAO.

Wengine huota vidonda hivyo kwenye kidevu na hata puani. Huu ugonjwa ni unaotokana na masuala ya kujamiiana. Yako maradhi mengi ya ngono ambayo watu hutembea nayo lakini hawajijui.”

Hivyo ni vizuri kupima afya usijiamini kwa kuulamba na kubeba simu za bei mbaya mikononi au kuvaa mavazi ya gharama kubwa kwa wanawake lakini una vilengelenge midomoni , ni vyema kupima na kujitibu kwanza.

 

Zama hizo hapa Tanzania yalikuwa yanafahamika kama magonjwa ya zinaa lakini nyakati hizi yanajulikana kama magonjwa ya ngono.Jina linabadilika kuondoa hali ya kuhukumu wagonjwa kuwa wamezini na kuambukizwa maradhi kwani kuna wengine hawakuhusika.

Mabadiliko yamekubalika kutokana na baadhi ya waathiriki kupata maradhi bila kushiriki tendo la kujamiiana bali waliambukizwa pengine kupitia mchakato wa uzazi, kuongezewa damu na hata wakati mwingine kubakwa na kuambukizwa.

Ripoti kutoka Kituo cha Kuzuia na Udhibiti Maradhi cha Marekani (CDC) ya mwaka 2014 / 2015,inaeleza kuwa kumekuwa na ongezeko la takribani asilimia sita za wagonjwa wanaobainika na maradhi ya ngono ikiwa wenye bacteria wanaoitwa ‘chlamydia’ na zaidi ya asilimia 13 ni ile yenye wagonjwa wenye kaswende maarufu kama gonorea.

 

Ripoti inasema pengine idadi ya watu wenye maradhi ya ngono ni kubwa mno kuliko kiwango kile kituo cha CDC kinachowafahamu hii ni kwa wengi hawana wazo kuwa wameambukizwa magonjwa hayo kwa sababu mara nyingi hayaonyeshi dalili wala kuleta hofu zinazomfanya mtu kujichunguza kuwa ana maambukizi.

Ndiyo maana anasema huitwa 'mashambulia ya kimya’ kwa vile hakuna dalili zinazoonekana wala hali ya kustua,” anaeleza daktari Debby Herbenick, mtaalamu wa masuala ya ngono wa Chuo Kikuu cha Indiana.

“Hii inamaanisha kuwa unaweza kuambukizwa lakini usifahamu kuwa unaumwa na kibaya zaidi ukamwambukiza hata mwenza wako.” Mtaalamu Herbenick anaongeza

Baada ya maelezo hayo anataja baadhi ya maradhi ya ngono ambayo unaweza kuambukizwa lakini usiyafahamu, kuwa ni mengi lakini anaanza na kufafanua maana ya maradhi ya ngono.

 

MAGONJWA YA NGONO

Neno maradhi ya ngono au kitaalamu limefupishwa kuwa STI yanamaanisha ugonjwa unaoambukizwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kwa njia ya kujamiiana. Ama hata kwa kufanya ngono za wenza wa jinsia moja na wengine hufanya ngono kwa midomo.

Magonjwa mengine ya ngono huingia mwilini kwa njia ya kuchangia mabomba ya sindano hasa wanaotumia mihadarati. Aidha mama anaweza kumwambukiza mtoto maradhi haya kupitia kumnyonyesha, hivyo yafuatayo ni magonjwa unayoweza kutembea nayo usifahamu kuwa una maambukizi.

 

Kuna aina zaidi ya aina 20 za magonjwa ya ngono mengine yakiwa na dalili zinazoonekana lakini mengine hayaonyeshi dalili japo wenye ugonjwa wanaendelea kuwa waambukizaji na mengine hayana dalili zenye maumivu.

Magonjwa ya ngono kama kisonono na Ukimwi yana athari kubwa kwa maisha ya wanawake na wanaume, japo magonjwa mengine hayana dalili kama hayatatibiwa athari zake ni za kutisha moja wapo ikiwa ni ugumba lakini hata kuleta saratani.

Dalili za magonjwa hayo ni kama vipele (upele), kuwashwa, kujisikia kama mwili kuwaka moto, kutokwa na uchafu hata usaha sehemu za siri kwa wanawake na wanaume. Kuwa na vidonda, malengelenge na maumivu. Aina za magonjwa ya zinaa ambayo unaweza kujihisi kuwa ni mzima wakati umeathirika ni pamoja na:

 

VIPELE

Kitaalamu hivi huitwa ‘herpes’ husambazwa na virusi viitwavyo Herpes Simplex Virus ( HSV) ambavyo vipo vya aina mbili ambavyo vinaweza kuathiri midomo au sehemu za siri . Midomoni au kinywani vinasababishwa na virusi vya HSV-1 na kwenye maeneo ya siri virusi vinavyosababisha huitwa HSV-2.

Dalili kubwa ya vipele hivyo ni pamoja na kuwa na vilengelenge vyenye maji wengine huita vipele vya homa. Japo, hakuna tiba inayofahamika moja kwa moja ya vipele hivyo inavyoshambulia kona za midomo kwenye ‘lips’ lakini wengine hupaka asali, humeza vidonge na hata kupaka dawa za kuvikausha.

Vipele hivyo ni hatari mno kwa watoto wachanga na vinaweza kuwadhuru hata kuwaua hivyo ni muhimu kuwachunguza na kuwatibu wajawazito ili kuzia wasiambukize watoto.

