Hii hapa shida ya kuvimba koo inavyotibiwa

06Aug 2020
Jackson Paulo
Dar es Salaam
Nipashe
Hii hapa shida ya kuvimba koo inavyotibiwa
  • • Yawanasa, watoto hadi miaka 25

UNAIJUA ‘tonsiltis’? Ni hali ya kuvimba tezi za kooni ambazo katika utaalamu wa kawaida inatamkwa ‘tonsils.’ Hiyo ni mishipa yenye mwonekano wa umbo kama yai na hukaa pande mbili nyuma ya koo.

Mara nyingi kuvimba tezi huko kunasababishwa na uvamizi wa virusi au bakteria. Matibabu yake sahihi yanategemea chanzo cha tatizo, yaani iwapo ni kwa bakteria au virusi. Ni muhimu mtu akapimwa kujua chanzo halisi, kabla hajapatiwa matibabu stahiki.

Kuna wakati upasuaji unafanyika kuondoa kabisa matezi, lakini unafanyika tu pale anapopendekeza daktari na mara nyingi inakuwa pake tatizo linajirudia kila mara.

Pia, katika namna tatizo linaposhindwa kupona kwa kutumia dawa za kawaida au tezi linaposababisha matatizo mengine makubwa mwilini.

DALILI ZAKE

Kuvimba kwa tezi mara nyingi inawaathiri zaidi watoto wenye umri mdogo (ambao hawajaanza shule) na walio katika ujana umri unaokaribia utu uzima (miaka 15-25).

Dalili anazopata ni pale ‘tonsilitis’ zinakuwa nyingi, zikiwa na sifa ya kuvimba tezi, kuwa na rangi nyekundu; kuhisi maumivu wakati wa kumeza chakula au kushindwa kumeza chakula.

Mengine inatajwa kuwa ni maumivu ya koo, utando mweupe au wa njano sehemu ya matezi, kupata homa, kukua kwa vitoki ‘lymph nodes’ eneo la shingo na sauti kukwaruza.

Pia, kuna suala la mtu kutokwa harufu mbaya mdomoni wakati wa kupumua, shingo kukakamaa na maumivu ya kichwa.

Kwa watoto wadogo wasio na uwezo wa kueleza hisia zao au hali wanayojisikia, huweza kuonekana wakiwa na dalili kama kutokwa na mate ‘udenda’ bila ta kujizuia, kukataa au kugoma kula, pamoja na kukasirika kila mara pasipo sababu yoyote.

Mara nyingi ‘tonsillitis’ inasababishwa na uvamizi wa virusi, japokuwa uvamizi wa bakteria pia unaweza kusababisha tatizo hilo. Bakteria ambaye mara nyingi husababisha ‘tonsillitis’ na maumivu ya koo anajulikana kama Streptococcus pyogenes.

KUSHAMBULIWA TEZI

Kwa kawaida tezi (tonsils) ni sehemu ya kwanza ya kinga ‘ulinzi’ wa mwili dhidi ya bakteria au virusi wanaoingioa mwilini kwa njia ya kinywa.

Kutokana na tezi kuwapo katika eneo hilo la kinywa, huangukia hatari ya kupata madhara ya kila mara.

Hata hivyo, kazi ya kulinda mwili inayofanywa na tezi za kooni hupungua kadri mtu anapoingia katika utu uzima na inatajwa kuwa sababu inayochangia kupungua madhara.

Nafuu kwa watu wazima iko juu, tofauti na watoto wadogo ambao tezi zao hutumika zaidi kwa ajili ya ulinzi wa mwili.
Zipo hali mbalimbali zinazosababisha mtu kuwa hatarini kupata tatizo hilo la tonsils.

Pia, anaeleza tatizo linawaangukia zaidi watoto na mara chache kwa wenye umri chini ya miaka miwili.

Kwao watoto wenye umri kati ya miaka mitano hadi 15, hupata tatizo hilo kutokana na mashambulizi ya bakteria na ile inayosababishwa na virusi, huwapata zaidi wenye umri chini ya miaka mItano.

VIJIDUDU NA BAKTERIA

Mara nyingi watoto wadogo waliopo shule hugusana na wenzao, hali inayowawekea hatari kubwa ya maambukizi. Lakini, watoto mara nyingi huweza kugusana na vitu hatari vyenye vijidudu na kupata matatizo.

Madhara yanatokea kwenye tonsils, pale mtu anapopatwa na matatizo, hasa mazingira yanapokuwa sugu.

Ni madhara yanayojumuisha kupumua kwa shida hasa anapokuwa usingizini, kusambaa kwa maambukizi pembezoni mwa tezi (tonsillar cellulitis) na maambukizi yanayochangia kukusanyika usaha nyuma ya tezi ‘peritonsillar abscess’.