 

GONOREA

Wengine huyaita maradhi haya kaswende ambao ni ugonjwa unaosababishwa na bakiteria waitwao ‘clap,’ dalili za gonorea mara nyingi hazionekani lakini inatokea kuwashwa mara kwa mara sehemu za siri na kutokwa uchafu unafanana na rangi ya kijani au njano.

Kwa upande wa wajawazito iwapo hawatatibiwa haraka iwezekanavyo wanaweza kuhatarisha maisha ya watoto kwani husababisha mimba kuharibika na kama hatatumia dawa kujitibu unaweza kuambukiza na kuambukizwa zaidi.

 

 

CHLAMYDIA

Hawa ni bakiteria wanaoshambulia mfumo wa mkojo, kizazi na hata macho. Ni vimelea maarufu sana huko Marekani hakuna dalili japo kama hutatibiwa utapata maradhi kama PID ambayo ni maambukizi ya via vya uzazi na wanaume wanapata ugumba.

Hata hivyo ni magonjwa yanayotibika kwa urahisi na bila usumbufu ukichunguzwa afya yako na kupata matibabu.

 

KISONONO

Kwa Kiingereza huitwa ‘syphilis’ ni bakiteria ambao wanapoanza kukuletea magonjwa ya zinaa dalili hazionekani lakini wakiingia katika hatua nyingine wanaanza kukusababishia kuchoka kupindukia, homa nyepesi, vipele na maumivu ya misuli.

Kama kisonono hakitatibiwa kinaumiza na kushambulia neva au mishipa ya fahamu na kuleta kifo.

 

PAPILLOMA

Virusi vingine ambavyo unaweza kuwa navyo usijue kuwa una maradhi ya ngono ni Human Papillomavirus (HPV), vinasababisha maambukizo kuanzia vidonda vidogo hadi saratani ya shingo ya kizazi .

Hakuna tiba kwa virusi vya HPV japo chanjo inaweza kuzuia maambukizi yake na kuwaokoa wanawake na saratani ya kizazi ambayo kwa asilimia 70 inatokana na kirusi hicho . Aidha, chanjo hiyo inaweza kutumiwa na wanaume kuwakinga na saratani za sehemu ya haja kubwa na ya uume.

Njia kubwa ya kuambukizwa virusi vya HPV ni kupitia kujamiiana mke na mume hivyo wanaume huambukizwa saratani ya uume.

 

GENITAL WARTS

Hivi ni kama vivimbe vigumu au sunzua baadhi ya makabila kama Wazaramo huviita ‘vikanga’ .Kitaalamu hujulikana kama genital warts chanzo chake ni virusi vya human papilloma (HPV) na husambazwa kutoa kwenye ngozi kupitia ngozi na vinapatikana sehemu za siri za wanawake na wanaume. Vinaota kwenye njia ya haja kubwa pia. Wakati mwingine vinaweza kuwa vikubwa kupindukia na kusababisha kuondolewa na wataalamu wa afya hospitalini.Sunzua hizi mara nyingine hutoweka zenyewe japo kuna zinazobakia na kuendelea kuota.

 

TRICHOMONIASIS

Hili gonjwa la zinaa hutamkwa ‘trikomoniyasis’ au “trich’ ni magonjwa yanayosababisha wanawake kuwa na harufu ya vumba la samaki sehemu za siri, kuwashwa na kujisikia kama kitu kinawachoma eneo hilo. Husababisha kuwa na harufu mbaya inayotoka sehemu za siri na kuingia kwenye nguo zako, kwenye kiti unapokaa na hata kwenye mashuka unayolalia.

Kwa bahati  wanaume ndiyo wanaobeba virusi hivyo na wanawake wanapata pia uchafu unaotoka sehemu za siri pamoja na hali ya muwasho unaosababisha kujihisi kama sehemu za siri zinawaka moto.

Ugonjwa huu unatibika bila matatizo lakini unaajirudia rudia maambukizo yanakuwa rahisi kutokea na kama hali hii ikijitokeza ni lazima wenza wote wawili watibiwe mke na mume bila kutolea visingizo kwa kuwa wanaume wanabeba maradhi haya.

 

HEPATITIS B NA C

Virusi vya Hepatitis B na C vinaonekana na kuishi kwenye damu. Vinaweza kusambaa kutoka mtu kwenda kwa mwingine kupitia kuchangia vitu vyenye ncha kali kama sindano wakati wa kujidunga kwa wanaotumia dawa za kulevya, viwembe lakini hata kuongezewa damu na pia huweza kuambukizwa kwa njia ya kujamiiana.

 

Virusi hivyo husambaa kwa njia ya kujamiiana kwa sababu kwenye mchakato huo ngozi inaweza kuchanika na kusababisha michubuko inayopitisha damu kutoka kwa wenza hao.

Leo hii kuna chanjo ya Hepatitis B na ni muhimu kuipata hasa kama wewe ni mdogo kwani ukiambukizwa unaweza kusababisha saratani ya ini.

Virusi vya Hepatitis B vinaweza kutibiwa lakini inakuwa rahisi kama vikigundulika katika hatua za mwanzo, hata hivyo hakuna chanjo kwa wagonjwa wa hepatitis C na ina uhusiano mkubwa na saratani ya ini kuliko ilivyo kwa virusi vya Hepatitis B. Yote hayo huambukizwa kwa njia ya ngono.