MATIBABU TEZI

Katika kutibu tatizo uvimbe wa tezi, zipo aina tatu za matibabu zinazotumiwa, yaani; utumiaji wa dawa, matibabu ya kufanyika nyumbani bila kutumia dawa na matibabu kwa njia ya upasuaji.

Iwapo tatizo la kuvimba kwa tezi ama limesababishwa na virusi au bakteria, kuna njia zinazoweza kufanyika nyumbani na kusaidia kumfanya mgonjwa kupata nafuu, akajihsi vizuri kiafya.

Iwapo chanzo cha kuvimba tezi kimebainika ni virusi, basi matibabu ya nyumbani huwa ndio sahihi zaidi na daktari hatakupangia dawa za bakteria (antibiotics).

Mara nyingi kwa njia hii ya matibabu ya nyumbani mtoto huweza kupata nafuu au kupona baada ya muda wa siku saba hadi kumi.

Njia zinazoweza kutumika nyumbani pale chanzo cha kuvimba tezi kimebainika kuwa ni virusi, hatua zifuatazo:

• Kupumzika; iwapo mgonjwa ni mtoto, mzazi anapaswa kumshawishi apate muda wa kulala vizuri.

• Kunywa maji ya kutosha yanayompatia mwana maji ya kila mara, ili kusaidia kuzuia koo lisiwe kavu, hata akajihisi vibaya.

• Kusukutua kwa kutumia maji yenye chumvi, kunapaswa kufanyika kwa kuandaa maji yaliyochanganywa na chumvi, walau kijiko kimoja cha chai kwa glasi moja ya maji ya vuguvugu, kisha sukutua maji hayo kwa muda mfupi na kutema. Hiyo inasaidia sana kuleta nafuu kwa mgonjwa.

• Kutibu maumivu na homa; mgonjwa anapaswa kujadili na daktari kuhusu utumiaji dawa za kupunguza maumivu, ili kusaidia kumaliza maumivu ya koo au kudhibiti homa.

Hata hivyo, homa ndogo zisizoambatana na maumivu ya koo hazihitaji matibabu yoyote.

MATUMIZI DAWA

Iwapo kuvimba tezi kumesababishwa na bakteria, daktari humpangia mgonjwa dawa za antibaiotiki na iliyozoeleka ni aina ya penicillin. Wapo watoto wenye aleji ya dawa hizo na daktari anampangia mgonjwa dawa nyingine tofauti.

Hata hivyo, ni muhimu kwa mgonjwa kumaliza dozi hata kama dalili za zimeshatokomea. Kushindwa kumaliza dozi kunatajwa kusababisha tatizo kubwa zaidi, bakteria kusambaa na kuvamia sehemu nyingi mwilini.

Kusambaa bakteria, kunaweza kumsababishia mtoto hatari kubwa ya tatizo la kuvimba figo, ijulikanayo kitaalamu ‘kidney inflammation.’

TIBA UPASUAJI

Inaelezwa kwamba, iwapo mtu anaandamwa na tatizo la kujirudia kuvimba tezi au dawa za kutibu bakteria kushindwa kufanya kazi vizuri kwa mgonjwa, basi upasuaji wa kuondoa kabisa tezi ‘tonsillectomy’ huweza kuwa njia bora zaidi la kumaliza tatizo.

Kuna vigezo kadhaa hufikiwa na unahitaji, hata upasuaji kwa mwenye shida ya koo kufanyika. Mosi, ni mtu anapopata tatizo la kuvimba tezi zaidi ya mara saba katika kipindi cha mwaka mmoja.

Pili, ni pale kuvimba tezi kunamsababishia mgonjwa kuziba njia ya hewa na mtu anashindwa kupumua vizuri anapokuwa amelala.

Tatu, iwapo mgonjwa anapata tatizo kubwa la kumeza chakula na nne, mgonjwa anapata usaha kwenye sehemu ya tezi ambao hauonyeshi dalili ya kupona, hata pale mtu anapotumia dawa za anti-bakteria.

KUIZUIA TONSILS

Virusi na bakteria vinavyosababisha tatizo la kuvimba tezi, huambukizwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda mwingine. Kwa maana hiyo, njia bora ya kuzuia ni kuiweka katika hali ya usafi kila wakati.

Mzazi, anapaswa kumfundisha mwanawe mambo yafuatayo:

• Kunawa mikono mara kwa mara, haswa baada ya kutoka chooni na kabla ya kula.

• Kuepuka kushirikiana chakula, glasi za kunywea maji, chupa za maji au vyombo vingine vya kulia chakula.

•Mwandishi anapatikana kwea barua pepe: [email protected]

Habari Kubwa